• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:57 PM
AKILIMALI: Unadra wa mistafeli na faida zake kiafya ulimsukuma kuikuza

AKILIMALI: Unadra wa mistafeli na faida zake kiafya ulimsukuma kuikuza

NA PETER CHANGTOEK

ALIPOKAMILISHA masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo mwaka 2010, alifadhaika na kuhangaika akitafuta ajira. Juhudi zake za kutafuta kuajiriwa hazikufua dafu, ndiposa akaamua kujitosa katika shughuli za kilimo.

Patrick Kimaita, ambaye ni mkulima katika eneo la Mitunguu, Kaunti ya Meru, kwa sasa hushughulika na ukuzaji wa migomba pamoja na mimea mingineyo ya matunda.

Hata hivyo, mkulima huyo mwenye umri wa miaka 34, hupenda mno shughuli ya ukuzaji wa mistafeli (Graviola/soursop plants).

Mmea wa mstafeli ni mmea ambao ni nadra sana kupatikana katika maeneo mengi, licha ya manufaa yake ya kiafya, matunda ya mmea wenyewe yanapoliwa.

Kimaita, ambaye ana shahada katika masuala ya biashara, ametenga sehemu fulani katika shamba la familia yake, ambalo ni ekari mbili, ili kutumia katika ukuzaji wa mimea hiyo.

“Nilianza kushughulika na kilimo takribani miaka kumi iliyopita, baada ya kukosa kupata ajira licha ya kuwa na shahada yangu. Hayo yalikuwa ni kinyume cha matarajio yangu niliyokuwa nayo, tangu nilipokuwa katika shule ya upili, hasa ikizingatiwa kwamba nilipata alama ya B+ ambapo kwa Hisabati nikapata A, na A- kwa Fizikia,” afichua, akiongeza kuwa alikuwa akiyapenda masomo ya Hisabati na Fizikia sana.

Masaibu yake, asema, yalianza alipokosa kupewa nafasi na bodi ya JAB kujiunga na chuo kikuu ili kusomea kozi ya uhandisi, ambayo alikuwa akisubiri kwa hamu na ghamu. Hivyo basi, akashurutika kusomea kozi inayohusiana na biashara. Anasema kuwa alianza kwa kuutumia mtaji wa Sh5,000 kuikuza mimea aina ya Atimoya (ambayo ni haibridi ya mitufaa na mitomoko), mitomoko, mitufaa na mifenesi.

KINGA YA MAGONJWA

“Nilianza kupenda matunda hayo zaidi mnamo mwaka 2014, baada ya kugundua kuwa yana uwezo wa kukinga magonjwa, tulipokutana na mtaalamu wa lishe, wakati marehemu babangu alipokuwa akiugua ugonja wa saratani.

La kushangaza zaidi ni kuwa, mengi ya matunda haya yanadaiwa kuwa na uwezo wa kuzuia kansa,” aeleza mkulima huyo, ambaye ni mzawa wa tatu katika familia ya watoto sita.

“Nilinunua mbegu kutoka kwa Kalro na kutoka kwa wauzaji wa matunda,” adokeza Kimaita, ambaye ni baba wa mtoto mmoja.

Mkulima huo anasema kuwa miche ya mimea ya mistafeli (soursop fruits) huuzwa kwa bei ya Sh200. Anasema kuwa matunda ya mastafeli yana virutubisho muhimu sana.

“Si watu wengi katika eneo hili na kote nchini ambao wanafahamu kuhusu matunda haya. Si kama matunda kama vile machungwa, maparachichi na mengine ya kawaida,” asema mkulima huyo.

Anafichua kuwa, kabla mbegu hazijapandwa, zinafaa kuoshwa na kuachwa zikae kwa muda wa mwezi mmoja hadi miezi sita.

Baada ya kupandwa, majani au nyasi zilizokauka zinafaa zitandazwe karibu na mimea ili unyevu uhifadhiwe kwenye mchanga, hususan wakati ambapo pana jua kali. Zikioza, nyasi na majani hayo hurutubisha mchanga.

Kwa mujibu wa mkulima huyo ni kwamba, baada ya kupandwa, mistafeli huchukua muda wa miaka mitatu hadi mitano ili ianze kuyazaa matunda.

Kuna baadhi ya changamoto ambazo mkulima huyo amewahi kuzipitia katika ukuzaji wa mimea ya mistafeli na mimea mingineyo.

Mojawapo ya changamoto hizo ni mimea yake kuvamiwa na wadudu waharibifu na kuathiriwa na baadhi ya magonjwa kama vile kuoza kwa mizizi. Aidha, ukosefu wa soko la kutegemewa ni changamoto nyingine ambayo mkulima huyo amewahi kupitia.

Katika masoko ya humu nchini, matunda ya mastafeli huuzwa kwa bei kati ya Sh50 na Sh200 kwa kilo. Mkulima huyo huyauza matunda yake katika eneo la City Park, Ngara, Nairobi.

MANUFAA YA MASTAFELI

Matunda ya mastafeli yana manufaa mengi ya kiafya. Yadaiwa kuwa yana uwezo wa kuzuia saratani. Pia, yana uwezo wa kuboresha utendaji kazi wa macho na hivyo kumfanya mtu kuona vyema.

Aidha, mastafeli hupunguza maumivu yanayosababishwa na ugonjwa wa jongo (arthritis) na kuimarisha kinga dhidi ya maradhi mengineyo.

Isitoshe, matunda hayo huimarisha utendaji kazi wa figo na kumfanya mtu kupumua ipasavyo. Pia, matunda ya mastafeli hupunguza msongo wa mawazo.

Mkulima huyo anasema kuwa ananuia kuikuza mimea mingine ambayo ni nadra kupatikana, mathalan; Kiwano, Durian and Mangosteen na mingineyo.

You can share this post!

AKILIMALI: Sh300,000 kila msimu kutokana na mauzo ya...

Mgombea urais wa Zanzibar atiwa mbaroni, Lissu apinga...