Makala

AKILIMALI: Kikundi chafaidi kwa kufuga kuku wa kienyeji mjini

October 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na DIANA MUTHEU

KULINGANA na ripoti katika magazeti humu nchini, zaidi ya watu milioni moja walipoteza kazi zao tangu janga la corona liikumbe Kenya.

Hata hivyo, kwa wakati huu, watu wengi wametafuta mbinu mpya za kujichumia riziki, kwa kuwa wengi wana familia zinazowategemea.

Katika mtaa wa mabanda wa KaaChonjo, Tudor, Kaunti ya Mombasa, kikundi kimoja kimejitahidi kufuga kuku wa kienyeji kwa manufaa ya wanachama waliopoteza kazi kwa sababu ya athari hasi za janga la corona.

Kikundi hicho kiitwacho KaaChonjo Excel kwa sasa kina wanachama 23 ambao wengi wao ni vijana wadogo lakini wenye maono makubwa.

Kilianza shughuli zake mwaka wa 2018 lakini lilianza kutia fora Machi 2020 baada ya baadhi ya wanachama kupoteza kazi zingine walizokuwa wakifanya.

Jinsi kikundi hiki kinafuga kuku hao, kinaleta mwonekano wa kuwa mtu anaweza kufanya shughuli za ufugaji hata katika maeneo ya mijini.

Wamejenga vibanda katika nafasi ya urefu wa mita kumi na upana wa mita moja, ambapo kuku hao wanafugwa na vyakula vyao kuhifadhiwa.

Akizungumza na Akilimali mwenyekiti wa kikundi hicho, Stephen Okumu, 24, alisema kuwa hawakununua bidhaa zozote kutengeneza vibanda hivyo.

“Tulikusanya mbao, vyuma, nyaya, misumari na vitu vingine vingi tulivyovihitaji kutengeneza vibanda hivi, huku mtaani. Katika kikundi chetu, tuna watu ambao wana ujuzi tofauti na walitusaidia kuvitengeneza,” akasema kijana Okumu huku akiongeza kuwa baadhi ya kuku huachiliwa wakatembea pale mtaani, kama wale wa mashambani.

Pia, sehemu za kuku kutagia mayai zimetengenezwa kwa bidhaa za kawaida kama vile mtungi wa maji wa lita 20 uliokatwa au katoni ya maziwa au bidhaa zingine, changarawe na nguo zilizochanika.

Vifaa vya kuku hao kulia vyakula vyao na kunywea maji pia vimetengenezwa kutoka kwa bidhaa za kawaida kama vile bakuli za chuma na chupa za plastiki.

“Nia yetu pia ni kuhakikisha kuwa mazingira yetu ni safi,” akasema.

Tayari, wana kuku karibia 100 na wamejisajili ili kuhakikisha kuwa wanaweza kupata mikopo inayotolewa kwa vikundi.

Okumu anasema kuwa wanaendelea kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu kuhusu jinsi ya kulea kuku hao na dawa zinazofaa kutumiwa.

“Vifaranga wakianguliwa, huwa tunawapa unga wa mahindi na maji, kisha wakifika miezi moja unusu tunawanunulia chakula kinachojulikana kama ‘starter’. Kuku wetu hulishwa mara tatu kwa siku na pia maji hubadilishwa mara tatu ili kuepuka magonjwa yanayosababishwa na uchafu,” akasema Okumu huku akiongeza kuwa kuku wakubwa hulishwa mabaki ya vyakula, nyasi na mboga.

Mtungi uliokatwa kwa minajili ya kuku kuatamia mayai. Picha/ Diana Mutheu

Msemaji wa kikundi hicho, kijana James Malova anasema kuwa wamepanga ratiba ya wanachama kuhudumia kuku hao.

“Vibanda hivyo lazima visafishwe kila siku na mayai yaliyotagwa yachukuliwe ili yasivunjwe. Pia, lazima kuweko na mtu wa kuwachunga kuku hao wasiibiwe manake vibanda vimejengwa kando ya njia,” akasema Malova.

Malova anasema kuwa soko lao kuu limekuwa wenyeji katika mtaa huu lakini katika maono yao wanalenga kuwa kikundi kitakachofuga kuku wa kienyeji wakilenga wakazi katika kaunti hiyo.

“Tunatazamia kuwa na kuku zaidi ya 1,000 ifikapo katikati ya mwaka 2021,” akasema.

Kulingana na Malova, yai moja wanaliuza kwa Sh30, huku kuku akiuzwa kwa Sh1,000 na zaidi.

“Pesa ambazo tumepata kwa kuuza mayai tumeweza kuwasaidia wanachama ambao walipoteza kazi zao. Hata hivyo, mayai mengi uhifadhiwa ili tuweze kuzalisha vifaranga wengi. Pia, kila mwezi huwa tunachanga Sh500 na tumefungua akaunti yetu na fedha hizo ni za kununua vyakula na dawa za kuku hawa,” akasema Malova.

Anataja baadhi ya changamoto kuwa ukosefu wa nafasi ya kutosha na fedha za kuwasaidia kujenga vibanda za kisasa. Pia, utovu wa usalama ni changamoto na baadhi ya kuku wao wameibiwa.

“Magonjwa ya kuku pia ni changamoto lakini huwa tunashauriana na wataalamu kujua ni dawa gani zinafaa,” akasema.

Malova alisema kudumisha maelewano katika kikundi, wametengeneza Katiba yao ya kuwaongoza na wanaweka rekodi ya bidhaa zinazotumika ili kuhakikisha kila mwanachama anafaidika, na hakuna wizi wowote wa fedha.

“Maono yetu ni kufuga kuku wa kienyeji zaidi ya 10,000,” akasema Malova.