Makala

AKILIMALI: Kunasa na kuandaa kumbikumbi humpa kipato

March 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na STEPHEN DIK

KUMBIKUMBI ni mchwa wenye mbawa wanaoishi ardhini au kwenye kichuguu, hupatikana wakati mvua inanyesha baada ya kiangazi.

Ni wadudu ambao huliwa wakishakaangwa au hata wakiwa hai wanaweza kutafunwa kama njugu, ni chakula adimu na muhimu zaidi kwa mwili wa mwanadamu.

Mama Rispa Awuor ni muuzaji kumbikumbi na bidii yake inaambatana na methali isemayo kawaida ni kama sheria, hii ni kwasababu amekuwa akivuna kumbikumbi kila msimu, usiku na mchana kwa zaidi ya miaka ishirini sasa.

Anafanya kazi ya kuuza kumbikumbi mjini Bumala kaunti ya Busia, ni mchuuzi anayefahamu zaidi kuhusu msimu wa kumbikumbi, anajua aina tofauti za kumbikumbi na pia ni mwenye ujuzi mwingi wa kuvuna kumbikumbi misimu yote.

Mama Awuor anasema kitoweo cha kumbikumbi ni bora, kimeshinda kitoweo cha nyama, mboga au mkate sababu kina madini ya hali ya juu zaidi yanayohitajika kwa mwili wa mwanadamu.

Anashangaa licha ya umuhimu wake, kitoweo cha kumbikumbi hakijatiliwa maanani kiasi kwamba hakuna bidhaa za kumbikumbi madukani.

“Katika kutayarisha kumbikumbi wa kuuza, tayari kwa kula, kwanza huoshwa na kutolewa mabawa, kisha wanakaushwa kwa jua na kukaangwa na kuwekwa chumvi pekee, hakuna kuweka tomato wala kitunguu kwa kumbikumbi,” Mama Awuor anasema na kuongeza kuwa kumbikumbi waliohifadhiwa kwa muda mrefu hawaliwi mara moja, huoshwa kwa maji moto kabla ya kukaangwa bila mafuta.

Mama huyu wa watoto wanne anasifu biashara ya kumbikumbi akisema humwezesha kupata karo ya shule kwa wanawe haraka.

Anafurahi akisema wakati kuna kumbikumbi, watoto husoma bila matatizo ya karo, maisha huwa mazuri kwa sababu hakuna shida, kumbikumbi huleta pesa nyingi.

Anasisitiza kwamba kumbikumbi hununuliwa haraka na kuleta pesa nyingi sababu wateja wengi hutoka mbali, wanasimamisha magari yao, au kutoka kwa magari ya uchukuzi na kununua kumbikumbi hata za Sh500 kwa wakati mmoja.

Gunia la kilo 100 lililojaa kumbikumbi huuzwa kati ya Sh20,000 na 25,000 kwa bei ya jumla, bei ya rejareja yaweza kuuzwa kwa kati ya Sh40,000 na 60,000 punde tu baada ya kuvunwa.

“Kuvuna kumbikumbi pia kunahitaji ujuzi kwa sababu kumbikumbi hujitokeza kwa msimu, kuna kumbikumbi za mwezi wa Februari na mwezi Machi, kumbikumbi za mwezi wa Aprili, kumbikumbi za mwezi wa Agosti na mwezi wa Septemba kisha mwisho kuna kumbikumbi wa mwezi wa Oktoba hadi Desemba,” anafichua.

Bidii na ujuzi

Anasema biashara ya kumbikumbi haihitaji mtaji kuazisha, ni bidii na ujuzi pekee na kwamba ni kazi inayoleta pesa nyingi, haraka zaidi.

Anaongeza kusema kumbikumbi hawana mmiliki, unapogundua shimo au tundu kwenye kichuguu, basi hilo ndilo shamba lako la kuvuna kumbikumbi kila msimu wa mvua.

Kando na kuvuna kumbikumbi mwenyewe, wakazi wa mji wa Bumala huvuna kumbikumbi kwa wingi vijijini na kumuuzia Mama Awuor kwa bei ya Sh50 kikombe ambapo yeye huuza kikombe hicho kwa Sh100 akiongezea thamani.