• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
AKILIMALI: Ufugaji wa sungura umempa upekee jijini

AKILIMALI: Ufugaji wa sungura umempa upekee jijini

Na PETER CHANGTOEK

SUALA la ukosefu wa ardhi au shamba la kuziendeshea shughuli za kilimo huwa ni kikwazo kikuu, aghalabu katika maeneo ya miji na majiji makuu si tu nchini, bali pia katika nchi nyinginezo.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaoishi mijini huvitumia vipande vya ardhi hata viwe vidogo kiasi gani, kukiendeleza kilimo na kujiruzuku.

Baadhi yao hushughulikia ukuzaji wa mimea tofauti tofauti, ilhali wengine hushughulika na ufugaji wa mifugo, mathalani; ng’ombe wa maziwa, mbuzi, kuku, sungura, mabatabukini, mabatamzinga, kanga, miongoni mwa mifugo mingine.

Lazaro Tumbuti ni mmojawapo wa wale wanaotumia sehemu ndogo ambazo ni nadra kupatikana kuendeleza shughuli za zaraa.

Yeye hushughulikia ufugaji wa sungura katika eneo la Lunga Lunga, Viwandani, jijini Nairobi.

Alianza kufanya shughuli hii mwaka 2019.

“Nilianza na sungura wanne; mmoja wa kiume na wengine wa kike. Niliwanunua kutoka kwa marafiki hapa mtaani, lakini kuna mmoja niliyemleta kutoka nyumbani,” afichua mfugaji huyo.

Anasema kuwa aliwanunua sungura hao kwa bei ya Sh500 kila mmoja; wote wakiwa wadogo. Kwa kuwa alikuwa limbukeni katika shughuli hii, aliwaacha sungura hao wote katika kibanda kimoja pasi na kuwatenganisha, na alipigwa butwaa alipogutuka siku moja na kupata idadi ikiwa imeongezeka baada ya vitungule (wanasungura) kuzaliwa.

Mfugaji huyo hutumia masalio ya mboga kama vile sukumawiki na kabeji anayokusanya kutoka kwa wauzaji wa mboga mtaani kuwalisha.

“Nilikuwa nimejaribu kuwapa chakula cha madukani, lakini kina gharama ya juu. Kuna chakula cha sungura ambacho kinakaa kama mchele. Ukienda hapa Pembe utauziwa kilo kumi kwa Sh500, na ukiwa na sungura wengi, gharama huwa kubwa. Niliona ni heri niendelee tu kuwapa sukumawiki,” asema, akiongeza kuwa alikuwa akizitumia lishe hizo kwa muda wa wiki moja tu.

Tumbuti anasema changamoto kuu ni magonjwa wakati wa mvua.

“Wakati kuna baridi na unyevunyevu sungura huwa wagonjwa, lakini wakati kuna jua, magonjwa si mengi,” adokeza mfugaji huyu mwenye umri wa miaka 32.

Miongoni mwa magonjwa hayo ni pamoja na kupooza miguu, vidonda vya masikioni, kufura kwa macho n.k.

Anadokeza kuwa yeye huwapeleka sungura wake kwa daktari ili awape dawa anazofaa kuzitumia kuwatibu sungura wake. Aidha, kwa wakati mwingine humchukua daktari wa mifugo ili awakague wanyama hao.

Mfugaji huyo anasikitika kuwa sungura wake wengi wamewahi kufa kutokana na magonjwa mbalimbali. Anasema kwamba kuna wakati wa mvua ambapo alikuwa akiwapa lishe zenye maji mengi, jambo lililosababisha kuvimbiwa tumboni na kufa.

“Wale wadogo wenye umri wa wiki tatu ndio waliokuwa wakifa sana,” aongeza mfugaji huyo.

Awali, sungura wake walikuwa wakiongezeka kwa kasi kwa sababu hakuwa akiwatenga wa kiume na wa kike, hivyo walipata fursa aula ya kujamiiana na kuongezeka upesi mno.

Hata hivyo, mfugaji huyu anasema kuwa kwa wakati huu, yeye huwafungia sungura wa kiume katika kibanda tofauti huku wale wa kike wakiwekwa katika sehemu yao.

“Wanapozaliwa ninawaacha kwa muda wa mwezi mmoja halafu ninaona kama ni wa kike au kiume na kuwatenganisha,” aongeza.

Tumbuti anafichua kwamba yeye huwauza sungura wake baada ya kuwapima kwa kilo.

“Kwa mfugaji ambaye anataka kuwafuga, mimi humuuzia kwa Sh800, na kwa wale ambao wanataka sungura wa kuliwa huwauzia kwa Sh650 kwa kilo moja,” asema mfugaji huyu, akiongeza kuwa sungura mmoja anaweza kufikisha uzito wa kilo tatu anapokomaa.

Hata hivyo, kuwapata wateja wanaotaka kununua nyama ya sungura huwa ni vigumu mno, na ameamua kuitangaza biashara hiyo mitandaoni, ili kuwavutia wateja wengi.

Mfugaji Lazaro Tumbuti akionyesha baadhi ya sungura wake katika eneo la Lunga Lunga, Nairobi. Picha/ Peter Changtoek

Yeye humuuza sungura mmoja mwenye umri wa mwezi mmoja na nusu kwa bei ya Sh500, na yule mkubwa kabisa humuuza kwa Sh800.

Mfugaji huyo anafichua kuwa amewahi kuwa na sungura 80, japo idadi imepungua kwa wakati huu, kwa sababu baadhi yao hufa wakati wa mvua, kutokana na maradhi, huku akiwauza wengine.

Licha ya kupata mbolea pamoja na mkojo kutoka kwa sungura wake, mfugaji yuyo huyo anasema hajawahi kupata wateja wa kuwauzia, na hivyo kushurutika kuumwaga mkojo huo pamoja na mbolea.

Mfugaji huyo anapania kujitosa katika ufugaji wa kuku pia, kwa sababu kupata soko la kuwauza kuku huwa si vigumu sana. Tayari, ameanza kuwafuga kuku kadha wa kadha karibu na eneo hilo anakowafugia sungura.

Tumbuti anadokeza kuwa yeye hulipia kodi ya Sh3,000 kukitumia kipande cha ploti anachotumia kuwafuga sungura hao.

Mfugaji huyu anasema shule ya upili ya Star of Hope, ambayo huwapeleka wanafunzi kujifunza kuhusu ufugaji wa sungura katika eneo hilo. “Pia huja kuchukua mkojo na mbolea kutumia kufanyia ukulima shuleni,” asema, akiongeza kwamba wao pia hununua sungura wa kufanyia upasuaji kwa ajili ya mafunzo kwa wanafunzi.

Anawashauri vijana kujitosa katika shughuli mbalimbali za kilimo, hata kama wana ardhi ndogo, badala ya kuhangaika na kufadhaika wakizitafuta ajira.

Mbali na shughuli ya ufugaji wa sungura na kuku, mfugaji huyo pia anaazimia kujitosa katika ukuzaji wa mimea kwa kutumia kivungulio (greenhouse).

  • Tags

You can share this post!

Sonko agawanya ODM

Thiwasco yaimarisha huduma ya usambazaji maji Thika

adminleo