MAKALA YA SPOTI: Qubaa Muslim yaibuka dume wa mashindano ya QASHM kwa shule
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
SHULE ya Qubaa Muslim iliyoko mjini Mombasa, imeibuka mfalme wa kombe la QASHM kufuatia kampeni kali iliyoshirikisha shule za kibinafsi
Mbali na ushindi huo, wachezaji wa timu hiyo wamedhihirisha weledi katika kusakata soka, dhihirisho likiwa wanasoka wake wawili kusajiliwa na timu inayocheza ligi ya Mombasa.
Wachezaji hao ni kiungo Salim Abdulaziz na beki Osama Salim, ambao wamejiunga na kikosi cha kwanza cha Bodo Glimts FC inayocheza ligi ya Kaunti ya Mombasa.
Salim na Osama walikuwa kwenye kikosi kilichowqezesha Qubaa Muslim kuibuka washindi wa mashindano ya QASHM Cup, baada ya kuishinda timu ya Liwatoni Muslim kwa bao 1-0 kwenye mechi ya fainali iliyochezwa Uwanja wa Mbuzi.
Mwanzilishi wa mashindano hayo, Talip Ozdemir, ambaye pia ndiye kocha wa timu hiyo ya Qubaa Muslim, ameweza kutayarisha dimba hilo kwa miaka mitano sana huku timu yake ikifanikiwa kushinda mara mbili – 2016 na mwaka huu wa 2019.
“Nimeanzisha na kutayarisha mashindano haya kwa ajili ya kuwafanya wanafunzi wa shule za kibinfasi wapate kuendeleza vipaji vya uchezaji wao. Pia nia ni kuwatayarisha kuwa wanasoka watakaochezea timu maarufu hapa nchini na huko ng’ambo,” akasema Ozdemir.
Mkufunzi huyo wa Qubaa anasema mashindano hayo yanawasaidia maskauti wa klabu za Mombasa kushuhudia wale wenye talanta kwa lengo la kuwasajili kwenye timu zao.
“Nina uhakika wachezaji wengi ambao walikamilisha masomo yao tangu mwaka wa 2015, kwa wakati huu wanachezea timu nyingine zinazoshiriki ligi ya Mombasa na zile za mkoani Pwani,” akasema Ozdemir.
Alisifu jinsi chipukizi wake pamoja na wa timu nyingine zinazoshiriki mashindano hayo wanavyoendeleza vipaji vyao, hasa kutokana na kukubali kufuata maagizo ya wakufunzi wao na kudumisha nidhamu nyakati zote, wakiwa ndani na nje ya uwanja.
Timu nane zilizoshiriki kwenye dimba hilo ni Qubaa, Liwatoni, Abu Hurreira, Aga Khan High, Memon Academy, Light International, Bhadala Secondary na Sheikh Khalifa Secondary.
Qubaa ilianza kampeni yao ya mechi za Kanda ‘A’ kwa kuifunga Memon Academy 1-0, ikawalaza Light International kwa idadi hiyo ya 1-0 na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Bhadala Secondary.
Sare
Kwenye mechi ya nusu fainali, Qubaa ilitoka sare tasa na Sheikh Khalifa lakini ikapata ushindi wa mabao 6-5 ya mipigo ya penalti.
Katika mechi ya nusu fainali nyingine, Liwatoni iliifunga Light International kwa mabao 5-4 pia kwa mipigo ya penalti.
Wanasoka waliowakilisha Qubaa katika mashindano hayo ni Saad Abdulrahman, Abdulrahman Abdurahim, Osama Salim, Ahmed Bisher, Imran Fazi, Ali Abdalla na Mohamed Osman.
Wengine ni Salim Abdulaziz, Fadhloon Mohammed, Anas Ali, Liban Abdi, Agil Juma, Sajjad Bakari, Abdulbasit Mohammed, Aidarus Elyas, Noordin Said, Mohammed Abdi na Aufi Mohammed.
Ozdemir alisema kuwa mafanikio ya timu yake yametokana na ushirikiano mkubwa na uongozi bora wa shule hiyo chini ya Mkurugenzi Fatih Akdogan.
“Ninaamini vijana wangu wengi watatakikana na timu zinazoshiriki katika ligi mbalimbali Mombasa,” akasema.