Makala

AKILIMALI: Manufaa ya mianzi kwa maisha ya binadamu

December 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA RICHARD MAOSI

[email protected]

Ukataji miti kiholela kwa muda sasa umechangia kwa asilimia kubwa ukosefu wa mvua, jambo linaloelekea kuhatarisha ustawishaji wa mimea yenye manufaa kwa binadamu.

Hii ndio sababu serilkali ilipiga marufuku ukataji miti katika misitu ya umma,na ile ya kibinafsi kuanzia Septemba mwaka uliopita ili kurejesha uhai wa misitu,na mwelekeo kabambe wa kuyalinda mazingira.

Hali ni kama hiyo kwa kijana Raphael Otieno Odipo, mzaliwa wa Ahero kaunti ya Kisumu anayetumia mianzi (bamboo sticks), badala ya mbao za kawaida kujipatia riziki ya kila siku.

Odipo anasema alianza kufanya kazi yenyewe mnamo 2006, akiwa mhudumu wa mkahawa mmoja mjini Nakuru, lakini akapata mwanya wa kujiajiri na baadae ili kuwa mtu wa kujitegemea.

Anasema ubora wa samani unategemea mambo mengi mojawapo ikiwa ni gharama nafuu, kwa mtu wa kipato cha chini asiyemudu kununua bidhaa za bei ghali.

Alifichulia Akilimali kuwa alikuwa akipokea mshahara mdogo kwa mwezi, kiasi kwamba hangeweza kukidhi mahitaji ya familia yake changa ndiposa akajaribu kutafuta njia mbadala ya kujiongezea kipato.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja aliweka akiba ya 5000, iliyomsaidia kupata mtaji wa kwanza kuwekeza katika utengenezaji wa fanicha za kisasa akitumia miti ya mianzi na kupiga teke miti mbao.

Ingawa mara ya kwanza haikuwa rahisi, alitumia mtandao wa kijamii kutafuta sehemu ambazo miti ya bamboo nchini hukuzwa kwa wingi, yaani Magharibi ya Kenya na Nyanza.

Alianza kuagiza mianzi kutoka kaunti ya Kakamega, akisema kuwa ni mimea inayofanya vizuri katika maeneo yenye chemichemi hususan kando ya mito na bahari bila kupandwa na binadamu.

Faida za Bamboo ni maridhawa kwa sababu huuzwa kwa bei nafuu na soko lake ni la uhakika.fanicha zinazoundwa kutokana na mianzi humpa mfanyibiashara hela nzuri, kwa sababu baadhi ya samani anazotengeneza ni baina ya 2500-14,000.

“Ingawa ni mti unaochukua muda mfupi kukomaa mashina yake ni dhabiti, na yanaweza kutoa bidhaa nzuri muradi mtumiaji ana ujuzi wa kuunganisha sehemu sehemu za bidhaa,” akasema.

Kulingana naye meza, viti na makabati huunganishwa kupitia katani au kamba ya mkonge, akisema misumari haifai kutumiwa kwa sababu hutengeneza nyufa ambazo haziwezi kurekebika.

Odipo anasema kazi yenyewe inahitaji subira, kwani fundi anahitaji kuchukua muda wake ili kuhakikisha kuwa Bamboo sticks zimekauka vizuri, na kuwa kavu ili ziweze kushikika vyema.

Mashina yake huwa laini ndiposa wakati mwingine watumiaji wanashauriwa kukausha miti ya Bamboo katika tanuri lenye moto wa kadri, kabla ya kuhifadhi ndani ya stoo zikisubiriwa kutumika.

Alisema kuwa miti ya mianzi ni dhabiti kuliko mbao za kawaida maana, haziwezi kuharibiwa na wadudu wa kawaida kama vile sisimizi na mchwa, waliozowea kutafuna mashina, jambo linaloweza kumsababishia mfanyibiashara hasara.

Pili alieleza kuwa miti ya mianzi haistahili kupakwa rangi labda mara moja moja ikilazimu kwa sababu ulaini wake unatosha kuleta mvuto wa kipekee.

Anasema kwa sababu ya ubora unaotokana na fanicha za mianzi amekuwa akiwavutia wanunuzi wengi kutoka Nakuru, Kisumu, Mombasa, Nairobi na hivisasa analenga kushika soko la kimataifa kupitia mtandao wa kijamii.

Ingawa soko la fanicha inayotokana na mianzi haijapata mashiko makubwa, anatumia mtandao wa kijamii kuwafikia wanunuzi wengi iwezekanavyo, akiamini kuwa siku moja wanunuzi watachangamkia bidhaa hii adimu.

Kando na hayo amekuwa akiwapatia vijana kutokaa mitaa ya mabanda ya Pondamali,Kenlands na Bondeni ujuzi wa bure akilenga kuwasaidia katika juhudi za kupigana na janga la ukosefu wa ajira.

Lengo lake kuu likiwa ni kuwabainishia kuwa wanaweza kutengeneza fanicha zao na kwa wakati huo wakiendelea kuyalinda mazingira .

“Hii ni katika kampeni ya kuhakikisha kuwa Kenya inafikia lengo lake la kufanikisha kuwa na asilimia ya misitu inaongezeka kutoka 3-16 ifikapo mwaka wa 2030,” aliongezea.

Anawashauri vijana kuacha kasumba ya kuchagua kazi kwa sababu,wanaweza kujiajiri katika ulingo wowote bila ya kutegemea serikali.

Miongni mwa bidha anazotengeneza ni saa za miundo ya kisasa zilizozungushiwa miti ya mianzi na kuongezewa mapambo ili kumvutia mnunuzi.

“Hakika bidhaa za haiba kubwa huwa ni bei ghali,kinyume na zile ambazo ni duni ambazo huuzwa kwa bei rejereja mitaani lakini haziwezi kudumu kwa muda mrefu,” akasema.