• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
AKILIMALI: Kifaa kipya kinachotatua changamoto nyingi za ufugaji kuku

AKILIMALI: Kifaa kipya kinachotatua changamoto nyingi za ufugaji kuku

Na RICHARD MAOSI

TEKNOLOJIA ya kisasa imekuja na mbinu nyingi za kuboresha ufugaji, hasa kwa wakulima wadogo na wakubwa waliojikita katika kilimo biashara.

Mfano mzuri wa kupigiwa darubini ni ule wa kufuga kuku, ambapo njia mbadala imezinduliwa baada ya wakulima kushirikiana na kundi la akina mama la Kenya Women kubuni kifaa cha kulinda ndege.

Ufugaji wa kuku ni chanzo cha kumwongezea mkulima mapato hasa wale wanaokaa mashambani.

Aidha bidhaa zinazotokana na kuku zinaweza kumpatia mkulima faida kubwa, endapo atazingatia taratibu zote na kukabiliana na changamoto.

Ufugaji kuku wa nyama na mayai ni fursa nzuri ya ajira kwa vijana wengi waliosoma na kuhitimu lakini hawajapata kazi kwa sababu ya ongezeko la soko kubwa la mahitaji ya bidhaa hizi.

Akilimali ilitembelea Maonyesho ya Kilimo ya Nakuru na kutangamana na shirika la Kenya Women ambalo limevumbua kifaa cha kisasa kinachoweza kutimiza mahitaji yote ya ufugaji.

Kulingana na mkurugenzi wao Micah Makori mkulima anaweza kufanya shughuli zake bila kutumia wakati wake mwingi kuwaangalia kuku wake.

Kifaa hiki kina sehemu ya kuwalisha kuku, kuhifadhi mayai na mzunguko wa maji unaohakikisha kuwa ndege wako hawapungukiwi na maji wala kiwango sahihi cha lishe.

Micah anasema kuwa wakulima wengi wanafaa kuhimizwa wawe wakitembelea maonyesho ya kilimo, kila wakatii ili wajiongezee ujuzi katika sekta ya ufugaji.

Alieleza kuwa mfugaji hawezi kutumia wakati mwingi kuwakagua ndege wake na badala yake atumie wakati wake kufanya kazi nyinginezo za kujiongezea kipato.

Kuku wa gredi

Micah alifichulia Akilimali kuwa kuku wa gredi ndio wanalengwa sana, kwa sababu hawana hulka ya kutembea kila sehemu kama wale wa kienyeji wasioweza kutulia sehemu moja.

Kifaa hiki kimegawanywa katika sehemu ya vyumba vidogo vilivyozungukwa kwa waya na kila sehemu inaweza kubeba kuku wanne bila kusababisha msongamano.

Anasema sio lazima mkulima awe na sehemu ya ardhi kufugia ndege wake, ila jambo la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa sehemu ya kufuga inapata usalama wa kutosha.

Kifaa hiki kimegawanyika katika sehemu ya kuweka lishe, sefu za kuhifadhi mayai na paipu za kuzungusha maji hadi kwenye makasha yaliyotengwa kimakusudi kubeba maji.

Vilevile kuku hawawezi kula mayai yao pindi yanapotagwa kwa sababu huingia katika sehemu tofauti ambayo haiwezi kufikika hata wakijaribu kudona namna gani.

“Kwa kuwa kifaa hiki kimeinuliwa sio rahisi kuku kupata maradhi mara nyingi maana, hawapati fursa ya kukanyaga ardhi iliyojaa vimelea na uchafu wa aina mbalimbali,” akasema Micah.

Micah anasema ufugaji wa kuku unaweza kumpatia mkulima faida nyingi kwa sababu hutoa ajira, mbolea na wakati mwingine kuzalisha nishati ya kawi.

Micah anaamini kuwa kwa kigezo hicho Wakenya wengi hawawezi kukwepa jukumu la kutekeleza kilimo kwa sababu bado ni uti wa mgongo kwa uchumi wa Kenya.

Micah Makori, mtaalamu wa ufugaji wa kuku aonyesha wateja kifaa cha kufugia kuku katika Maonyesho ya Kilimo ya Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Kulingana naye kuku wa kutaga mayai huwa tayari kuanzia miezi minne hadi tano tangu waanguliwe.

Kipindi cha kuku kutaga mayai aghalabu huwa ni mwaka mmoja na nusu bila kukoma katika kipindi chote cha maisha yake, ambayo ni takriban wiki 90.

Katika upana wa mita 20 mraba mkulima anaweza kufuga zaidi ya kuku 1,200, ambao kwa siku wanaweza kumpatia zaidi ya 24,000.

Anashauri kuwa kuku akitunzwa vizuri anaweza kutaga baina ya mayai mawili kila siku lakini hali hii hupungua kadri ya umri wa kuku unavyosonga.

“Kuku wa mayai huuzwa mara tu kipindi chake cha kutaga mayai kinapofikia tamati na anaweza kutumika kama kitoweo,” alisema.

Micah anaona kuwa ni jambo ya heri endapo wakulima wengi watajifundisha umuhimu wa kuhudhuria semina au taasisi za kuwapokeza mafunzo kuhusu utunzaji bora.

Mtu yeyote mwenye kipato cha chini au kile cha kadri anaweza kujifundisha ujasiria mali kwa kutumia ujuzi wa kufuga kuku wa gredi kama hatua ya kwanza kujitafutia kipato.Anahimiza kuwa ni vyema kwa mkulima kabla ya kuanzisha mradi wa kufuga kuku wa mayai kuzingatia kanuni muhimu kwanza ikiwa ni kuchagua vifaranga bora, chakula, kudhibiti mkurupuko wa maradhi na kibanda safi cha kuwafugia.

Hii ndio sababu kundi la akina mama la Kenya Women kwa ushirikiano na wakulima walijizatiti kuvumbua kifaa hiki cha kisasa ambacho kinayaafikia mahitaji hayo yote.

Cha msingi mkulima atahitajika kuhifadhi kumbukumbu zote za ufugaji, ili kuelewa endapo mradi wake unampatia faida ama hasara.

“Watu wengi siku hizi wameingia katika ufugaji kuku wa kisasa kwa sababu ya ongezeko la watu mijini ambao wanafanya kiwango cha shamba kukosekana,” aliongezea.

Anawashauri vijana kujiunga na sekta ya ufugaji ili waibadilishe mifumo ya zamani na kuingilia mifumo ya kisasa inayozingatia teknolojia.

You can share this post!

Ahukumiwa kifo kwa kuua mwanamke aliyemkataa

MIRADI PWANI: Minazi mipya inayokomaa baada ya miaka mitatu...

adminleo