Makala

AKILIMALI: Manyoya ya kondoo ajira nzuri kwa kundi kongwe la vijana

August 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na STANLEY KIMUGE na CHARLES WASONGA

HUKU akitumia miguu yake miwili, anamkamata kondoo kwa mkono wake mmoja huku mnyama huyo akitulia ndani ya kibanda kilichojengwa kwa mbao.

Na katika mkono mwingine, amekamata makasi maalum ambayo yeye hutumia kukata manyoya ya mnyama huyo.

Huyu si mwingine ila ni Joseph Kiptarus mwanachama wa kundi la wakulima wanaoibuka la Chemosong Young Farmers kilichoasisiwa mnamo 1988. Amedumu katika kazi ya kunyoa kondoo kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita.

“Ninaweza kunyoa kati ya kondoo 45 na 60 kwa siku. Mimi hutumia muda wa takriban dakika tano kunyoa kandoo mmoja, ambayo huzalisha kati ya kilo mbili na tano ya manyoya, uzalishaji unaotegemea namna ambavyo kondoo husika anavyolishwa,” anaeleza huku akiendelea na kunyoa mnyama huyo.

Shughuli hiyo iinapoendelea, mwanachama mwingine wa Chemosong Young Farmers, huwa ange na mafuta maalum ambayo hupaka kondoo ambao, kwa bahati mbaya, hujeruhiwa na makasi hayo maalumu akinyolewa.

Kibanda hicho cha mbao ambako shughuli hiyo huendesha kiko katika kijiji cha Kerer katika kata ya Lelan, eneo-bunge la Marakwet Magharibi, kwenye mpaka wa kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi.

Kondoo aina ya Merino katika eneo la Kerer, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet. Picha/ Jared Nyataya

Kimegawanywa katika sehemu kadhaa. Kuna sehemu ya kuweka kondoo, sehemu ya kunyoa, ghala la kuhifadhi manyoya ya kandoo na afisi za kundi hilo.

Na kuna sehemu ambako kondoo hupitia kwenda nje baada ya kunyolewa.

Mbali na ufugaji kondoo, eneo hilo lenye milima na mabonde na liliko mita 3,000 juu ya kimo cha bahari huku kiwango cha joto kikiwa sentigredi 5, viazi pia hukuzwa kwa wingi na huuzwa katika miji mbalimbali nchini.

Kikundi cha Chemosong Young Farmars kina takriban wanachama 160 ambao hufuga kondoo 50, kwa wastani, kila mmoja. Wao hupeleka kondoo wao katika kibanda hicho kwa ajili ya kunyolewa.

“Huwa tunawanyoa kondoo wetu baada ya kipindi cha mwaka mmoja wanapofikisha uzani wa kilo 30 na zaidi. Na sharti tuhakikishe kuwa wamelishwa vizuri ili waweze kuzalisha kati ya kilo tatu na tano ya manyoya kwa awamu,” anasema John Chelanga, katibu wa kikundi hicho.

Lakini kwa muda mrefu wanachama wamekuwa wakiathiriwa na bei duni ya bidhaa hiyo sokoni. Hali ilikuwa mbaya zaidi hasa kufuatia kuwekwa huru kwa sekta ya utengenezaji nguo.

Hii ndiyo maana kati ya viwanda 52 vya kutengeneza nguo vilivyokuwa vikihudumu wakati huo, vingi vilifungwa kutokana na ushindani wa nguo zilizoingizwa nchini kutoka nje.

Hali hii, anasema Bw Chelang’a, iliwavunja moyo wafugaji kondoo wa manyoya katika eneo zima la Elgeyo Marakwet.

“Isitoshe, baadhi yetu tuliathirika kwa kupunjwa na wafanyabiashara mawakala ambao walinunua manyoya yetu kwa bei duni mno,” anaongeza.

Hata hivyo, hawakuvunjika moyo. Mnamo mwaka wa 2009 walitia saini makubaliano na kampuni ya Stanage Services Limited iliyoko Nakuru. Kampuni hiyo hununua, kusafisha na kuuza manyoya ya kondoo katika masoko ya ng’ambo.

