AKILIMALI: Mradi wa biogesi wapunguza gharama ya kuni shule tatu
Katika shule ya upili ya wasichana ya Kombeni katika kaunti ya Kilifi, Bw Albanus Mutuku anaonekana akikoroga mchanganyiko wa samadi na mkojo.
Uvundo wa aina fulani unatukaribisha hapo wakati tukikaribia zizi la ng’ombe katika shule hiyo yenye wanafunzi takribani 600.
Hata hivyo, ni katika uvundo huu ambapo mradi wa kwanza wa kutayarisha gesi kutoka kwa kinyesi cha mifugo hawa sasa umeanza kusaidia shule hiyo.
Ni mradi ambao ulianzishwa na serikali ya kaunti ya Kilifi na unafanyiwa majaribio katika shule tatu za kaunti hiyo. Shule hizo ni ile ya Kombeni, Malindi High na shule ya upili ya Godoma.
“Hapa tunatayarisha gesi kupitia kwa kinyesi ambacho tunatoa kutoka kwa ng’ombe hawa wanane ambao wako hapa.
Ng’ombe hawa mbali na kutoa kinyesi hiki ambacho tunatumia kutayarisha gesi, mabaki ya kinyesi hiki hutumika kama mbolea ambayo tunatumia katika shamba la shule,” akasema Bw Mutuku.
Bw Mutuku ambaye anasimamia mifugo hao katika shule hiyo alisema kuwa hata hivyo kiasi cha gesi ambacho kinatolewa na mifugo hao bado ni kidogo na akaomba waongezewe kifaa ambacho kitakuwa na uwezo wa kutayarisha gesi nyingi zaidi.
“Ombi letu ni kuwa licha ya usaidizi ambao serikali ya kaunti ilileta hapa, bado tuko na uhitaji zaidi na hivyo tunaomba tupatiwe kifaa chenye uwezo wa kuhifadhi gesi nyingi ambayo inawea kupikiwa kwa muda mrefu, hasa ikizingatiwa kwamba hii ni taasisi ambayo iko na watoto wengi,” akasema Bw Mutuku.
Afisa anayeshusika na masuala ya kawi katika serikali ya kaunti ya Kilifi Bw Wilfred Baya aliambia Akilimali kwamba kinyesi hicho huwekwa katika chungu maalum ambapo huchanganywa na maji au mikojo kisha baadaye ikorogwe na rojo la kinyeshi hicho limwagwe katika kifaa maalum chenye mirija ya kutengeneza gesi.
“Wakati gesi inapoendelea kutengezwa, yale mabaki hutoka katika bomba maalum na kuelekezwa katika shamba la shule kama mbolea. Kiasi cha gesi ambacho tunatayarisha hapa ni cha kiwango cha milimita 30. Kiwango hiki kinaweza kupika chakula cha wanafunzi kwa siku yote bila kutumia kuni wala makaa,” akasema Bw Baya.
Hata hivyo, afisa huyo alisema kuwa mradi huo unatekelezwa katika shule hiyo kama majaribio ambapo baadaye utapelekwa katika shule zingine katika kaunti.
“Hii ni mojawapo ya miradi ya kaunti kuhakikisha kwamba tunatumia kawi mbadala badala ya kutumia kuni na makaa.
Baada ya mradi huu kufaulu, tutauelekeza katika vijiji ili kuhakikisha kwamba wakazi wa Kilifi pia wanaacha kutumia kuni na makaa,” akasema Bw Baya.
Katika vijiji, familia zinaweza kutumia gesi ya kiasi cha milimita 12, gesi ambayo inaweza kutumika kupikia chakula na hata kupasha maji moto,” akasema.
Akiongea na Akilimali, Bw Jackson Nguwa ambaye anasimamia shamba la shule hiyo alisema kuwa tangu mradi huo uanzishwe mwaka jana, sasa wameimarisha mazao shambani na mboga zinapatikana kwa wingi shuleni.
“Awali tulitegemea mbolea ya kununua dukani. Kwa sababu ni ghali tulizoea kuweka kwa kubana, hivyo basi kuathiri mazao yetu. Hali kwa sasa ni tofauti na tunakuza mboga zenye afya. Hatununui tena mbolea kutoka dukani,” akasema Bw Nguwa.
Katika shamba hilo, tulipata kuna ndizi ambazo ziko na afya huku shamba hilo ambalo liko katika uwanja wa shule hiyo likiwa limejaa rotuba na mboga tele.
“Hapa mimi hukuza biringani, nyanya, sukuma wiki, mchicha, na ndizi. Mimea hii ili iweze kunawiri vyema inahitaji mbolea kama hii ya kienyeji na matokeo yake ni kama haya ambayo unayaona hapa,” akasema msimamizi huyo.
Katika eneo la jikoni, tulikutana na mpishi mkuu Bw Jospeh Muta ambaye alisema kuwa tangu mradi huo uanze matumizi ya kuni katika majiko yao umepungua.