Makala

AKILIMALI: Kazi ya uchakataji macadamia yamvunia hela

July 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MAGDALENE WANJA

ALIPOWASILI nchini Kenya, Mohammad Khan alikuwa na madhumuni ya kutafuta biashara ambayo ingemwezesha kupata riziki.

Hata hiyo, hakujua ni biashara ipi ambayo ingemfaa kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuwa nchini.

Alianza kufanya utafiti jijini Nairobi na maeneo ya karibu na kujifahamisha kuhusu mila na desturi za wakazi.

Katika pilkapilka hizo, alipata kuwa ya Thika Superhighway ilikuwa ikijengwa kwa mara ya kwanza.

“Nilijiambia kuwa ikiwa serikali imeamua kuijenga barabara hii kuu, lazima barabara hii inaunganisha jiji la Nairobi na mahali ampapo kuna biashara ama mapato mazuri. Niliamua kuifuata barabara hiyo,” alisema Bw Khan.

Bw Khan alikuwa amesafiri kutoka Bangladesh alikozaliwa.

Kulingana na Bw Khan, nchi hiyo ina idadi kubwa ya watu na hiyo watu wengi wanaugua maradhi ya aina mbalimbali.

“Mbali na kupata faida, nilitaka biashara ambayo ingekuwa na manufaa ya kiafya hasa kwa watu niliowaacha nyumbani,” aliongeza Bw Khan.

 

Alipofika Mjini Thika, alipata kuna baadhi ya viwanda ambayo vilikuwa vikijihusisha na kutegemea malighafi ambayo ni mavuno ya shambani kama vile kahawa, majanichai na vyakula mbalimbali.

Hata hiyo, alivutiwa na viwanda vidogo vilivyokuwa vikijihusisha na macadamia.

“Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuona macadamia na nilitaka kujua zaidi kuyahusu,” akasema Bw Khan.

Baada ya kufanya utafiti zaidi, aligundua kwamba hii ndio biashara iliyomfaa zaidi.

Aliamua kuanzishwa kiwanda chake amvapo angejihusisha na ununuzi wa macadamia kutoka kwa wa kulima na kupakia.

Miaka tisa baadaye, biashara hio imekuwa na manufaa makuu kwake na familia yake haswa kwa wale wenye ugonjwa wa kisukari.

“Macadamia ni muhimu kwa afya hasa kwa wale wenye maradhi ya kisukari. Hii ni kutokana na utafiti wangu mwenyewe na ule wa wataalam,” aliongeza Bw Khan.

Bw Khan hupata macadamia kutoka kwa wa kulima kutoka sehemu mbalimbali nchini kama vile Embu, Meru, Nyeri na Kirinyaga.

Ananuia kutengeneza maziwa ya macadamia na mafuta ya kujipaka, huku tayari akiwa ameanza kupakia mafuta ya kupikia kutoka kwa macadamia.

Bw Mohammad Khan akiwa katika kiwanda chake cha kutayarisha Macadamia mjini Thika. Picha/ Magdalene Wanja