“Mkataba huu ulifufua matumaini yetu. Tulianza kupata faida kwani kampuni hii ilianza kununua manyoya yetu kwa bei nzuri,” Bw Chelanga anaeleza.

Anasema manyoya kutoka kwa aina mbalimbali ya kondoo huwekwa kwenye viwango kutegemea ubora wa manyoya.

“Kwa hivyo, wanachama wa kikundi chetu hufuga kondoo aina ya Corriedale na Merino ambao manyoya yao huwa magumu na rahisi kuosha na kutayarisha kwa ajili ya kuuzwa,” Bw Chelanga anasema.

Kwa mfano, anaeleza, manyoya aina ya C1 ni yale yaliyonyolewa kutoka kwa kondoo aina ya Corriedale.

Na M1 yanatoka kwa kondoo aina ya Merino. Nayo M9 yanazalishwa kutoka kwa kondoo wa kike aina ya Merino.

Na manyoya ya viwango vya chini kabisa ni ya gredi X1 ambayo hunyolewa kutoka sehemu ya kichwa na utumbo wa kondoo. Manyoya kutoka sehemu hizi huwa ni yenye urefu wa inchi nne.

“Bei pia huwa ni tofauti. Sisi huuza gredi ya M1 kwa Sh265 kwa kilo huku C1 ambayo huwa na urefu wa kati ya nchi tatu na tatu na nusu huuzwa kwa Sh260 kwa kilo. Lakini tukibahatika kupata manyoya safi, huuzwa kwa bei nzuri ya Sh700 kwa kilo,” Chelanga anasema.

Manyoya ya kondoo ya gredi C1 aghalabu hutumiwa kutengeneza suti za bei ghali. M1 na X1 nayo hutumiwa kutengeneza nguo za kawaida, leso na mablanket.

“Tunaweza kuzalisha kati ya tani saba na tani 15 za manyoya kwa mwaka mmoja. Lakini changamoto ni kwamba barabara za sehemu hii ziko katika hali mbaya. Vile vile, bado hatuna kiwanda cha kusafisha manyoya ili yaweze kuuzwa kwa bei nzuri,” anasema mwenyekiti wa Chemosong Young Farmer, James Kimaget.

Mkulima huyu anaongeza kuwa mbali na manyoya ya kondoo, wao huchuma pesa za ziada kwa kuuza kondoo kwa bei ya kati ya Sh4,000 na Sh10,000 kutegemea msimu.

Bw Kimaget anaongeza kuwa baadhi ya changamoto zinazoathiri kazi yao ni maradhi ambayo hukumba kondoo na kusababisha baadhi yao kupoteza manyoya.

Mtaalam wa afya ya mifugo, Bi Monica Yator anasema kondoo hupoteza manyoya yao baada ya kuvamiwa na wadudu kama vile kupe na viroboto ambao husababisha mwasho katika miili yao.

“Wadudu wanapovamia kondoo, miili yao huwasha, hali inayowalazimi kujisugua kwenye kuta za nyumba na hivyo kupoteza manyoya. Ni muhimu kwa wakulima kutumia dawa aina ya Acaricide kila mara kwa kuwatumbikiza kwenye majosho yenye dawa hii. Hii ni kwa sababu unyunyiziaji pekee hauwezi kuangamiza wadudu hawa,” anashauri mtaalamu huyo ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Eldoret.

Bi Yator anaongeza kuwa ukosefu wa madini bora kama selenium, zinc, copper (ambayo huyapa manyoya rangi) pia unaweza kusababisha upungufu wa manyoya kwa kondoo.

“Zizi la kondoo sharti lijengwe kwa njia maalum inayotoa nafasi kwa kinyesi kupitishwa kupitia sehemu ya chini. Pia inapaswa kujengwa juu ya ardhi na kuwekwa sehemu za kuingiza na kutoa hewa,” anaongeza.

Wakulima, anaeleza, pia wanapaswa kuhakikisha kuwa usafi umedumishwa katika zizi la kondoo ili kuzuia maambukiza ya magonjwa.

“Na wafugaji wahakikishe kuwa kondoo wao wamepewa dawa za kuangamizi minyoo kila mara ili kuwazuia kula mabaki yenye vimelea waharibifu,” Bw Yator anashauri.