• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
AKILIMALI: Mtambo wa kuangua mayai umeimarisha idadi ya kuku

AKILIMALI: Mtambo wa kuangua mayai umeimarisha idadi ya kuku

Na LUDOVICK MBOGHOLI

UFUGAJI wa kuku unahitaji umakinifu mkubwa, bidii na uvumilivu wa mfugaji mhusika.

Haya ni kwa mujibu wa mkulima wa mazao na mfugaji Zahra Ahmed Saad tuliyemhoji hivi majuzi wakati akiendelea na shughuli zake za ufugaji.

Zahra ambaye ni mkulima wa kujitegemea na pia kioo cha jamii za wakulima wa Mijikenda katika eneo la Kaskazini mwa Kaunti ya Mombasa, anasema shughuli za ufugaji kuku zina changamoto nyingi kiasi kuwa mfugaji asipokuwa makini anaweza kupoteza thamani ya ufugaji.

Bi Zahra Ahmed akiwa kwenye makazi ya ufugaji kuku katika eneo la Bombo, Utange, Mombasa. Picha/ Ludovic Mbogholi

Juhudi zake za ufugaji zilimwingiza kwenye ufugaji kuku wa kienyeji mbali na kumwezesha kujihusisha na ufugaji wa kuku wa kisasa.

Hata hivyo, anadokeza kuwa ufugaji wa kuku wa kienyeji ni mgumu zaidi kuliko wa kuku wa kisasa kutokana na ongezeko kubwa la athari za kutamausha.

“Nyama ya kuku wa kienyeji inapendwa mno kuliko ya kuku wa kisasa maarufu ‘kuku wa gredi’. Ladha ya nyama ya kuku hao wa kienyeji ni tamu mno ukilinganisha na utamu wa nyama ya ‘kuku wa gredi’ wanaopatikana kwa wingi katika masoko ya umma au kwenye maduka ya kuuzia nyama,” asema Zahra.

Maradhi

Anafichua kuwa ugumu wa ufugaji wa kuku wa kienyeji unatokana na maradhi ya maambukizi ya mara kwa mara ya ugonjwa wa ‘kideri’ unaoambatana na kuhara chokaa au kinyesi cha rangi nyeupe au cha majimaji.

Maradhi hayo huambatana pia na kukohoa au kuku kupiga chafya na kupoteza hamu ya kula na kunywa maji.

“Mfugaji hukumbana na changamoto hizo za maradhi, na asipojihadhari anaweza kupoteza kuku wote akose faida licha ya kuwagharamia kiasi kikubwa cha pesa,” asema Zahra.

Akizungumzia suala la afya ya kuku wa kienyeji, Zahra anatoa ushauri akisema mkulima anayeanza mradi huu anapaswa kuwaendea maafisa wanaohusika na ufugaji kuku ili aelekezwe vyema namna ya kuwatunza na kuwalisha, hasa vifaranga wa awali, ambao ndio wenye matatizo mengi ya kuugua kuliko wale waliokomaa.

Zahra anafichua kuwa huyanunua mayai ya kuku wa kienyeji na ya kuku wa kisasa halafu anayazalisha kwa kutumia mtambo wa kisasa wa kuyatamia na kuyaangua kabla ya kumpa vifaranga wenye afya.

“Mtambo ninaotumia unatoa kiwango cha joto la kawaida linalohitajika sawa na kiwango cha joto la kuku anayetamia mayai baada ya kuyataga,” asema.

Kwa ‘utamiaji’ na ‘uanguaji’ wa vifaranga kwa kutumia mtambo huo wa kisasa, Zahra anakiri mtambo huo huangua vifaranga baada ya kutamia mayai kwa siku 21 sawa na atamiavyo kuku aliyetaga.

Aidha, Zahra anasema siku mbili au tatu kabla ya vifaranga kuanguliwa, huyatoa mayai kwenye mtambo huo na kuyaweka pahala maalumu yakisubiri kuanguliwa.

Asema mfugaji anayetumia mtambo anaweza kuangamiza vifaranga ambao wako tayari kuanguliwa endapo atapitisha siku, au kutoa mayai kwenye mtambo kabla ya wakati wa kuanguliwa.

Kama njia ya kufanikisha shughuli za ufugaji kuku, Zahra ameajiri wahudumu wawili kwenye mabanda ya kuku wa kisasa na kienyeji huku akiwapa wahudumu hao ushauri wa jinsi ya kuwahudumia na kuwalinda afya zao dhidi ya maambukizi ya maradhi.

Mama huyu anaendesha shughuli zake za ufugaji kuku kwenye mabanda yaliyoko kwenye shamba lake huko Bombo eneo la Utange kaunti ndogo ya Kisauni mjini Mombasa.

Shughuli hii ya kufuga kuku tayari imemwezesha kufanikiwa pakubwa licha ya changamoto kadha kwa kadha.

“Nilianza kufuga kuku wa kienyeji wasiozidi watano na wa kisasa wasiozidi kumi kabla ya kupata mtambo wa kutamia na kuangua vifaranga, hatimaye nikaanza mradi wa kununua mayai ya kuku wa kienyeji na kisasa nikinuia mtambo uyatamie na kuyaangua kwa wakati,” asema.

Zahra amekuwa akiwalea zaidi ya kuku 4,000 wa kisasa na zaidi ya 3,000 wa kienyeji, lakini sasa anao kuku wa kisasa wasiozidi 1,000 na wa kienyeji wasiopungua 500 baada ya idadi kubwa kuuziwa wateja.

Anasema anafuga kuku wa mayai na wa nyama kibiashara.

You can share this post!

Serikali yakana njaa imeua Wakenya, madaktari wataka...

AKILIMALI: Maua kama mbinu ya kukabiliana na wadudu...

adminleo