AKILIMALI: Ng’ombe wa kisasa siri yake ya maziwa tele
PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA
JAMII ya Wamaasai inajulikana kwa ufugaji na wengi wa wanajamii husika humiliki idadi kubwa ya mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Na kwa sababu wao ni wafugaji wa kuhamahama; kusaka maji na lishe wengi wao hufuga ng’ombe wa kienyeji ambao wanaweza kutembea kwa mwendo mrefu bila kuchoka.
Gharama ya kuwatunza ng’ombe hawa wa kienyeji si ya juu ikilinganishwa na wale wa kisasa kwa sababu huwa nadra kwao kuathiriwa na magonjwa.
Lakini hali ni tofauti katika ranchi ya Mama Malelo Ipani iliyoko kando ya barabara ya Kitengela – Namanga, kilomita tano kabla ya kufika mjini Kajiado.
Malelo, kama anavyofahamika eneo hili, ni mwenyekiti wa Kundi la Wanawake la Osupuko, ambalo wanachama wake huendesha biashara ya kufuga nyuki, kunenepesha na kuuza fahali, kutengeneza na kuuza vipuli kwa kutuma shanga.
“Vilevile, tunafuga ng’ombe wa maziwa na kuendesha mpango wa kuweka fedha na kukopeshana miongoni mwetu, maarufu kama table banking,” alituambia tulipomtembelea hivi majuzi.
Wanachama wa kundi hili ambao wengi wao ni wanawake walioolewa na waume wenye wake wengi, huwa hawatembei na ng’ombe wao kutoka sehemu moja hadi nyingine, kama ilivyo ada katika jamii ya Wamaasai. Badala yake wao hufuga ng’ombe wachache ambao wao huwalisha karibu na maboma yao. Kwa kufanya hivi, wao hupata nafasi ya kufanya kazi nyingine za kuwaletea mapato.
Mnamo mwaka wa 2016 Malelo aliwauza ng’ombe wake wa kienyeji kisha akanunua ng’ombe mmoja wa maziwa, aina ya Freshian, hatua iliyoonekana kama kinyume na tamaduni za jamii hiyo.
Hii ni kwa sababu katika jamii ya Kimaasai, watu wanaomiliki ng’ombe wachache huonekana kama duni kwa sababu katika jamii ya Wamaasai ng’ombe si tu chanzo cha utajiri bali ishara ya hadhi katika jamii.
Huku akionekana mwenye raha, Malelo anasema kuwa hajuti kuenda kinyume na taratibu na tamaduni za jamii yake.
“Ng’ombe aina ya Freshian ni rahisi kutunza ikilinganishwa na ng’ombe 20 wa kienyeji ambao niliwamiliki zamani. Ng’ombe wa kienyeji wanahitaji eneo kubwa la malisho,” anasema, akiongeza kuwa ng’ombe huyo wa maziwa humletea faida kubwa kuliko ng’ombe 20 wa kienyeji aliowauza.
Ng’ombe huyo ambaye Malelo alimnunua kutoka kwa mkulima mmoja wa kaunti ya Kiambu kwa Sh150,000, hulishwa ndani ya shamba hilo ambako amepanda nyasi ya kisasa inayojulikana kwa kimombo kama “guinea grass”, “horsetail grass” na “African foxtail grass.”
Majirani wake hushangaa namna ameweza kutunza aina hizi za nyasi katika eneo hili ambalo hushuhudia kiangazi kwa kipindi kirefu kila mwaka.
“Aina hii ya nyasi inakuwa kwa haraka haswa wakati huu ambapo mvua imekuwa ikinyesha hapa kwetu kwa wingi,” anasema.
“Ng’ombe huyu alizaa ndama wa pili miezi mitatu iliyopita. Yeye hutoa lita 24 za maziwa kila siku; lita 12 asubuhi na lita 12 jioni. Na bei ya maziwa hapa kwangu ni Sh60 kwa lita moja,” Malela anasema, akiongeza kuwa huweza kuchuma Sh1,000 kila siku kutokana na mauzo ya maziwa.
Huku akionekana kufurahishwa na ufanisi aliopata katika kazi hii, Malelo anasema kwamba anapanga kununua ng’ombe wengine watatu aina ya Fresian.
Tayari ufanisi wake umewatia motisha wanachama watano wa kundi lake ambao wameamua kununua ng’ombe wa maziwa ili kuimarisha mapato yao.
Malelo anasema yeye huzingatia mbinu bora za utunzaji ng’ombe wa kisasa, kwa mujibu wa ushauri kutoka kwa wataalamu, kwa kumpa ng’ombe wake dawa za kuangamiza minyoo na kupe kila mara.