• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
AKILIMALI: Njugu, na udogo wake zilivyofaulu kumtimizia hitaji la pesa

AKILIMALI: Njugu, na udogo wake zilivyofaulu kumtimizia hitaji la pesa

Na GRACE KARANJA

LICHA ya kuwa na umbo dogo, njugu karanga zina ubora wa lishe na afya katika mwili wa mwanadamu.

Njugu husaidia katika kuongeza nguvu za uzazi kwa wanawake na pia wanaume; tafiti za mara kwa mara zikionyesha kwamba wanawake wanaokula njugu kila siku kabla na wakiwa wajawazito wana uwezo wa kupunguza matatizo ya mgongo kwa watoto wachanga kwa asilimia 70.

Pia kwa kula njugu zina asidi ambayo husaidia katika utengenezaji wa kemikali ambayo hupunguza mawazo mengi. Wengi hapa nchini wanaamini kwamba njugu karanga huongeza hamu ya ngono.

Mbegu za njugu zina mafuta asilimia 38 hadi 50, protini asilimia 25, Calcium na Vitamini.

Hujulikana sana katika matibabu ya kuharisha na mara nyingi mbegu hizi hukuzwa ili kukamuliwa mafuta ya kupikia. Keki ambayo hubaki baada ya mafuta kukamuliwa husagwa na kuwa unga ambao hutumiwa kama chakula ambacho kina protini.

Zinaweza kuliwa zikiwa mbichi au zikikaangwa kwa chumvi.

Uchina ndio nchi inayozalisha njugu kwa asilimia kubwa zaidi kwani nusu ya njugu zinazoliwa duniani hutoka nchi hiyo ikifuatwa na India, huku Nigeria ikishikilia nafasi ya kwanza hapa Afrika.

Wakulima wa Kenya hukuza zao hili kwa matumizi ya nyumbani na sio wengi wanaotilia maanani kilimo hiki.

Julius Macharia ambaye ni mzaliwa wa Kandara, Kaunti ya Murang’a anasema kuwa hana nia ya kubadilisha biashara hii ya kutayarisha na kuuza njugu karanga akieleza kwamba fedha anazopata baada ya mauzo zinamtimizia mahitaji yake.

“Niliamua kuuza njugu karanga kwa sababu ni chakula cha bei rahisi kinachopendwa na wengi hasa wa kutafuna. Naifanyia biashara yangu mjini Nairobi na vijana waache kunung’unika kila wakati wakisema kwamba hakuna kazi. Biashara hii nimeifanya kwa zaidi ya miaka mitano na badala ya kuzunguka nikitafuta kazi kwa ofisi, niliona nitulie, nijitolee kuchoka na ninapata pesa zinazoweza kukimu mahitaji yangu yote bila wasiwasi,” Macharia alisema wakati wa mahojiano na Akilimali.

Anaeleza kwamba wateja wa njugu hawachagui msimu wa kiangazi au baridi huku akirekodi mauzo ya juu kati ya mwezi Juni na Septemba kwani huu ni msimu wa baridi na watu wengi huamini njugu huongeza joto mwilini.

Julius Nduati akianika njugu zilizoloweshwa kwenye maji ya chumvi. Picha/ Grace Karanja

Nduati ni mtaalamu wa masuala ya mimea na anadokeza kwamba mimea hii hufanya vizuri katika maeneo ya joto la nyuzi 30 na kuongeza kwamba punde joto linapopungua hadi nyuzi 15 mimea hiyo hudumaa huku akionya wakulima dhidi ya kukuza mimea hii wakati wa baridi au mashamba yaliyo na maji mengi.

“Mimea hii huhitaji kiwango cha mvua cha 500mm hadi 600mm wakati wa kipindi cha kukuza, mmea huu hustahimili kiangazi na unaweza kuendelea kukua hata mvua ikipungua hata ingawa mazao yake yatapungua kwa kiasi,” anaeleza Nduati.

Mimea hii hukua kwenye udongo tifutifu (loam soils) lakini pia inaweza kufanya vizuri kwenye udongo wa ufinyanzi (clay soils) huku akiwaonya wakulima dhidi ya kuvuna njugu wakati kuna unyevu au mvua, hii ni kwa sababu mbegu hizi zinaweza kuambukizwa sumu aina ya aflatoxin ambayo ni hatari sana kwa mwanadamu.

Mtaalam huyu anashauri kwamba baada ya kutayarisha shamba vizuri mitaro ikatwe yenye upana wa sentimita 80 kisha mbegu zipandwe sentimita 5 hadi 8. Hekari moja inaweza kupandwa kilo 40 hadi 50 kulingana na ukubwa wa mbegu. Nduati anashauri kwamba mbegu za kupanda zihifadhiwe bila kuchambuliwa maganda yake hadi siku chache kabla ya kupanda.

Kuna aina mbili za mbegu ambazo hupandwa nchini ikiwa ni ile ya kichala mfano Red Valentia ambayo hukomaa kwa kati ya siku 90 hadi 100. Pia kuna ile ambayo hupwelea chini na hukomaa kwa kati ya siku 120 hadi 150. Wakulima wengi wana uwezo wa kuzalisha kati ya kilo 450 hadi 700 za njugu katika hekari moja lakini wataalam wanasema ikiwa wakulima watakubali kutafuta ushauri wa mbinu mwafaka za kilimo mazao haya yanaweza kuongezeka zaidi.

Kama mimea mingine, njugu zipaliliwe kwa wakati ili kuepuka ushindani mkubwa na kwekwe hasa zikiwa changa hii ikiwa ni majuma sita baada ya kuota. Magugu yote yatakayomea baadaye yang’olewe kwa kutumia mikono. Madini ya calcium huhitajika wakati wa kusawiri kwa maganda, hapa madini ya Nitrojeni hayastahili katika kukuza zao hili kwa sababu mmea huu una uwezo wa kujipatia nitrojeni.

Njugu kukauka

Punde mimea hii itakapokomaa njugu hukauka na kuwa ngumu huku maganda yake yakibandilika na kuwa ya rangi ya kahawia. Ng’oa mimea hiyo na kuiwacha kwa jua kwa siku 2 hadi 3 kisha dondoa mbegu kutoka kwa mmea na kuanika kwa chandarua kwa siku 7 hadi 10 hadi iwe na unyevu wa asilimia 10.

Kama anavyoeleza Macharia, soko la njugu liko tayari kila siku ingawaje inachukua muda mwingi wa kutayarisha. Yeye huchukua muda wa masaa manne kutayarisha ili zipendwe na wateja wake.

“Wateja hupenda njugu ambazo hazijaungua, mimi huchukua karibu nusu siku ili kuziandaa kazi ambayo sio rahisi hata kidogo, inahitaji uvumilivu sababu moja ambayo hufanya vijana wengi wasipende kazi hii,” anasema.

Biashara hii kama zingine haikosi changamoto kama vile bei ya juu na ukosefu wa makaa ambayo siku hizi hayapatikani kwa urahisi tangu serikali ilipopiga marufuku ukataji wa miti na uchomaji wa makaa nchini, akisema kwamba gorogoro moja ni Sh80 bei ambayo ni ghali sana. Pia wateja wengine huteta kwamba anapima kidogo sana.

Hata hivyo njugu karanga zina faida na yeyote anaweza kujiajiri. Anawataka wasio na kazi waingilie kazi hii akisema kila mwezi hakosi Sh40,000.

You can share this post!

AKILIMALI: Mbinu mpya ya kufuga samaki bila vidimbwi

Peter Munya ajipata njia panda ugenini Jubilee

adminleo