AKILIMALI: Kiangulio cha kisasa shuleni
NA RICHARD MAOSI
Huwezi kufikia hatua ya kuwa mkulima mkubwa endapo huna mtambo wa kuangulia mayai, na baadae kuyatotoa kwa urahisi, pia katika kilimo biashara inashauriwa kuwa mkulima asisite kutumia masine ya Incubator.
Mashine yenyewe inaweza kutumia nishati ya umeme au sola kuongezea mayai joto, lakini mara nyingi wakulima huona kuwa ni bora kutumia sola ili kujiepusha na changamoto za kukatika kwa umeme kila mara bila kukusudia.
Sasa mayai yanaweza kuangua vifaranga baada ya siku 21 tu kwa hisani ya mtambo huu, bila kuatamiwa na kuku, hii ni kulingana na ufugaji wa kisasa ambapo teknolojia imechukua nafasi ya kuboresha ufugaji.
Uvumbuzi huu utasaidia kukidhi mahitaji ya kimsingi, hasa katika maeneo ambapo mayai yanahitajika kwa wingi, kulisha idadi kubwa ya watu kwa mfano wanafunzi wanaohitaji lishe ya protini zaidi ya mara moja kwa wiki.
Ishara tosha kuwa teknolojia katika ulingo wa ufugaji wa kuku imepiga hatua ya kupigiwa mfano, hususan kwa wakulima waliojikita katika kilimo biashara mashinani na mijini,wakilenga soko pana.
Mwalimu Shikuku Edwin kutoka shule ya wasichana ya Njoro Precious kaunti ya Nakuru anasema shule yake iliona haja ya kutumia mtambo wa artificial incubator kuangua mayai mengi kwa wakati mmoja.
Walitaka wanafunzi wajumuishiwe protini kwenye lishe yao ya kila siku, kwa gharama nafuu,aidha walihusisha mradi wenyewe kama nyenzo ya kufundisha somo la zaraa na Bayolojia katika vipindi vya masomo yao.
Vilevile shule ilitaka kufanya utafiti kuhusu aina mbalimbali ya ndege wanaoweza kufanya vyema, katika eneo la Njoro viungani mwa mji wa Nakuru nao kuku wa kutaga mayai wakaibukia kuwa bora zaidi.
Kwanza walilenga kupunguza idadi ya kuku watakaohitajika kuatamia mayai kwa muda fulani,kabla ya kuangua vifaranga.
Mtambo wenyewe ni wastani na unaweza kubeba mayai 500 kwa awamu moja, na huchukua wiki tatu(siku 21), kuangua vifaranga bila uangalizi wa usimamizi wa shule ,muradi kiwango sahihi cha joto kuweko.
Kufikia sasa shule inamiliki zaidi ya kuku 220 ambapo 150 hutaga mayai kila siku,Hii ina maanisha kuwa kwa wiki moja mambo yakiwa mazuri shule inaweza kuvuna hadi mayai 950, yanayotumika kulisha wanafunzi.
“Wakati wa likizo mayai hayo huuzwa sokoni, na fedha zinazopatikana hutumika kuongeza akiba ya vitabu kwenye maktaba na kuboresha maabara na miundo msingi ya shule,” mwalimu Edwin akasema.
Ambapo shule inaweza kuhifadhi hadi 10,000 kwa wiki ambazo ni sawa na 40,000 kila mwezi, takriban 160,000 kila muhula ,kipato ambacho kimebadili hali halisi ya matumizi ya fedha shuleni.
Mwalimu Edwin aasema kuku wanahitaji lishe ya kawaida ili kupatia mayai kiwango sahihi cha madini yanayostahili kama vile Calcium (madini yanayofanya gaagaa la mayai kuwa gumu).
Wakati mwingine ni jambo la busara kuchanganyiwa lishe hii na ile inayopatikana viwandani ili kuhakkikisha kuku wanachukua muda mfupi kokomaa.Aidha shule hutumia sukumawiki kama ziada ya lishe za viwandani.
Aidha ili kukabiliana na mkurupuko wa maradhi,anashauri kuwa kuku wanastahili kunywa maji safi na kutengenezewa sehemu safi na salama ya kukaa ili mayai yasije yakaanguka na kuvunjika wala kudonwa kabla ya kuangua.
Aliongezea kuwa kuna masine nyinginezo kubwa za incubator zinazoweza kubeba mayai 1400 na zile ndogo zinazoweza kukidhi mahitaji ya wakulima wadogo mashambani.
“Mtambo wa Incubator imesaidia shule ya Njoro Precious kuyalinda mayai yasije yakaharibika yanapochelewa kuanguliwa na kuku pindi tu baada ya kutagwa,”akasema.
Anasema kuwa mtambo wenyewe umesaidia kupunguza msongamano wa kuku ndani ya kibanda ambao labda ungesababisha maambukizi ya maradhi kutoka kwa kuku mmoja hadi mwingine kwa sababu wao hutangamana na pia pangehitajika nafasi kubwa ya kuatamia,wanapopigania nafasi ndogo.
Mtambo huu unaweza kuangua mayai ambapo yote hutumika kuwalisha wanafunzi.Kwa upande mwingine wao pia hushiriki katika mradi wa ufugaji kama vile kuwalisha mara mbili kwa siku.
Mwalimu Edwin alifichulia Akilimali kuwa kuku wanaweza kutaga mayai mara mbili kwa siku kulingana na lishe ambayo wamekuwa wakipatiwa ya mkulima bila kusahau chanjo.
Aidha wanastahili kunywa maji ya kutosha na tena yawe safi kila wakati , mbali na kupatiwa utulivu wa mawazo.Kuku wanastahili kufugwa mbali na mijengo na sehemu zenye kelele kama vile viwanda ili kuwapunguzia msongo wa mawazo na kuwapatia nafasi nzuri ya kutaga mayai.
Mwalimu huyu anaona kuwa itakuwa ni jambo la busara kwa mradi kama huu kuigwa na shule nyinginezo, hasa zile zinazopatikana mashinani kutokana na ufaafu wake wa kupunguza gharama ya kununua mayai au nyama kutoka soko la nje.
Aidha anawashauri wazazi kuwafundisha watoto wao stadi ya ukulima mbali na kujitafutia elimu za shuleni kwa sababu siku za baadae wanaweza kuwa watu wa kujitegemea katika sekta ya kilimo.