• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
AKILIMALI: ‘Kilimo cha spinachi na brokoli kinaniletea hela si mchezo’

AKILIMALI: ‘Kilimo cha spinachi na brokoli kinaniletea hela si mchezo’

Na SAMMY WAWERU

IKIWA kuna uamuzi asiojutia kamwe, uite “kuingilia shughuli za kilimo” kwa kile anasisitiza hakijamuangusha, hususan wakati huu ambapo janga la corona linatesa.

Monica Mwangi, ni mkulima wa mseto wa mimea Ragati, eneobunge la Kieni Mashariki, Kaunti ya Nyeri na kilomita tano kutoka mjini Nanyuki, Laikipia.

Shamba lake na lenye ukubwa wa ekari tatu, ametenga ekari mbili kuzalisha mboga maalum aina ya brokoli (broccoli), spinachi, viazisukari (beetroots) na kiukamba.

Machi 2020, Kenya iliporipoti kuwa mwenyeji wa Covid – 19, ugonjwa ambao sasa ni kero la kimataifa na unaoendelea kuathiri uchumi na sekta mbalimbali, wengi walipoteza nafasi za ajira na baadhi ya biashara kufungwa.

Hata ingawa Monica ni mtaalamu wa masuala ya kibinadamu, alikuwa katika sekta ya uuzaji wa ploti na mashamba.

“Mkurupuko wa corona nchini na mikakati iliyowekwa kuzuia msambao zaidi, viliathiri kwa kiasi kikuu kazi yangu, ikizingatiwa kuwa uuzaji wa mashamba unajumuisha kusafiri kukutana na wateja na pia kuwapeleka ardhi ilipo,” anasimulia.

Licha ya kuwa alikuwa mkulima ingawa kama shughuli ya ziada, janga la corona limemgeuza mwanazaraa kamilifu. Siku kadhaa kabla Kenya kuwa mateka wa virusi vya corona, Monica anasema alikuwa amefanya upanzi wa spinachi na brokoli.

Anadokeza kwamba awali, miaka minne iliyopita, alikuwa amejaribu kulima vitunguu saumu ila vikamfisha moyo kwa kile anataja kama “kulima kwa njia ya simu”.

Brokoli, alizalisha kupitia oda za mikahawa na hoteli Nanyuki katika Kaunti ya Laikipia na Meru.

“Kabla ya kuanza kuzikuza, kutokana na funzo nililopata katika vitunguu saumu nilifanya utafiti wa kutosha, unaojumuisha wateja na jinsi ya kuzalisha kitaalamu,” anafafanua.

Ni hatua iliyoshirikisha mtaalamu wa kilimo kumpevusha kuotesha miche, na Monica anafichua kwamba alitumia jumla mtaji wa Sh25, 000 kukuza brokoli katika robo ekari. Aidha, ni mboga nadra kupatikana na inayouzwa mithili ya dhahabu.

Ikizingatiwa kuwa wateja alioafikiana kuzalisha brokoli ni mikahawa na hoteli, amri ya sekta hiyo kufungwa kwa muda ili kuzuia msambao wa Covid – 19 ikawa sawa na moyo kudungwa kwa sindano.

“Ni mboga ya muda mfupi kukomaa baada ya upanzi na isiyohifadhika muda mrefu baada ya kuvuna. Brokoli ikikomaa inapaswa kuvunwa mara moja, ikikawia, kwa sababu ya ‘maisha yake mafupi’ hukataliwa sokoni. Wateja wangu nao ndio hao biashara zao zilifungwa. Nilianza kufanya hesabu ya hasara inayobisha hodi,” anaeleza.

Aidha, inachukua miezi miwili na nusu kukomaa, baada ya upanzi.

Kupitia mashauriano na mkulima mwenza, anayemtambua kama Kathurima Mwongera, Monica anasema alimshauri kutumia mitandao ya kijamii kufanya matangazo. “Oda ninazopokea ni tele,” anasema.

Kikwazo

Kikwazo kilichopo ni kufikia wateja wa Nairobi hususan wa Soko la Marikiti anaosema ni chungu nzima, kutokana na vizuizi vya barabara kufuatia amri ya kuingia na kutoka Nairobi na viunga vyake.

Wakati wa mahojiano, alisema anahudumia wateja wa kijumla Nyeri, Nanyuki katika Kaunti ya Laikipia na Meru, na vilevile wanaofanya uuzaji wa matunda na mboga. Pia, wapo wenye hoteli na mikahawa iliyoafikia matakwa ya ufunguzi.

“Nina takriban brokoli 2,400 katika robo ekari. Kijumla, mboga moja ni Sh80. Mbali na wanunuzi wa jumla, ninauzia wateja rejareja,” Monica akasema. Maduka ya kijumla, brokoli moja inauzwa kati ya Sh180 na Sh220.

Amekuza spinachi kwenye ekari moja, vitunguu robo tatu, kiukamba na viazisukari chini ya robo.

Kati ya mimea hiyo, ikiwa kuna yanayomtia tabasamu anapofanya mauzo yaite brokoli na spinachi.

“Tangu nianze kilimo cha brokoli na spinachi, sijakosa hela kwenye M-Pesa,” Monica na ambaye ni mama wa watoto watatu anaiambia Akilimali.

Anaeleza, kila baada ya siku kumi huvuna kati ya kilo 400 – 600 za spinachi, kilo moja kijumla ikinunuliwa Sh10.

“Mseto wa mimea ninayokuza, umenigharimu mtaji wa Sh190,000 na ninalenga mapato ya Sh500,000,” Monica anasema.

Wengi wanaamini brokoli ina ugumu kuzalisha na inayotumia mbolea na dawa zenye kemi kali. Hata hivyo, mkulima huyu anasema amekumbatia kilimohai.

“Hutumia mbolea asilia, hasa ya mbuzi. Kudhibiti kwekwe, hufanya palizi mara kwa mara,” anasema.

Kulingana na Caroline Murage, mtaalamu kutoka Royal Seeds, changamoto za mboga hii ni haba, wadudu wanaoshuhudiwa wakiwa wale wanaotoboa mashimo kwenye vichwa vya brokoli na majani.

“Ugonjwa unaotatiza brokoli unatokana na baridi, blight. Ekari moja inasitiri zaidi ya miche 12,500 na inazalisha kati ya tani 6 – 9,” Caroline anafafanua, akitilia mkazo haja ya kuzingatia mfumo wa kilimohai katika uzalishaji wa mboga hii.

Ni mboga iliyosheheni madini, hasa Vitamini, na katika kipindi hiki cha corona watu wanahimizwa kula chakula kinachoimarisha kinga mwilini.

Monica Mwangi, amekumbatia mfumo wa kutumia mifereji kunyunyizia mimea na mashamba maji. Kiini chake cha maji ni Mto Ragati.

Anasema changamoto kuu, ni barabara mbovu hasa msimu wa mvua na ambazo hazipitiki, zinachelewesha mazao kufika sokoni. Sawa na wakulima wengine, anasihi mbunge wa eneo hilo Kanini Kega na viongozi husika, waimarishe hali ya barabara.

Monica alipoulizwa ikiwa ataacha kilimo baada ya corona, alisema: “Nitarejelea uuzaji wa mashamba na ploti, ila ukulima sitaugura. Nimegundua katika kilimo sikosi hela, na ndicho kinakidhi mahitaji ya familia yangu.”

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Maria Mvati

HAENDI: Arsenal yakaribia kukamilisha mazungumzo na Bukayo...

adminleo