Makala

AKILIMALI: Mbunifu wa fasheni aliyeweka mawazo katika kilimo cha mboga

February 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES ONGADI

NI shamba la ekari tano lililoko Mwakirunge, Kisauni, takribani kilomita 18 kutoka kitovuni mwa jiji la Mombasa ambako Bi Nancy Nimwaka Goye anaendesha kilimo cha pilipili mboga, nyanya, biringani na mabenda.

Licha ya hali ya kiangazi eneo hili, Bi Goye kamwe hajakata tamaa na amezidi kugaagaa katika kilimo hiki ili kufikia malengo yake ya kutosheleza mahitaji ya wateja wake wengi.

Amechimba visima vinne katika kuhakikisha anakabiliana barabara na hali ya kiangazi kwa kunyunyizia kila mara shamba hili lake la ekari saba.

“Sijuti kamwe kuacha taaluma yangu ya ubunifu wa fasheni kufanya kilimo kwa sababu moyo wangu umeridhika na ninachofanya,” asema Bi Goye alipotembelewa na Akilimali shambani mwake eneo la Mwakirunge, Kisauni, Mombasa.

Kulingana na Bi Goye, mshawasha wa kujitosa katika kilimo ulianza kumwandama tangu utotoni kutokana na motisha aliopata kutoka kwa babake mzazi ambaye ni maarufu kwa kilimo cha mpunga (mchele) eneo la Ramsi kaunti ya Kwale.

Baada ya kuwaza na kuwazua kwa kipindi kirefu, mkulima huyu aliamua kuanza kilimo cha pilipilihoho ambacho kulingana naye sio wakulima wengi Pwani hupenda kukifanya.

Bi Goye anafichua kwamba aliamua kujitosa katika kilimo cha pilipili mboga, nyanya, mabenda, biringani na mchicha kutokana na kwamba zinachukua kipindi kifupi kabla ya kuanza kuvuna.

Kwa pilipili mboga, humchukua kati ya miezi miwili hadi mitatu pekee kabla kuanza kuvuna wakati nyanya ikichukua takribani miezi mitatu huku mabenda na biringanya zikichukua mwezi mmoja pekee.

Wiki tatu hadi nne

Kwa pilipili mboga Bi Goye anasema kwamba anaziotesha katika nasari kwa kipindi cha kati ya wiki tatu hadi nne kabla ya kuzihamisha shambani ambako zinachukua takribani wiki tatu hadi nne kukomaa na kuanza kuvunwa.

Aidha, Bi Goye asema kinyume na baadhi ya wakulima wanaopendelea kilimo cha biringanya ya kawaida, yeye anapanda biringani nyeupe ambayo hupendwa na wengi eneo la Pwani kutokana na kwamba haina mwasho na ladha yake ni kama nyama.

Aghalabu mkulima huyu hutumia samadi  na kinyesi cha kuku, mbuzi na kondoo kama mbolea katika kuhakikisha anapata mavuno mazuri tofauti na baadhi ya wakulima wanaotumia kemikali katika kupata mavuno mengi na kwa haraka.

“Najivunia kuwa na mbolea kibao ninazopata kutoka kwa ng’ombe, mbuzi na kuku ninaofuga hapa shambani mwangu,” asimulia Bi Goye.

Kulingana na mkulima huyu, msimu mmoja wa mavuno unaochukua kipindi cha miezi mitatu, ana uwezo wa kutia kibindoni faida ya Sh200,000.

Mara nyingi Bi Goye analenga kuuzia maduka makubwa ya jumla (Supermarkets na Wholesalers) yanayopatikana Mombasa na Kilifi na pia wafanyabiashara wachuuzi.

Anasema kwamba mara nyingi huvuna pilipilihoho mara mbili kwa wiki huku akipata kilo 200 kwa kila vuno. Wakati wa msimu mzuri anauza kilo moja ya pilipili hoho kwa kati ya Sh80 hadi Sh120 na wakati biashara iko chini anashukisha bei hadi kati ya Sh30 hadi Sh25.

Anaongeza kwamba kwa mabenda huuza fungu (iliyo na mabenda kumi) kwa Sh10 huku akiuza mabenda 14 kwa Sh10 wakati kuna mvua.

Aghalabu kwa nyanya huuzia madukamakuu yaani supermarkets na wakati mwingine akipeleka soko kuu la Kongowea au lile la Marikiti lilioko katikati mwa mji wa Mombasa.

Hata hivyo, Bi Goye ambaye ameajiri wafanyakazi watano wanaomsaidia katika mishemishe shambani asema kwamba changamoto kuu anayokabiliana nayo mara nyingi huwa ni wadudu kama White flies ambao ni waharibifu kwa mimea na magonjwa fangasi yanayolemaza ukuaji wa mimea.

Anawashauri wakazi wa Pwani kutotegemea kazi za kuajiriwa na badala yake kutumia vyema ardhi kubwa walizo nazo kufanya kilimo kuzalisha mali.