Makala

AKILIMALI: Mkosi kazini ulivyompa ufumbuzi wa jinsi ya kuvuna pato nono ndani ya uandishi

July 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

[email protected]

MWAKA wa 2018 ulikuwa wa mkosi katika kazi ya uanahabari ya Bw Mwangi Mbuthia, akifahamika kwa jina la majazi la Dkt Mugikunjo.

Alisimamishwa kazi kwa muda wa mwaka mzima na ndipo akiwa nyumbani aliwaza na kuwazua jinsi ambavyo angebakia katika hali ya pato.

“Nilikuwa nimezoea kuamka na kuingia katika studio kila siku ili kuchapa kazi. Ushirika wangu na mashabiki wangu ulikuwa umeniingia katika hisia na bongo kiasi kwamba kujipata nimetimuliwa kwa muda nusura kunipe uwazimu,” akiri.

Anasema kuwa shida nyingine kuu ilikuwa ya kuendeleza maisha yake akiwa nje ya pato na akang’amua kuwa angetaabika sana ikiwa hangejipa riziki mbadala kama hali ya dharura.

“Hapo ndipo wazo la kuandika kitabu lilinijia. Niliamua kuandika kitabu kwa lugha ya mama kwa kuwa kazi yangu studioni ilikuwa ya kutangaza kwa lugha iyo hiyo ya Gikuyu,” asema.

Hapo ndipo alianza safari ya miezi 10 ya kuandika kitabu kinachofahamika kama ‘Ngai wa Hiti na Ng’ano ingi’ yaani (Mungu wa Fisi na Hadithi Nyingine).

Alizindua utafiti wake wa misamiati mwafaka ya kupamba kitabu hicho na baada ya mashauriano ya kina na wadau wa lugha hiyo, akaanza kuchapa kazi ya kufanikisha ndoto hiyo.

“Leo hii nimekuja kuelewa kuwa kuna pato nono katika uandishi wa vitabu. Kuna habari potovu ambazo husambazwa kuwa Wakenya wengi hawapendi kusoma vitabu lakini mimi ni shahidi kupitia uwepo wangu sokoni nikiuza kuwa kuna soko kubwa la uandishi hapa nchini,” asema.

Dkt Mugikunjo anafichua kuwa licha ya kurejeshwa kazini baada ya mwaka huo mmoja kuisha, alikuwa ameingia katika mkondo wa kujipa ukwasi mkuu kupitia kitabu hicho.

“Nilichapisha nakala 30, 000 za kwanza za kitabu hiki changu ambacho kimeandikwa kikilenga usomi wa watoto wa elimu ya msingi na ambapo kina hadithi saba,” asema.

Huku bei ya kitabu kimoja ikiwa ni Sh300 Dkt Mugikunjo anasema kuwa alisaka wadhamini wa kununua nakala hizo kwa bei ya Sh170 kwa kila kimoja na akafanikiwa kuuza zaidi ya nakala 25,000 ya kitabu chenyewe.

Bw Mwangi Mbuthia anayefahamika kama ‘Dkt Mugikunjo’ aonyesha kitabu alichokiandika kwa lugha ya Gikuyu. Picha/ Mwangi Muiruri

Anasema kuwa alikumbatiwa vizuri na wadau wengi wa lugha ya Gikuyu ambao wamekuwa wakifanya juu chini kufanikisha lengo la kuhifadhi lugha hiyo kwa vizazi vijavyo.

Anasema kuwa alifanya uamuzi wake kuwa safu hii ya uandishi vitabu iko na matumaini makuu ya kumpa ukwasi halali na ambapo anaapa kuwa kabla ya mwaka wa 2030 kutinga, atakuwa ameandika vitabu kadhaa akilenga kuuza nakala Milioni moja kwa Sh300 kwa kila kimoja na hapo aingie katika jumuiya ya Mamilionea.

“Hesabu ya haraka itakwambia kuwa nikifanikiwa kuuza nakala Milioni moja nitakuwa nimejipa pato la Sh300 milioni. Sio ndoto bali ni suala nimelijaribu katika mauzo ya kitabu hiki niko nacho sokoni kwa sasa; na kuna matumaini makuu,” asema.

Anawapa motisha waandishi wengine hapa nchini ambao wako na uwezo wa kuandika vitabu kwa lugha zao za mama kuwa wasiwe na wasiwasi kuhusu soko na pato.

“Tujumuike pamoja tuchafue soko na vitabu kwa lugha ya mama. Kufanya hivyo pia ni kusaidia taifa hili kutekeleza ibara ya 3(a na b) ya katiba yetu ambayo hulenga kuafikia kulinda na kuendeleza lugha asili nchini na pia utumizi wazo kwa kuendeleza nyaja za kilugha nchini mtawalia,” asema Dkt Mugikunjo.

Huku akimtambua msomi Prof Ngugi wa Thiong’o kama kielelezo chake, Dkt Mugikunjo anasema kuwa atafuata nyayo zake hadi aibuke gwinji katika uandishi wa vitabu na majarida kwa lugha ya mama.

Anasema kuwa safari yake ya kuafikia uandishi wa kitabu hiki chake cha kwanza ilimpa mwanya wa kufumbua kwamba lugha asili ziko na utajiri wa misamiati na kuna raha tele katika kuichambua.

Cha mno, asema, uandishi kwa kutumia lugha za mama kutasaidia Kenya na pia bara la Afrika kuhifadhi utamaduni wake wa kilugha, akiomba mataifa yawajibikie kauli mbiu ya Asmara (2000) ambayo ilipendekeza kuwa lugha hizi zitumiwe kwa kila njia ili kueneza maendeleo na utamaduni.

Anasema kuwa bara la Afrika kwa mfano huwa na lugha asili 2000 kati ya zote zaidi ya 6, 000 za Ulimwengu lakini hazitumiki kwa lolote lingine lolote la maana isipokuwa tu mawasiliano na utumbuizaji.

“Tunafaa tiukome huu ukonde wa kimawazo ambapo hatutumii lugha hizi kuzua faida katika riziki. Tunazitumia tu katika mawasiliano yetu ndani ya nyumba na vijiji lakini uwezo halisi wa kutupa ukwasi wa haraka na wa maana haujakumbatiwa kwa kiwango kinachostahili,” asema.