AKILIMALI: Tafuta soko la viazi asilia usahau uhaba wa hela mfukoni
Na SAMMY WAWERU
MAHITAJI ya viazi vitamu nchini Kenya yanaendelea kuongezeka hasa kwa sababu ya matumizi yake na faida kiafya.
Hata hivyo, ni wakulima wachache wanaovikuza.
Ni viazi asili vinavyoaminika kusheheni wanga na vitamini.
Pia vina madini mengine kama vile Potassium, Iron, Calcium na Zinc.
Soko lake jijini Nairobi ni mithili ya mahamri moto na hata katika miji mingine nchini.
Badala ya mkate wa boflo na vitafunio vilivyotengenezwa kwa unga wa ngano, wengi wamegeukia viazi vitamu hasa wakati wa staftahi.
Mapishi yake ni rahisi kwani vinahitaji kuchemshwa au kuchomwa kwa makaa moto.
Eneo la Magharibi mwa Kenya ndilo huzalisha viazi hivi kwa wingi. Busia, Bungoma, Kakamega, Homa Bay na Kisii, ndizo kaunti tajika eneo hilo katika ukuzaji.
Eneo la Kati, vinazalishwa kwa uchache, Kirinyaga ikiwa ndiyo inajikakamua.
Ikizingatiwa kuwa ni zao linaloweza kukuzwa maeneo yanayopokea mvua kiduchu, wataalamu wa kilimo wanasema viazi vitamu havina kikwazo cha udongo wala hali ya anga.
Maeneo mengi nchini yana udongo wenye rutuba, hususan ule tifutifu.
“Ule usioshikamana na kutotuamisha maji unawezesha mizizi yake ambayo ndiyo mazao kupenyeza ardhini, ikielekea chini,” anaeleza Bw James Kimemia, mtaalamu.
Kuna aina tofauti ya viazi vitamu. Vyekundu juu ndani vyeupe, vyekundu juu ndani manjano na vyeupe juu ndani manjano.
Vile vyekundu juu na ndani manjano ndivyo vina soko la haraka.
Kuna aina ya KeMbu 10, KeMbu 20, na Kenspot 4 na Kenspot 2, kwa mujibu wa maelezo ya Bw Kimemia.
Kulingana naye viazi vitamu ni rahisi mno kupanda.
Hauhitaji mbolea wakati wa upanzi wala dawa yoyote kukabiliana na wadudu kwa sababu ni vigumu kuathiriwa.
“Cha msingi, ni kufuata maelekezo ya mtaalamu na kuvipogoa (prunning) ili kupata mazao bora,” ashauri mdau huyu, akihimiza maeneo kame kukumbatia ukuzaji wa viazi hivi ili kukabiliana na upungufu wa chakula haswa msimu wa kiangazi.
Sawa na mihogo, mtama na wimbi, viazi vitamu pia vinastahimili kiangazi.
Mfumo unaotumiwa na wengi katika upanzi wa viazi hivi ni ule wa kuandaa mashimo au mitaro.
Hata hivyo, Kimemia ambaye pia ni afisa wa kilimo kaunti ya Murang’a anasema upandaji kwa njia ya kuinua udongo ili kuunda mtaro na ‘mlima’ (ridges), ndio bora na rahisi na kwamba huongeza kiwango cha mazao.
“Udongo uinuliwe kuunda mfano wa mlima hadi karibu futi mbili,” asema. Anashauri kwamba iwapo mkulima ana lazima ya kutumia mbolea, ya mifugo itumike.
Anaendelea kueleza kwamba mbolea imwagwe kabla ya upanzi na kuchanganywa vyema na udongo.
“Mlima mmoja hadi mwingine, kati yake uwe na nafasi ya hadi futi nne,” aeleza.
Kinachotia motisha katika ukulima wa viazi vitamu ni kuwa hauna gharama mbegu. Matawi yake (cuttings) ndiyo mbegu, na Kimemia anapendekeza yenye urefu wa karibu futi moja yapandwe. Mkulima atayapata kutoka kwa anayevipanda, na wengi hupeana bila malipo.
Wakati wa mahojiano na Akilimali katika maonyesho ya kilimo yaliyofanyika Mariira Farm, Murang’a mwaka huu 2019, afisa huyu alisema matawi yapandwe katika kilele cha vilima vilivyoandaliwa.
“Yapandwe kwa kulalishwa, nusu futi kuenda chini. Nafasi kati ya matawi iwe futi moja,” akaeleza.
Maonyesho hayo yalihudhuriwa na wataalamu na wakulima kutoka dira tofauti za nchi, wakiwemo wanafunzi.
Bw Kimemia alihimiza haja ya kudhibiti ukuaji wa kwekwe kupitia palilizi. Alisema huleta ushindani mkali wa maji, mbolea na miale ya jua, ambayo ni mahitaji muhimu katika kupata mazao bora.
Changamoto
Changamoto kuu katika kilimo cha viazi vitamu ni shambulizi la fuko.
Fuko ni wanyama wanaoorodheshwa katika himaya ya Animalia, na ambao huandaa makazi yao udongoni na kuishi humo takriban maisha yao yote.
Ni waharibifu kwa mimea yenye mazao yake udongoni.
“Ni tishio kubwa kwa wakulima. Wamenihangaisha, kila viazi vinapoanza kuzaa wanyama hawa huvila na kunisababishia hasara,” analalamika Mary Wairimu, mkulima wa viazi hivi Kirinyaga.
Kimemia anasema kando na kujaribu kuwakabili kwa dawa, mitego ndiyo njia bora ya kuwadhibiti. Kuna mitego maalum inayoundwa kwa minajili ya kuwanasa. Hata hivyo, itahitaji mkulima atambue njia za fuko hao ili kuwakamata.
Viazi vitamu huwa tayari kwa mavuno miezi mitano baada ya upanzi. Mtaalamu huyu anasema ekari moja iliyotunzwa vizuri ina uwezo wa kuzalisha kati ya tani 7 hadi 10.
Kilo moja huuzwa kati ya Sh50 hadi Sh100. Gunia la kilo 90 halipungui Sh2, 500 na wakati vimeadimika hupaa hadi zaidi ya Sh4, 000.
Ili kupata soko lenye mapato, mkulima anahimizwa kufanya utafiti mwezi mmoja kabla ya mavuno. Pia ni muhimu kutumia mitandao ya kijamii kutafuta wateja, katika makundi ya soko la mazao ya kilimo.
Hali kadhalika, ni muhimu wakulima kukumbatia mfumo wa kuongeza mazao thamani ili kukwepa kero la mawakala ambao wamezorotesha soko. Viazi vitamu vinaweza kukaushwa na kusagwa ambapo unga wake unaweza kutumika kuandaa vitafunio kama vile chapati, keki, mahamri, na biskuti.