• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
AKILIMALI: Ukuzaji wa pilipili mboga ni kitega uchumi hakika

AKILIMALI: Ukuzaji wa pilipili mboga ni kitega uchumi hakika

Na PETER CHANGTOEK

KEN Lagat amekuwa akishughulika na ukuzaji wa mimea mbalimbali kwa muda mrefu.

Amekuwa akishughulikia ukuzaji wa mimea mfano wa sukumawiki, kabichi, mnavu, pilipili manga, na pilipili mboga, pamoja na mimea mingineyo.

Alianza kujihusisha na masuala ya ukuzaji wa nyasi aina ya ‘hay’ kabla ya kujitosa katika ukuzaji wa mimea hiyo.

“Niligawagawa shamba kuwa sehemu ndogo ndogo. Sehemu nyingine nilipandia sukumawiki, nyingine mnavu, nyingine pilipili, kabeji,’’ asema mkulima huyo, ambaye anasakini katika eneo la Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu.

Hata hivyo, kati ya mimea hiyo yote, mkulima yuyo huyo anasema kuwa mmea uliokuwa ukimpa faida nyingi zaidi ni pilipili mboga, ndiposa akaamua kujitosa kikamilifu katika shughuli ya ukuzaji wa mmea uo huo, mnamo miaka mitatu iliyopita.

“Mimi hukuza pilipili mboga aina ya F1,’’ afichua mkulima huyo mwenye umri wa miaka 35.

Ken Lagat akiwa katika shamba lake la mimea ya pilipili mboga, katika eneo la Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu. Picha/ Peter Changtoek

Yeye huzinunua mbegu za pilipili mboga kutoka kwa kampuni tofauti tofauti kama vile Amiran, Syngenta, Continental na nyinginezo.

“Zenye zinafanya vizuri ni za Amiran na Continental. Ninaagiza za Continental moja kwa moja kutoka Nairobi. Kuna maduka ya kuuza mbegu za Syngenta huku Eldoret,’’ asema mkulima huyo.

Anaongeza kwamba yeye huziagizia mbegu za pilipili mboga za kampuni ya Amiran moja kwa moja kutoka Nairobi, kisha hutumiwa kutoka kwa kampuni hiyo.

“Amiran huzihesabu mbegu. Kwa mfano, mbegu 1,000 kwa Amiran, mimi huzinunua kwa Sh7,000. Mbegu moja ni Sh7,’’ asema akiongeza kuwa yeye huzipanda mbegu hizo kwenye kitalu, baada ya kuzinunua.

Lagat anasema kwamba mbegu za pilipili mboga, baada ya kupandwa huchukua muda wa miezi miwili kwa kitalu kabla miche kutoka kwa mbegu hizo kuota na kupandwa katika shamba lililotayarishwa kwa kulimwa ipasavyo.

Hata hivyo, anasema hilo hufanyika tu iwapo hali ya anga ni shwari; kama kuna baridi, miche huchukua takribani siku 75 kabla haijapandikizwa.

Mkulima yuyo huyo anadokeza kwamba yeye huligawanya shamba lake kwa vipande tofauti, ambapo katika kila kipande yeye huipanda miche mia tatu. “Kwa kila kipande, mimi huipanda miche karibu mia tatu. Kwa hivyo, ekari moja huwa na vipande hamsini,’’ asema Lagat.

Aidha, mkulima huyo huipanda miche ya pilipili mboga kwa kuacha nafasi ya sentimita 60 kwa sentimita 45, japo wataalamu hupendekeza kuwa miche hiyo inafaa kupandwa kwa kuacha nafasi ya sentimita 60 kwa sentimita 60.

“Wanasema upande miche 10,000 kwa kuacha nafasi ya sentimita 60 kwa 60, lakini mimi huipanda miche 15,000 kwa kuacha nafasi ya sentimita 60 kwa 45,’’ asema Lagat, ambaye ni baba wa watoto wawili.

“Ukiacha nafasi kubwa kubwa, inazaa halafu inaanguka,’’ adokeza mkulima huyo. Anaongeza kuwa yeye mwenyewe hujifanyia kazi nyingi shambani.

