Makala

AKILIMALI: Kuna njia bora zaidi ya kuzalisha mbegu bora za viazi mbatata

June 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

VIAZI mbatata hutumika katika mapishi ya chipsi, kripsi na kama kitoweo, pamoja na kuandaa mukimo (mchanganyiko wa viazimbatata na kande).

Nchini Kenya, Nyandarua, Nakuru, Elgeyo Marakwet na Nyeri, ndizo kaunti tajika katika uzalishaji wa viazi hivi.

Kaunti zingine ni; Meru, Kiambu, Taita Taveta, Narok, Bomet, Trans Nzoia, Bungoma, Uasin Gishu na West Pokot.

Pia Kisii, Nyamira, Kirinyaga, Murang’a, Baringo, Nandi, Laikipia na Kericho, ni wakuzaji wa zao hili.

Bw Timothy Mburu (kushoto) na mtaalamu wa kilimo, Meshack Mburu, waonyesha berries za viazi mbatata ambazo hutumika kuzalisha mbegu bora. Picha/ Sammy Waweru

Viazi mbatata vinastawi katika udongo tifutifu (loam) na kichanga (sand), usiotuamisha maji. Wataalamu wa kilimo wanahoji udongo unapaswa kuwa wenye rutuba ya kutosha.

Aidha, unapaswa kuwa na asidi-pH kati ya 5.0-6.5, kulingana na wadau.

Maeneo yanayozalisha viazimbatata yawe yenye uwezo wa kupokea mvua milimita 850-1400, kwa mwaka au vikuzwe kwa mfumo wa kunyunyizia mashamba maji kwa mifereji. Vinastawi maeneo yenye kiwango cha joto cha nyuzi 16-30.

Viazi hupandwa moja kwa moja shambani kutoka kwa vilivyovunwa.

Mbegu zake (tubers) ni vilivyochaguliwa, hasa vile vidogo.

Katika eneobunge la Kieni, Nyeri, mkulima mmoja ameibuka na mbinu maalum kuzalisha mbegu bora.

Bw Timothy Mburu anayekuza viazi hivi kwa wingi eneo la Naromoru, anasema ‘matunda’ ya zao hili maarufu kama ‘berries’ yanaweza kutumika kuzalisha mbegu.

Mimea ya viazimbatata huchana maua yanayozalisha matunda, ambayo yana mbegu ndogo zinazotumika kufanikisha shughuli hii. “Tunda huwa na kati ya mbegu 60 hadi 80, kwa mujibu wa utafiti niliofanya na tajiriba niliyonayo katika ukuzaji wa viazi,” anadokeza Bw Mburu.

Mkulima huyu anaendelea kueleza kwamba matunda yaliyokomaa, kabla mimea ya viazi kukauka-dalili uvunaji unabisha hodi, huchumwa kisha mbegu zinatolewa (kuyakama).

Zinaoshwa vyema kwa maji, kisha zinakaushwa juani.

“Zikaushwe kati ya wiki 2-3,” anashauri mkulima Mburu.

Meshack Wachira, mtaalamu wa kilimo anasema matunda yanayopaswa kuchumwa yawe makubwa, yenye afya bora na huru dhidi ya magonjwa na wadudu.

Vilevile anahimiza yasiwe na udhaifu wala alama yoyote ya kuathirika.

“Mmea unaoyazalisha (mother plant) uwe wenye afya na usiwe na athari zozote zile ambazo zinaufanya udhoofike,” anasisitiza Bw Wachira.

Kulingana na Timothy Mburu, mbegu zinapokauka, hupandwa kitaluni, na kati ya mwezi mmoja na nusu hadi miwili, miche yake huhamishiwa shambani.

“Inapandwa kama miche mingine ya mboga, na baada ya miezi mitatu mkulima atapata mbegu bora na ya hadhi ya juu,” anaeleza.

Bw Mburu anafafanua kwamba utunzaji wake ni sawa na vinavyokuzwa viazimbatata shambani.

Wakati wa mahojiano, Taifa Leo iligundua kwamba mmea mmoja una uwezo wa kuzalisha hadi viazi 13.

Kwa hili, Mburu anasema mengi ya mazao huwa na umbo la aina yake na hata yenye rangi ya kijani.

Kuna aina mbalimbali ya viazi kama vile Tigoni, Shangi, Kenya karibu, Kenya Mpya, Sherekea, Ambition na Laura, miongoni mwa vingine vingi.

Mburu anasema hupanda aina ya Shangi.