KITUNGUU ni zao ambalo huhitaji uangalifu mkubwa kutoka wakati wa kusia mbegu kitaluni hadi kuvuna hivyo mkulima anahitajika kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuanza shughuli nzima.
Jambo ambalo mkulima anatakiwa kufahamu ni kuwa kitunguu huchelewa kukomaa ikilinganishwa na mimea mingine ya aina ya mboga hivyo anashauriwa kuwa mvumilivu sana.
Kulingana na mtaalam wa kilimo ambaye pia ni mwanzilishi wa Kampuni ya African Soil and Crop Care Limited Julius Nduati, kupeleka udongo wa shamba lako katika maabara ili kupimwa ugonjwa na kisha kutibiwa ndio mwanzo katika kilimo cha kitunguu.
“Ninawashauri wakulima na sio tu wale wanaopanga kujishughulisha na upanzi wa vitunguu lakini mkulima yeyote yule awe wa mboga, matunda, mahindi na mazao mengine lazima ajue upungufu wa madini yaliyo kwenye udongo kabla ya kununua mbolea yeyote ile. Hii itamwezesha kujua na kufahamu kiwango cha madini yanayohitajika,” anasema Bw Nduati.
Anaeleza kwamba kilimo ni maji, hivyo kama katika shamba lako kuna upungufu wa maji itakuwa tatizo. Kuchagua na kununua mbegu ni muhimu sana, ndio chanzo cha mazao bora.
Kulingana naye ikiwa eneo lako halina maji ya kutosha itakuwa vigumu kupanda na kukuza zao la kitunguu kwa sababu kinahitaji kunyunyiziwa maji kwa wingi.
Pili kupanda mbegu zilizo na afya ndio chanzo cha kupata mazao mengi na bora. Kuna aina tofauti za mbegu za vitunguu ambazo huuzwa kulingana na eneo kama vile Red Creole, Red Pinnoy, Jambar 1and, Red Bombay.
Aina ya Jambar F1 hupendelewa sana na wakulima wa humu nchini Kenya kwa sababu ya ukubwa wa umbo lake na mazao mengi.
Kitunguu hufanya vyema katika maeneo yaliyo na mvua ya wastani na baridi kiasi wakati wa jua kali.
Matayarisho
Jambo la kwanza ni kuandaa kitalu kilicho na upana wa mita moja, urefu hutegemea na idadi ya mbegu ambazo mkulima anapanga kupanda.
Kitalu kinafaa kuinuliwa 10cm hadi 15cm na kama utakuza mbegu katika vitalu zaidi ya kimoja zitenganishwe 70cm kutoka kitalu kimoja hadi kingine.
Katika ekari moja ya shamba utahitaji kilo 1 hadi kilo moja na nusu ya mbegu.
Kulingana na mtaalamu huyu, ni vyema kuchanganya mchanga na mbegu zako za vitunguu kabla ya kusia.
“Changanya kilo mbili za mchanga kwa kilo moja ya mbegu (1kg mbegu: 2kg mchanga) ili kurahisisha usiaji wa mbegu,” anaeleza.
Kisha sia mbegu katika kina cha 1cm hadi 2cm na upana wa 10cm. Funika mbegu kwa udongo mwepesi huku ukifunika juu kwa matandazo. Nyunyizia kitalu maji mara mbili kwa siku asubuhi na jioni.
Mbegu zitaanza kuota kati ya siku 21 hadi 45 ambapo zitahamishwa katika shamba lililotayarishwa vizuri na kuwekwa mbolea majuma mawili kabla ya kuhamisha miche ya vitunguu.
Julius anasema kwamba siku 7 kabla ya kuhamisha miche punguza umwagiliaji maji pamoja na kuondoa kivuli ili kuifanya miche kuwa na uzoefu wa jua.
Hakikisha umemwagilia maji kitalu kabla ya kuhamisha miche shambani na kila mche ung’olewe na ndonge la udongo ili kuhakikisha mmea huo hautarudi nyuma punde tu utakapopandikizwa.
Hata hivyo Julius anashauri wakulima kutoweka mbolea ambayo haijaoza vizuri kwa sababu itafanya shingo na majani ya vitunguu kuwa makubwa zaidi na kupunguza vichwa vyake ambavyo vinahitajika.
Hamisha miche ambayo ina nguvu zaidi na kuacha mingine ikiendelea kukomaa. Baada ya kuhamisha endelea kunyunyizia maji na kuhakikisha magugu yote yametolewa kwa mkono kwa sababu vifaa vingine vinaweza kutia vichwa vidonda au majeraha.
Fanya hivyo hadi majani yaonyeshe dalili ya vichwa kukomaa siku 90 hadi 150.
Ya kuzingatia
Mbegu hulingana na muuzaji ikiwa ni kati ya Sh20,000 hadi 30,000 kulingana na aina ya mbegu.
Matayarisho ya shamba Sh20,000 kulingana na umbo la shamba lako.
Dawa za viwandani 10,000
Mbolea ya mifugo ambayo imeoza tani 2 ikiwa itagharimu Sh10.
Dawa ya kukinga wadudu na magonjwa Sh15, 000.
Kazi ya vibarua vya kila siku ikiwa ni kupanda, unyunyiziaji maji na madawa, kupalilia, kuvuna 10,000, kunyunyizia maji kwa njia ya matone, 160,000, matumizi ya ziada 20,000.
Jumla ni Sh330,000
Ikiwa mkulima atazingatia yaliyoelekezwa anafaa kuvuna kati ya tani 18 hadi 24 au tani 20 za wastani. Ikiwa mkulima atauza Sh50 kwa kilo moja hivyo basi atatia mfukoni Sh1 milioni katika ekari moja kutoa Sh330,000 za matumizi mkulima atapata faida ya Sh670,000.
Julius anawashauri wakulima kutafuta ushauri kabla ya kuendeleza aina yeyote ya kilimo ili kupata matokeo bora na yenye faida.