Makala

AKILIMALI: Kwake pato la maboga haya lazidi faida ya mboga na matunda

March 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER CHANGTOEK

BAADA ya kuhitimu masomo yake ya shahada katika chuo kikuu, Josephat Kiptoo alijitosa katika ukuzaji wa mimea ya pilipili mboga na kabichi.

Hata hivyo, alishurutika kuachana na ukuzaji wa mimea hiyo alipokosa kupata mapato mazuri kutokana na mimea hiyo.

Alilazimika kujitosa katika uzalishaji wa mazao yanayolandana sana na maboga, ambayo hujulikana kama butternuts, baada ya kusimuliwa na rafiki yake kuhusu mmea huo.

Kiptoo alijitosa katika shughuli hiyo kwa kuutumia mtaji wa Sh15,000, katika eneo la Litein, Bureti, Kaunti ya Kericho.

“Mimi hukuza mimea ya butternuts katika shamba la ekari mbili,” asema mkulima huyo, ambaye huukuza mmea huo kwa kutumia mbolea asilia.

“Nilijuzwa kuhusu mimea ya butternuts na jirani mmoja ambaye alinielezea kuwa kuna butternuts ambazo ni hybrid. Nilianza kushughulika na kilimo hiki mnamo mwaka 2015,” afichua mkulima huyo, ambaye alihitimu shahada ya Sayansi ya Tarakilishi, katika Chuo Kikuu cha Kabarak, mnamo 2015.

Kiptoo anadokeza kuwa alizinunua mbegu alizozikuza kutoka kwa kampuni ya kutengeneza mbegu ya Simlaw, kwa bei ya Sh10,000.

Anasema kwamba kwa kuwa watu wengi hawakuwa wakifahamu kuhusu mazao ya butternuts katika eneo hilo, alilazimika kubandika vijikaratasi vyenye maelezo ya jinsi ya kupika.

“Baadhi ya watu walikuwa wakipika jinsi maboga (pumpkins) yanavyopikwa. Nikaamua kubandika maelezo kuhusu jinsi ya kupika, na watu wakaanza kujua kupika,” aongeza mkulima huyo.

Kabla ya kuzipanda mbegu, mkulima huyo huyo, kwanza, hulitayarisha shamba ipasavyo. Ni sharti mchanga uwe mwororo maadamu mizizi ya mmea huo huhitaji mchanga laini.

“Mbegu zinafaa kupandwa kwa kuacha nafasi ya mita moja kwa mita moja, kutoka kwa mbegu moja hadi kwa nyingine,” asema.

Kiptoo anasema kwamba kwa kuwa yeye hutumia mbolea asilia kuikuza mimea yake ya butternuts, magugu huota shambani kwa kasi mno, na hivyo basi huhitajika kupaliliwa kila mara ili kuyaangamiza maotea hayo.

“Kuzuia kuota kwa magugu ndiyo imekuwa changamoto kubwa sana,” asema mkulima huyo.

Kwa mujibu wa Kiptoo, mmea uo huo huchukua muda wa miezi mitatu hadi minne ili kukomaa na kuzaa mazao.

Mkulima huyo, ambaye huyauza mazao yake kwa watu wa kawaida katika kaunti hiyo na kwa supamaketi kadha wa kadha nchini, anasema kuwa huyauza mazao hayo kwa bei ya Sh100 kwa kilo moja.

Yeye huyauza mazao yake katika duka-kuu la Smart Shelves jijini Nairobi, na katika maduka-kuu ya Souk Bazaar na Giftmart yaliyoko mjini Litein.

Kiptoo anadokeza kuwa mchanga katika eneo hilo ni bora kwa shughuli za kilimo.

Aidha, mvua ya mara kwa mara ambayo hunyesha katika eneo hilo huwawezesha wakulima kujishughulisha na kilimo kama hicho, japo ni wakulima wachache ambao hujihusisha na ukuzaji wa butternuts.

Mkulima huyo anawashauri wale wanaonuia kujishughulisha na ukuzaji wa mmea huo kupata maelezo kuhusu mchanga ili kujua iwapo mmea huo unaweza kukua vyema katika maeneo yao.

Aidha, anawashauri kutafuta soko la mazao hayo kwanza, kabla hawajaanza kujitosa katika kilimo hicho.

Pia, anawashauri wayazalishe mazao kwa mbinu asilia.

Hali kadhalika, ni muhimu kuyazalisha mazao bora ambayo ni ya kufaa kuliwa.

Anasema kuwa ni muhali mno kwa mimea ya butternuts kuathiriwa na magonjwa au kuvamiwa na wadudu waharibifu.

Kiptoo, ambaye anaazimia kujitosa katika uongezaji wa thamani kwa mazao hayo katika siku za usoni, anafichua kuwa uzalishaji wa mazao hayo una faida, mradi tu mkulima awe na soko la kuyauzia mazao hayo.

Anaongeza kwamba ni nadra sana kwa mazao ya butternuts kuathiriwa na mfumukobei.

Mimea ya butternuts hukua vyema katika naeneo yenye nyuzijoto 18 hadi nyuzijoto 24.

Pia hukua kwa mchanga wenye tindikali kiwango cha 6.0-6.5 katika kipimo cha pH.