Lagat anafichua kuwa mbegu anazozipanda katika shamba ekari moja ni ghali na humgharimu takribani Sh16,000. Anaongeza kuwa mche mmoja wa pilipili mboga huuzwa kwa Sh5.

“Hata saa hizi ukitaka kuinunua miche ya pilipili mboga aina ya F1, bei ya chini utakayonunua kwayo ni Sh5,’’ asema, akiongeza kuwa mkulima anaweza kutumia takribani Sh75,000 pesa taslimu kwa miche tu.

Mkulima huyo anasema hujifanyia kazi nyingi shambani, na hivyo, gharama yake ya uzalishaji hupungua.

“Kazi nyingi ziko upande wangu. Hivyo, mtu ambaye anataka kutumia pesa kwa kila kitu anaweza kutumia hadi Sh200,000,’’ afichua Lagat.

Anaongeza, “Gharama ya uzalishaji kwa ekari moja, kwa upande wangu, nikiangalia kwa rekodi ni Sh83,000. Ina kazi nyingi, lakini najaribu kupunguza gharama ya uzalishaji ili nipate faida nzuri.’’

Mkulima huyo, vilevile, huiuza miche ya pilipili mboga kwa wakulima wengine kwa bei ya Sh5 kwa wale ambao huinunua kwa wingi, lakini kwa wale ambao huinunua miche michache, yeye huwauzia kwa bei inayoenda hadi Sh7 kwa kila mche.

Anafichua kwamba wakati anapoipanda miche yake, huzitumia mbolea za kiasili zinazotengenezwa na kampuni fulani jijini Nairobi.

Pia, baada ya mimea yake kuanza kualika maua, yeye huanza kuzitumia mbolea nyingine za kiasili kila mara, ili kuboresha mazao anayoyazalisha.

Kwa wakati huu, mkulima huyo ana pilipili mboga katika shamba ekari mbili; iliyoko katika ekari moja inaendelea kuvunwa, hali ile iliyoko katika shamba jingine haijakomaa.

Anasema kuwa bei ya pilipili mboga kilo moja huuzwa kuanzia Sh30 hadi Sh80, ambapo kilo moja huwa na matunda matano hivi.

Mkulima huyo anasema wakati mimea hiyo inapokomaa, yeye huyachuma matunda ya pilipili mboga kwa muda wa miezi sita, na hupata takribani Sh60,000 kila wiki, na akitoa gharama ya uzalishaji ya Sh5,000, hubaki na faida ya Sh55,000 kwa juma moja, au Sh40,000 kwa wiki isiyokuwa na mazao mengi.

“Pilipili mboga huweza kukupa hadi Sh60,000 kwa wiki, lakini mahindi kwa msimu mzima hayawezi,’’ asema Lagat, akisisitiza kuwa yeye hupata takribani kilo 1,000 za mazao ya pilipili mboga kwa juma moja.

Kwa mujibu wa mkulima huyo, hakuna wakulima wengi ambao hujihusisha na shughuli ya ukuzaji wa pilipili mboga katika eneo hilo na anafichua kuwa gavana wao, Joseph Mandago amekuwa akiwahamasisha wajihusishe na ukuzaji wa mimea kama vile pilipili mboga, badala ya kufikiria tu kuhusu uzalishaji wa mahindi.

Anasema kuwa mkulima anafaa kuyazalisha mazao bora na kwa wingi ili wateja hata kutoka mbali wavutiwe nayo.

Hali kadhalika, anafichua kuwa ana wateja wengi kutoka sehemu nyingi za nchi kama vile Nairobi na kwingineko.

Kwa kuwa changamoto yake kuu ni ukosefu wa maji ya kutegemewa, ananuia kuchimba kisima ili awe na maji ya kutosha kila mara.

You can share this post!

Nguvu mpya za Raila serikalini

USHAURI: Ukitaka kunawiri katika ufugaji; hasa wa kuku,...

adminleo