AKILIMALI: Ujuzi wa kupanga maua nyumba za kifahari wamuinua
Na SAMUEL BAYA
KILOMITA mbili kabla ya kufika mjini Kilifi kutoka Mombasa, kuna eneo linalojulikana kama Mnarani Garden Centre.
Ni hapa ndipo Fikirini Katana amekuwa akijipatia riziki kwa miaka kadhaa sasa.
Akiwa sasa ana umri wa miaka 29 na baba ya watoto wawili, hufanya shughuli za kurembesha nyumba za kifahari, kwa Kimombo ikijulikana kama ‘landscaping’.
Vilevile, yeye huunda vyungu vya kuwekea maua kama mojawappo ya kuongeza pato katika shughuli zake za kila siku.
Tulipozuru katika eneo hilo tulimkuta akiendelea kushughulikia baadhi ya vyungu vyake ambavyo baadaye huuzia watalii na mabwanyenye. Baadaye yeye hupewa fursa ya kwenda kurembesha nyumba hizo na kuweza kujikimu kimaisha.
“Tuko na oda ya kupeleka vyungu vya maua vyenye thamani ya Sh80,000 hadi jijini Mombasa. Ndio maana unaona tuko mbio mbio,” akasema Katana. Katika karakana yake hiyo, ameajiri vibarua ambao huja na kuunda vyungu hivyo, akiwalipa wanapomaliza. Kisha yeye baadaye huvipeleka kwa wateja.
Lakini zaidi, kijana huyu alisema kuwa kazi yake kuu ni kutayarisha na kupanga maua katika mitaa ya kifahari na hajutii kazi hiyo akisema iko na pato la kutosha. “Kazi yangu hasa ni kupanga maua katika mitaa na nyumba za kifahari. Lakini huwezi kuitelekeza vyema kama huna vyungu vya kuweka maua hayo na ndio maana nikaanzisha biashara hiyo pia. Kwa ufupi katika karakana hii niko na biashara mbili ambazo zinaendana kwa wakati mmoja,” akasema Katana.
Alisema kuwa mojawapo ya masuala ambayo yamemtia motisha ni jinsi ambavyo ameendelea kupata sifa kutoka kwa wateja wake ambao wamemsifia kwa kazi nzuri. Biashara yangu kwa sasa iko na thamani ya Sh12 millioni na kwa siku nzuri, mimi hupata kipato cha Sh100,000 katika mauzo,” akasema.
“Nilianza kazi hii katika mitaa ya Kiwandani mjini Kilifi lakini sasa nimeweza kujistawisha na kuwa na wateja ambao uwezo wao wa kuwahudumia uko juu zaidi. Mara nyingi mimi hupata oda ya kurembesha nyumba nyingi ndani na nje ya kaunti ya Kilifi,” akasema.
Baadhi ya wateja ambao wamewahi kununua bidhaa zake ni pamoja na wakili wa Mombasa Bw Tawfiq Balala pamoja na mwanasoka maarufu nchini Bw Macdonald Mariga.
“Nilienda kumrembeshea nyumba Mariga katika mtaa wa kifahari wa Vipingo na alifurahi sana na kunipongeza. Kisha Balala pia amekuwa mteja wangu wa muda mrefu akinunua vyunbu vya maua katika eneo hili. Pia nimefanya miradi mingine mingi ya kurembesha nyumba katika Kaunti ya Mombasa na imefaulu sana,” akasema Katana.
Chungu kikubwa cha kuwekea maua kinauzwa kwa Sh5,500, ilhali kuna vyungu vyingine alivyosema vinaweza kugharimu kati ya Sh10,000, lakini kulingana na ukubwa wake. “Mimi hulipisha kati ya Sh25,000 hadi Sh70,000 kurembesha nyumba na mara nyingi hili litategemea na ukubwa wa nyumba na eneo lenyewe. Kuna aina nyingine za kurembesha nyumba ambazo zinahitaji utaalamu zaidi na hiyo pia iko na gharama yake,” akasema.
Tulipotaka kujua jinsi alivyojipata katika shughuli hii, Katana alisema kuwa yote yalitokana na yeye kuzaliwa katika familia ambayo inapenda sana masuala ya maua katika eneo la Kiwandani.
“Nilipokuwa nikikua katika eno hilo niliona maua ya kupendeza sana. Yalinivutia na mara nyingi nilijifundisha kuketi kwa muda nikiangalia jinsi nyuki na wadudu wengine wanavyoyazunguka,” akasema kwenye mahojiano na Akilimali.
Alisema familia ilimpatia jukumu la kufyeka magugu katika maua hayo na kila alipokuwa akitekeleza jukumu hilo, ndivyo ari ilizidi ya kutaka kuingiia zaidi kazi hiyo.
“Siku moja nilipata kazi ya kupalilia maua kwa jirani na pesa nilizopata zikanifungua macho na kuona kwamba biashara hii inaweza kulipa vyema,” akasema.
Jamaa huyu aliacha masomo ya sekondari akiwa kidato cha kwanza baada ya kukosa karo lakini akasema kuwa alijipatia moyo na kuamua kuingilia kazi anayofanya hadi leo hii.
“Ninapanga hata hivyo kurudi tena darasani niendelee na masomo yangu,” akasema.
Anawataka vijana wafanye kazi kwa bidii na kutumia talanta ambazo wako nazo kufanikisha ndoto zao za maisha. Aidha alisema ni jambo la kutamausha kwamba katika enzi hizi, bado kuna vijana ambao wanadhani maisha yatawanyokea bila kuweka bidii.