AKILIMALI: Taswira ya kilimo cha mjini
Na RICHARD MAOSI
MTINDO wa kukuza mboga za majani, viungo vya lishe (dania, pilipili, na vitunguu) na kufuga wanyama mijini almaarufu kama Urban Farming ni ajenda mojawapo ya serikali, kuhakikisha kuwa Kenya inajitosheleza katika sekta ya kilimo.
Wakazi wa mijini wakihimizwa kuzingatia nyenzo kama hizi kujizalishia chakula cha kutosha ili kutengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana wengi wanaosumbuka mijini na kupigana na umaskini.
Wakazi wengi wa Nairobi, Kisumu na Mombasa wameanza kukuza mimea katika makazi yao rasmi hususan mboga za kiasili kama vile managu, suja, mrenda, spinach na sukumawiki na kupiga teke suala la uagizaji wa mazao ya shamba kutoka masoko ya nje.
Hii ni kwa sababu wakati mmoja ilibainika kuwa baadhi ya wafanyabiashara kutoka Nairobi, wamekuwa wakitumia maji taka kukuza sukumawiki kando ya barabara, na kupata pesa za haraka, jambo linalohatarisha afya ya wanunuzi.
Aidha, kuzuka kwa maradhi sugu kama vile saratani kumekuwa kukihusishwa moja kwa moja na baadhi ya vyakula vinavyouzwa sokoni, huku baadhi yavyo vikiwa vimeshamiri madawa ya kupulizia.
Ni kwa sababu hiyo kijana Dennis Mureithi na babake Daniel Gitau kutoka Gatundu kaunti ya Kiambu wameamua kutengeneza vifaa mfano wa magurudumu, vinavyoweza kujazwa udongo uliochanganyika na mbolea ya aina yoyote iwe samadi ama kinyesi cha kuku kwa minajili ya kukuza mimea.
Mimea yenyewe inaweza kutumika nyumbani ama kuuzwa sokoni kulingana na lengo la mkulima kuendesha Urban Farming katika eneo lake.
Tulikutana na Mureithi katika eneo la Muthaiga North ambapo ametengeneza sehemu ambayo anafanyia majaribio ya mradi wake huu na tayari amepata mafanikio kwa kusambazia wakulima wengi katika jiji la Nairobi hususan mitaa ya Karen na Muthaiga.
Kulingana na Mureithi anasema kuwa ongezeko la idadi ya watu nchini (takriban milioni 47), limemsukuma binadamu kubuni njia mbadala ya kulisha watu vyakula vyenye afya, vilivyosheheni virutubishi vya asilia kutoka mchangani badala ya kutegemea lishe kutoka viwandani.
Anasema Urban Farming itasaidia watu wanaokaa mijini kupata mboga za majani na matunda mara kwa mara, na kupunguza uwezekano wa wananchi kupata maradhi ya moyo , kisukari na uzito wa mwili kupita kiasi.
Aidha itawasaidia vijana kujianzishia miradi midogo ya kijiongezea kipato kwa mtaji mdogo wa Sh2,500, badala ya kutegemea kazi za kuajiriwa ambazo siku hizi ni nadra kupatikana.
Kwa Sh2,500 Mureithi amekuwa akiwatengenezea wakulima mijini, ngazi sita za magurudumu haya yaliyojazwa mchanga na mbolea kwenda juu, akieleza kuwa mtindo huu ni bora kuliko utumiaji wa shamba la kawaida, kwa sababu zifuatazo:
“Kwanza Urban Gardening ni bora zaidi ya mara 10 ikilinganishwa na mtu anayekuza mimea yake katika shamba la kawaida na tumepata ushahidi wa kutetea hayo,” akasema.
Anasema akishirikiana na taasisi za kufanya utafiti, shule za upili na msingi na makazi ya watu binafsi, amekuwa akiwasaidia vijana kupata ujuzi jinsi ya kutengeneza magurudumu haya na kuyasambaza nchini, ambapo baadhi yao wamejitengenezea nafasi za kazi.
Anasema wakulima wengine wamekuwa wakiendesha kilimo hiki ndani ya kitalu, ijapo haja ya kuzuia vidudu, mmomonyoko wa udongo na mkurupuko wa maradhi hasa kwa mazao kama nyanya, yanayohitaji uangalizi wa hali ya juu.
Mureithi alitoa mfano wa kilimo ndani ya magurudumu haya ambayo katika kipande cha nusu ekari ya shamba mavuno ndani ya magurudumu haya ni sawa na mavuno yanayopatikana katika shamba la ekari tano.
Akisema kuwa huweza kumsaidia mkulima kutumia nafasi ndogo ya shamba ipasavyo na anaweza kukuza aina tofauti ya mimea.
Mureithi anasema alibuni vifaa hivi ili kuhakikisha kuwa wakulima wanaweza kutumia nafasi ndogo inayoweza kupatikana mijini kujiongezea kipato, akidai kuwa siku hizi gharama ya kukodisha shamba imekuwa ghali sana.
Akizungumza na Akilimali alifichua kuwa analenga miji yote mikuu nchini akisema vifaa hivi ni bora kuliko shamba la kawaida kwa sababu mimea mingi ya aina tofauti inaweza kufanya vyema kwa wakati mmoja.
Mureithi anahimiza serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na zile za kaunti kuwekeza katika miradi kama hii mijini na kutenga sehemu maalum za kufanyia utafiti namna ya kuboresha kilimo cha mijini.
Isitoshe anaomba serikali kuwahimiza vijana kujiingiza kikamilifu katika ukulima kwa sababu ndio uti wa mgongo kwa mataifa yanayoendelea kukua.