Makala

AKILIMALI: Maua ni pesa na kwa Mzee Konde yamelisha na kumvisha miaka 25

February 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES ONGADI

MARA tu unapovuka daraja la Nyali ukitokea Mombasa kisiwani, mita chache na kanisa la St Emmanuel, unaona maua mazuri ya kupendeza pembeni mwa barabara.

Ni maua aina tofauti yanayovutia na kumeremeta na ambayo wengi hudhania ni mapambo yaliyowekwa kwa minajili ya kung’arisha mazingira katika barabara hiyo inayotumiwa sana na watalii wakielekea hoteli za kifahari kaskazini mwa Pwani.

Hata hivyo, kama wasemavyo wavyele kwamba pesa ni maua lakini kwa Bw Konde Washe mzaliwa wa Kilifi miaka 62 iliyopita, maua kwake ni pesa ambayo kwa miaka na vikaka imekuwa sabuni ya roho yake.

Bw Konde Washe akifurahia maua aina ya Thuya katika bustani yake ndogo iliyoko karibu na daraja la Nyali, Mombasa. Picha/ Charles Ongadi

“Maua haya yamekuwa yakinipatia hela kwa muda wa miaka zaidi ya 25 na ndiyo tegemeo langu kiuchumi,” asema Bw Washe aliyeamua kuwacha kazi aliyofanya tangia ujana wake ya ugemaji wa tembo la mnazi.

Bw Washe anapanda aina tofauti ya maua katika bustani hiyo ambayo imekuwa maarufu kwa wapita njia wanaotumia barabara ya Mombasa/Malindi.

Kuna maua kama Coconut palm, Palm trees, Fuladino flowers, Golden palm, Royal palm, Umbrella palm, Indian trees, Cotton flowers miongoni mwa mengine mengi.

Aidha, Bw Washe anaiambia Akilimali kwamba maua aina ya Indian trees ambayo ni mirefu na yenye majani makubwa huwa kama lulu katika biashara yake.

Wengi hupenda maua aina ya Indian trees kutokana na kwamba yanatumika sana katika kuzungushia mipaka kwenye boma hasa katika mitaa ya mabwanyenye.

Upanzi

Bw Washe anasimulia kwamba miche ya Indian tree hupandwa katika nasari kwa kipindi cha mwezi kabla ya kuhamishwa kwenye pakiti maalum tayari kuuzwa.

Bw Washe afichua kwamba mche mmoja wa Indian tree huuza kwa kati ya Sh300 hadi 400 wakati ukiwa ungali mdogo huuza kwa kati ya Sh30 hadi Sh40.

Kuna maua mengine kama Cotton flower ambayo huenda kwa kati ya Sh200 hadi Sh300 huku Palm tree akiuza kwa Sh600, Coconut palm akiuza kwa Sh500, Golden palm kwa kati ya Sh500 hadi Sh600, Royal palm kwa kati ya Sh400 na Sh500 miongoni mwa mengine.

Tofauti na biashara zingine ni kwamba siyo kila siku wateja hujitokeza kununua maua na kuna msimu mfanyabiashara hulazimika kurudi nyumbani patupu bila kuuza lolote, ila wakati wa msimu mzuri anatia kibindoni kati ya Sh3,000 hadi Sh5,000 kwa siku.

Bw Washe aongeza kwamba maua huhitaji kunyunyiziwa maji kila wakati ili yaweze kunawiri na kuvutia na mara nyingi ukosefu wa maji ya kutosha huyafanya kusinyaa na kunyauka.

“Ni bora kuwa na kisima au mfereji wa maji kwa minajili ya kunyinyizia maua kila asubuhi na jioni hasa wakati wa kiangazi,” asema Bw Washe anayeongeza kusema kwamba biashara ya maua imeweza kubadilisha maisha yake kiuchumi.

Na ili kuhakikisha wateja wake wanapata wanachohitaji kila wakati, Bw Washe hulazimika kusafiri hadi eneo la Kaloleni, Giriama kaunti ya Kilifi kwa minajili ya kusaka aina mbalimbali ya maua asilia yanayopatikana mashambani.

Aidha, Bw Washe anakiri kuwepo kwa changamoto kibao katika upanzi wa maua ikiwemo uvamizi wa wadudu waharibifu ambao husababisha hasara kubwa wasipokabiliwa kwa wakati ufaao.

Ili kuwaangamiza wadudu waharibifu kwa wakati ufaao, Bw Washe aghalabu hutumia dawa maarufu aina ya Dudu Thrin na aina mengine ya dawa za kuwaangamiza wadudu na pia magugu.

Tatizo lingine huwa ni wakati wa kiangazi ambapo biashara hushuka kwa kiwango kikubwa na kusababisha hasara.

Hata hivyo, Bw Washe anakiri waziwazi kwamba biashara ya kuuza maua inalipa na ndiposa aliamua kuwacha kazi ya kugema tembo la mnazi.

Kazi ya kuuza maua imemfanya Bw Washe kuweza kuwakimu kimaisha familia yake mbali na kuwapatia wanawe masomo yanayohitajika.

Anaiomba serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwapatia motisha zaidi kupanda maua kandokando mwa barabara kwa sababu yanaleta mazingara mazuri hasa kwa wanaozuru mji huu wa kitalii.

“Licha ya kwamba ni biashara inayotuletea tija lakini pia tunapamba mji huu na kuwa na mwonekano wa kuvutia kwa hivyo tunastahili kupewa morali na wala siyo kupigwa vita na wenye mamlaka,” asema.

Anaipongeza serikali ya kaunti chini ya gavana Ali Hassan Joho kwa kuwaruhusu kuendeleza biashara zao kandokando mwa barabara nyingi eneo la Mombasa huku akiwashauri vijana kuanza kuchukua mikoba kutoka kwao.