Makala

AKILIMALI: Mwelimishaji wa kina mama afunzaye mbinu za kilimo na afya

March 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WAIGWA KIBOI

UNAPOTEMBELEA sehemu ya Gituamba iliyoko Lari, Kaunti ya Kiambu utavutiwa na hewa safi yenye baridi kiasi.

Wakazi wa sehemu hii ya Gituamba ni watu wenye bidii wanaojitafutia riziki ya kila siku kwa njia tofauti.

Wengi ni wakulima wadogo wa kuchanganya ukuzaji vyakula na ufugaji.

Ni hapa ambapo tunakutana na Rose Makimei ambaye anatueleza jinsi anavyowaleta pamoja akima mama wa sehemu hii na kuwafunza umuhimu wa kutumia maji safi ya kunywa ili kuepukana na magonjwa mengi yanayoletwa na utumiaji wa maji machafu.

Asema Rose: “Baada ya kukaa na wakazi wa sehemu hii kwa muda mrefu na kujua matatizo ya mara kwa mara, nilionelea nitilie maanani zaidi utumiaji wa maji safi ya kunywa. Ili kupunguza gharama ya kuchemcha ama kuweka maji dawa ya kuua viini, nimekuja na mpango ninaoupatia jina la Zawadi ya Dola 30 Kwa Kila Nyumba.”

Hii inamaanisha ya kwamba, kwa kila nyumba wenyewe wamepanda miti miwili ya kiasili na miche mitatu ya matunda yanayofanya vyema sehemu hii, watapewa mtungi maalum wa kutoa maji safi ya kunywa yasiyo na viini vyovyote.

“Kila mtungi unagharimu Dola 30 au Sh3,000. Ili mradi huu uanze, nimeongea na watu binafsi na makampuni mbali mbali na kuwahimiza waone umuhimu wa kuwapatia wengi maji safi ya kunywa na vilevile ukuzaji wa vyakula tofauti kwa afya ya jamii,” asema Rose.

Rose Makimei akihutubia akina mama wa Mwireri Women Group- Lari katika shamba lake sehemu ya Gituamba, Kaunti ya Kiambu kuhusu umuhimu wa afya bora, ukuzaji wa miti ya kiasili, matunda na mboga. Mitungi maalum ya maji safi iko mbele yake. Picha/ Waigwa Kiboi

Ombi la Rose kwa wakati huu ni watu wenye nia njema na makampuni wajitolee kwa njia zozote zitakazowafaidi watu wengi iwezekanavyo. Kwa sasa amepeana mitungi maalum sita ya maji safi.

Waliobahatika ni akina mama ambao tayari walikuwa wamepanda miti ya kiasili na miche ya matunda jinsi walivyoagizwa wafanye.

Jambo la kufurahisha ni kwamba hata wale ambao hawakupata bahati ya mtungi maalum walipendezwa na mipango hiyo na pia masomo mengi ya afya bora kwa jamii Rose aliwafundisha.

Katika siku ya leo tunalitembelea shamba la Rose, wengi wa akina mama ni kutoka kikundi cha Mwireri Women’s Group, Lari kikiongozwa na mwenye kiti wao Esther Wangui Karubia.

Yeye ni mama aliyejitolea kuwaunganisha akina mama wa sehemu hii na wameanza kujionea manufaa ya umoja wao.

Wanapofundishwa, akina mama hao huwa na maswali mengi kuhusu maisha na jinsi ya kuinua uchumi.

Jinsi idadi ya watu inavyoongezeka, ndivyo mashamba yanakuwa mandogo na ni lazima utumizi wa ardhi hasa kwa kilimo utiliwe maanani kwa kuongeza ujuzi zaidi.

Rose amekuwa akiwahimiza wawe wakitumia mbolea kutoka kwa mifugo na kuku ama matawi ya majani yanayooza ili kuepukana na magonjwa yanayotokana na fatalaiza na madawa ya kunyunyizia mimea.

Peter Kiiru Njoroge, mbaye ni mkazi wa sehemu hii, ndiye mwanaume pekee aliyejitokeza kuungana na akina mama katika kikao hiki. Maoni yake ni kwamba, wamama huwa ndio wanajitolea kwa mambo mengi na wakati umewadia kwa wanaume nao wajitokeze na kuwaunga wamama mkono kwa maendeleo.

Asema Bw Njoroge: ‘Unapompatia mama nafasi ya kujifunza mengi kuhusu kilimo, usafi na mengineo kuhusu maisha bora, watu wengi hufaidika kwa sababu ujuzi huo utasambazwa mbali. Hivyo ndivyo nchi hujiinua kiuchumi kwa sababu watu wengi wataungana kufanya mambo mengi ya maana.”

Kilimo na ufugaji

Rose anapogeukia kueleza yanayoendelea katika shamba lake lenye ekari 12, asema amejaribu kulima na kufuga ng’ombe na kondoo.

Licha ya hayo kuwa sawa, kuna wakati mambo huenda tofauti na matarajio yake hasa anapokuwa nje ya shamba lake kwa muda mrefu kulingana na kazi zake.

Ili kuepukana na hasara nyingi, aligeukia upandaji wa miti kwa wingi akipatiwa mawaidha na shirika la Kenya Forest Service (KFS).

Uhusiano wake na KFS ni wa manufaa kwa vile miti ikifikisha miaka ya kuvunwa, Rose atapata wanunuzi bila shida yoyote.

Ana zaidi ya miti 5,000 kati yake ikiwa aina ya pine, eucalyptus na cypress. Kuna matunda ya aina mbali mbali, mboga, kondoo na mizinga kadhaa ya nyuki.

Ametuzwa hapa nchini na Mama wa Taifa, Margaret Kenyatta, mashirika kama KFS, Total Eco-Challenge Award na nje ya Kenya amepata Green Apple Award aliyetunukiwa London, Uingereza katika Jumba la Bunge, Westminister, na akatajwa kama Balozi wa Green Apple 2019.

Rose amefanya mengi na anataka kufanya mengi zaidi kwa upandaji miti na kuinua afya ya jamii kupitia miradi ya akina mama.