AKILIMALI: Siri ya kufaulu katika ufugaji ng'ombe wa maziwa
NA RICHARD MAOSI
NG’OMBE aina ya Jersey ni aina mojawapo ya mifugo maarufu duniani kuwahi kufugwa na wakulima ikiaminika kuwa asili yake ni zaidi ya miaka 1700 iliyopita, nchini Uingereza.
Wanafahamika kutokana na mchanganyiko wa michirizi au mabaka meupe na meusi; rangi inayowatofautisha na Friesian.
Aidha ni wakubwa kwa kimo, watulivu na hawana tabia ya kutembea sana.
Uzani wa mifugo hawa ni zaidi ya ule wa ng’ombe wa kawaida ikiwa ni kati ya kilo 500-800 endapo watalishwa vyema na kuwekwa katika mazingira yenye baridi shadidi yanayoweza kuchangia ukuaji wa lishe ya wanyama (nyasi).
Akilimali ilizuru kaunti ya Nandi kutangamana na wakulima wanaoendesha kilimo cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa almaarufu kama Jersey.
Katika eneo la Biribiriet kaunti ya Nandi, mkulima Erick Kiprotich anaendesha shughuli za ufugaji kama kazi, akisema kazi ya kujiajiri ni bora kuliko ile ya kuajiriwa kwa sababu mfanyabiashara anaweza kujivunia faida yote.
Anaona afadhali wazazi kuwafundisha watoto wao ukulima mapema, na kuwahimiza kuwa na subira ya kuchanika kwa kazi za shambani badala ya kukimbilia kazi za ofisini ambazo ni haba kupatikana siku hizi.
Erick alianza ufugaji kati ya mwaka wa 2007-2009 na ndama wawili na ilichukua muda kabla ya kustawi na kuwa mkulima wa kupigiwa mfano. Alitafuta ushauri wa kitaalam ili kuteua mifugo mwafaka wanaoenda na hali ya anga kwenye Bonde la Ufa.
Aghalabu yeye huwalisha mifugo wake ndani kwa ndani, akisema mkulima anahitajika kuwa na vyakula vya kila aina endapo anatarajia kuvuna pakubwa kutokana na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
“Huwezi kuendeleza mradi wa kufuga ng’ombe kwa ajili ya maziwa endapo hauna nyasi za kutosha ambazo ni pamoja na michicha, kunde na wakati mwingine nafaka,” akasema.
Ni jukumu la mkulima kuotesha nyasi za kutosha na ikibidi anaweza kukodisha kipande kingine cha ardhi ili aweze kuotesha malisho ya ziada kisha akayakata na kupelekea mifugo.
Anasema siri kubwa ya kufanya ufugaji huu ni kuwa ni aina ya biashara ambayo haina ushindani wowote muradi mkulima aelewe jinsi ya kutekeleza wajibu wake.
Yeye hukama mara tatu na kiwango cha maziwa hutegemea msimu ambapo majira ya kiangazi lita za maziwa hupungua, na kuongezeka sawia msimu wa mvua nyingi ambapo bei ya lita hupanda na kupungua.
Kwa siku moja Erick anaweza kupata maziwa hadi lita 200 lakini wakati wa kiangazi idadi hii ya lita hupungua hadi lita 150 hivi, lakini bado anasema ni shughuli anayojivunia kwa sababu imemwezesha kuanzisha miradi mingine kama vile ukulima wa mahindi na maharagwe.
Alitufichulia kuwa ng’ombe hawa huwa ni wapole na ameamua kuwafuga katika sehemu tulivu kwani hawafai kutishwa na kitu chochote cha kuogofya kama vile kelele za viwanda na magari.
Ni mifugo ambao huwa na wakati mrefu wa kuishi na mahitaji yao sio mengi. Aidha, wao huchukua muda mrefu kuwanyonyesha ndama wao hadi wakomae na jambo hili hufanya ndama kunenepa na wanaweza kumpatia mkulima hela nzuri anapowauza.
“Pia wanaweza kustahimili hali mbaya ya anga na hawaathiriki na maradhi ya matiti kama ng’ombe wa Friesian wanaougua mara kwa mara maradhi ya miguu na midomo,” akasema.
Alisema kuwa mifugo wa Jersey huchukua muda mfupi kushika ujauzito na baadaye hujifungua kabla ya miezi kumi kinyume na ng’ombe wa kienyeji, wanaoweza kuchukua hadi miaka mitatu kabla ya kushika ujauzito.
Desturi hii imetoa awamu kwa mifugo wake kuzaana haraka baada ya muda mfupi na kufikisha zaidi ya ng’ombe 10 anaomiliki, wanaompatia maziwa, nyama na mbolea.
Anasema pia kuna faida nyingi ambazo mkulima anaweza kupata kutokana na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
“Mkulima anaweza kutengeneza hela pale anapouza samadi au anapowauza ndama wake kwa wakulima wanaofanyia majaribio ufugaji kwa ajili ya maziwa,” aliongezea.
Anasema ni lazima mkulima aelewa kuwa uzalishaji wa maziwa katika ng’ombe unategemea umbile la mifugo yako, ng’ombe wazito au wakubwa sana kimwili sana sio bora kwa kukama ila wanafaa kufugwa kwa sababu ya nyama pekee.
Mbali na ng’ombe kuzalisha maziwa anahitaji kuangaliwa kwa ukaribu, alieleza kuwa ng’ombe wa Jersey ambao ni chotara wana uwezo wa kufanya vizuri katika mazingira yoyote hata kama ni magumu.
“Kwa sababu mifugo wa asili si rahisi kupatikana siku hizi, ni vizuri mkulima kuwatafuta ng’ombe wa kisasa na kuwaboresha kutokana na upandikizaji na dume ili kuzalisha mifugo wanaoweza kustahimili uhaba wa malisho,” akasema.
Anasema kama utawafuga wanyama katika sehemu ndogo isiyokuwa na nafasi ya kutosha, basi utakuwa umewaweka katika hali ya usumbufu, ni vyema kuandaa shimo maalum la kuhifadhi samadi kabla ya kuzisafirisha katika shamba.
Kwa jumla, Kiprotich anasema ng’ombe wa maziwa wanahitaji kiwango kikubwa cha lishe na cha mara kwa mara ukilinganisha na mifugo wanaofugwa kwa ajili ya nyama.
Kwa sababu yeye hufuga mifugo wake kwa ndani (zero grazing) anajaribu kuhakikisha kuwa mazingira yao ni safi na pana ili kuwapatia uhuru wa kutembea.
Mapipa ya kuhifadhia maji ameyaweka karibu na vyanzo vya maji safi. Kila ng’ombe anahitaji kunywa lita 5-8 ya maji kila siku ambazo ni ndoo tatu hadi tano hivi.
Anasema ni vizuri kuwa na paa la kuwalinda mifugo dhidi ya hali mbaya ya hewa kama vile jua kali na upepo unaovuma bila mwelekeo maalum.