Makala

AKILIMALI: Kilimo cha mboga asili aina ya mnavu

July 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

MNAVU ni mboga asili ya majani inayoenziwa na wengi nchini Kenya na katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ni mboga ya kienyeji yenye ukali wa aina yake, lakini unaovutia walaji.

Kuna wanaoipika ikiwa pekee, wengine kwa kuichanganya na kunde, mchicha au spinachi, ama na mboga nyingine ile.

Ili kuongeza ladha, baadhi hutia matone ya maziwa.

Vilevile, hutiwa shahamu; krimu ya maziwa.

Mboga hii imesheheni Vitamini A na C, madini muhimu katika mwili wa binadamu.

Damacline Nyaboke ni mkulima wa mnavu eneo la Kasarani Nairobi, na anasema ni miongoni mwa mboga rahisi mno kupanda na kutunza.

Bi Nyaboke pia hukuza mchicha, saga na kansella, zote zikiorodheshwa kama mboga za kienyeji.

Mkulima huyu anasema mnavu hukua upesi, ikilinganishwa na mboga kama sukuma wiki na kabichi.

“Mboga aina ya mnavu haina kikwazo cha upanzi na kutunza,” anasema Bi Nyaboke.

Miche yake huandaliwa katika kitalu, hatua inayochukua wiki tatu hadi nne. Kuna kampuni aina mbalimbali zinazozalisha mbegu za mnavu.

Simlaw Seeds ndiyo tajika nchini katika shughuli hiyo.

Wataalamu wa kilimo wanahimiza wakulima kutumia mbegu bora ili kupata mazao ya kuridhisha. Aidha, zinapaswa kuwa zimeidhinishwa na Kephis na Karlo, taasisi zinazoangazia masuala ya kilimo nchini.

Pia, pembejeo; mbegu, mbolea na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, zinapaswa kuwa na stempu ya halmashauri ya ubora wa bidhaa nchini (Kebs).

“Kuna pembejeo bandia zilizosheheni sokoni, mkulima awe makini anaponunua,” anashauri Bi Emmah Mwenda, mtaalamu kutoka HM. Clause, kampuni inayotafiti na kuzalisha mbegu za mboga, nyanya, matikitimaji na pilipili mboga.

Kulingana na mkulima Nyaboke ni kwamba taratibu za upanzi wa mnavu ni sawa na za mchicha, kansella au saga.

“Andaa mashimo ama mitaro yenye urefu wa karibu sentimita 10 kuenda chini,” aelezea mkulima huyu.

Anapendekeza kipimo cha laini ya mashimo au mtaro hadi nyingine kiwe kati ya sentimita 30-40.

Mkulima huyu mwenye tajiriba ya kulima mboga za kienyeji kwa miaka mitatu sasa anasema miche ipandwayo iwe na karibu majani sita, na mche uwe na urefu wa sentimita 10-15.

“Kwa kuitazama kulingana na urefu wake utabaini ikiwa i tayari kwa upanzi,” anaelezea.

Kitalu kinapaswa kumwagiliwa maji kabla ya kuing’oa.

Mkulima anashauriwa kufanya shughuli za upanzi majira ya jioni au wakati anga limetanda mawingu yanayozima makali ya miale ya jua.

Mbolea inaweza kuchanganywa na udongo kabla ya mitaro au mashimo kuandaliwa. Kuna wanaotimua baada ya kuyaandaa.

“Mbolea inayopaswa kutumika ni iliyoiva sawasawa. Pia, inaweza kuchanganywa na fatalaiza,” asema Bw Timothy Mburu, mtaalamu wa kilimo na pia mkulima.

Pawepo nafasi ya kutosha baina ya miche

Miche ya minavu ipandwe na kupewa nafasi ya karibu futi moja kutoka mche mmoja hadi mwingine.

Sababu hasa ya kipimo hicho ni kuruhusu miale ya jua kufikia ardhi kwa ajili ya mizizi, na pia kuyapa nafasi majani ambayo ndiyo mboga kukua huru.

Maji ni kiungo muhimu katika kilimo, na endapo si msimu wa mvua minavu inyunyiziwe asubuhi na jioni.

Makwekwe ni miongoni mwa changamoto zisizokosa kuepuka na huleta ushindani mkali wa lishe; maji na mbolea. Palizi huyadhibiti badala ya kutumia dawa.

Kwa kuwa ni mboga ya kienyeji haja ipo kuzingatia kilimo-hai (organic farming) kwa kukumbatia mfumo wa asili kufanya zaraa. Hii ina maana kuwa fatalaiza inayotumika kustawisha sucha isiwe yenye kemikali.

Wadudu kama vile viwavi na vidukari, ndio hushuhudiwa sana kwa mboga.

Mkulima anahimizwa kupata ushauri kutoka kwa wadau wa kilimo ili kujua dawa bora kutumia kuwakabili na isiyo na kemikali.

Hata hivyo, palizi dhidi ya makwekwe na unyunyiziaji maji ya kutosha hufukuza wadudu.

Magonjwa kama vile Powdery mildew, Leaf blight na Bacterial wilt, ndio huhangaisha mnavu na mkulima pia anashauriwa kupata maelekezo ya kuyadhibiti kutoka kwa wataalamu.

Managu huanza kuvunwa mwezi mmoja baada ya upanzi, na kuna yanayovunwa kwa karibu miezi mitatu mfululizo ikiwa yatatunzwa vyema kwa maji.