AKILIMALI: St Claire inavyohusisha wanafunzi katika kilimo kinachookoa gharama
Na RICHARD MAOSI
TAKRIBAN kilomita mbili kutoka mjini Naivasha tunakumbana na wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya St Claire of Assisi wakipalilia shamba lao lililojaa sukumawiki na spinachi wakati wa mapumziko mafupi.
Kilichotushangaza ni jinsi mimea yao ilivyojaa afya na kusheheni rangi ya kijani kibichi, ikizingatiwa kuwa eneo hili huwa na joto jingi tena ni rahisi mimea kunyauka.
Mwalimu wa somo la Zaraa, Bi Rosemary Kimani alitufichulia kuwa mbali na wanafunzi kushughulika na masomo yao ya kawaida, shule imewapa fursa ya kujiongezea ujuzi wa kustawisha mimea na kufuga sungura.
Kwa sababu wengi wao wanatokea mijini, ambapo hawawezi kujifundisha ukulima, hapa wanatumia njia nyepesi za kuhimiza wanafunzi kuenzi kilimo na matokeo yake yameonekana katika mitihani ya kitaifa kila mwisho wa mwaka.
Hatua chache ni kibanda cha sungura wanaowasaidia kutosheleza mahitaji ya shule hasa ijapo katika suala la kuongeza rutuba katika mradi wa shule.
“Mbali na mradi wa kufuga sungura kutumika kama nyenzo ya kufanikisha masomo, pia wanatumika kuongeza mbolea mchangani. Mara nyingi mbolea inayotokana na mkojo wa sungura ni ghali,” akasema Bi Rosemary.
Aidha, sungura wanasaidia kupunguza magugu yanayoweza kuangamiza mimea, wakati mwingi wao hula majani ya mboga na magugu ya aina yoyote yanayokuwa kandokando ya shamba.
Wanafunzi wa St Claire of Assisi hulisha sungura wao kati ya mara nne hadi tano kwa siku, wakitumia mchanganyiko wa lishe za kiasili na zile zilizonunuliwa kutoka viwandani
Bi Rosemary anasema pia hawahitaji kutembelea taasisi nyinginezo kujifunza spishi mbalimbali za sungura. Vilevile idadi ya sungura inapoongezeka baadhi yao huuzwa na kuongezea shule kipato.
Kipato hiki husaidia kukidhi mahitaji ya shule kama vile kununua vifaa vya maabara na kuongeza nakala za vitabu katika maktaba ya shule.
Kwa wiki, shule inaweza kuvuna zaidi ya kilo 100 za mboga, ambapo msimu huu kilo moja ni baina ya Sh100-150. Hivyo basi Sh15,000 huhifadhiwa kwa wiki moja ambazo ni Sh60,000 kila mwezi kwa mboga tu.
Aidha, shule haina gharama ya kununua mbolea kwa sababu ya sungura wanaotosha kukidhi mahitaji ya mbolea za Ammonia na Phosphorus kipindi chote, kuanzia mimea inapokuwa midogo hadi inapokomaa.
“Awali mchanga haukuwa na Ammonia na Phosphorus ya kutosha lakini tangu tuanzishe mradi wa kufuga sungura mambo yalibadilika,na tumefanya hili kuwa desturi,” Rosemary aongezea.
Anawahimiza wanafunzi kote nchini kupenda na kujivunia somo la kilimo, kwa sababu mbali na kupanua mawazo yao huwasaidia kuwa na mtazamo tofauti kuhusu zaraa.
Uwekezaji
Awali ilidhaniwa kuwa ni watu wanaoishi mashambani tu ndio walikuwa wakitekeleza kilimo lakini sivyo, kilimo kinaweza kufanya vyema mijini mradi washikadau watawekeza kikamilifu.
Kulingana na mwalimu mkuu Mugo Maina anasema ni mradi mzuri ambao pia umesaidia kuwapatia wafanyikazi wanne nafasi ya ajira, wanaohakikisha sungura wanalishwa vyema na pia kuwalinda dhidi ya wanyama hatari wanaoweza kushambulia makao yao.
Mwalimu Mugo anaongezea kuwa ni mradi ulioanza yapata miaka mitatu iliyopita na sungura mmoja lakini sasa wamezaana kiasi cha haja.
Baadhi ya sungura waliuzwa miaka ya mbeleni ili kutoa nafasi ya kuanza kufuga spishi za kisasa.
“Kwa wanafunzi wengine, ni mara yao ya kwanza kushiriki moja kwa moja katika ukulima na hili limetoa nafasi ya kupata ujuzi kwa kutangamana na wanyama,” Mugo aliongezea.
Spishi maarufu wanazofuga zikiwa ni zile za Carlifornia white na wale wa rangi ya kijivu, kwa hilo cha msingi lengo lao kuu ni kuwasaidia wanafunzi kuwa na mtazamo chanya kuhusu kilimo.
Watambue kuwa mtu anaweza kujiajiri na kuwaajiri wengine katika Nyanja ya kilimo endapo atayaelewa mahitaji ya soko na njia bora za kuendesha kilimo chenye tija.
“Kupitia makongamano na maonyesho ya kilimo wanafunzi wamekuwa wakijumuika na wenzao kutoka shule mbalimbali ili kujiongezea maarifa,namna ya kutunza mimea kama vile kunyunyizia maji,kupanda na kuvuna,” akasema.
Aidha shule huzawidi kitengo cha wanafunzi wanaopata mavuno mengi wakati wa uvunaji kama njia mojawapo ya kuwapatia moyo.
Kinyume na shule nyinginezo zinazowapa wanafunzi adhabu ya kulima kila wanapopotoka, Bw Mugo anasema hili halifai kwani huwanyima wanafunzi hamasa ya kuwajibika shambani.
Somo la zaraa katika shule ya wasichana ya St Claire of Assisi linaendelea kupata ufuasi mkubwa ikiwa ni zaidi ya nusu ya wanafunzi wanaofanya kilimo kama somo .
Miongoni mwa miradi mingine inayoendeshwa na wanafunzi hawa ni upandaji wa nyanya, vitunguu, kufuga ng’ombe wa maziwa na mradi wa kitalu ambao utaanzishwa hivi karibuni.