Makala

AKILIMALI: Upanzi maua wampigisha hatua licha ya changamoto

May 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES ONGADI

NI robo ekari ya bustani ya maua inayopendeza na kuvutia iliyoko kijiji cha Mtomondoni kilomita moja kutoka mji unaokua kwa kasi wa Mtwapa kaunti ya Kilifi.

Hapa tunamkuta Wilson Kombe, 38, akiwa katika shughuli zake za kusaka riziki ya kupanda maua kila sampuli katika bustani yake.

“Ni kazi ambayo nilianza kupenda tangu utotoni na ni kama mwito ila kwa sasa ni kama kitega uchumi kwangu,” asema Bw Kombe mara alipoanza mahojiano na Akilimali.

Kombe ambaye amekuwa katika biashara hii ya upanzi wa maua kwa kipindi cha miaka mitatu, anasema alianza kwa mtaji wa Sh7,000 na kwa sasa amefaulu katika kupiga hatua maishani.

Ijapokuwa alidinda kufichula kiasi anachotia kibindoni kwa siku ama kwa mwezi, anakiri kwamba ni biashara iliyo na tija.

“Ni biashara ambayo imeniwezesha kupiga hatua kimaisha hasa kwa kuimudu barabara familia yangu na pia kuendeleza shughuli zangu za kila siku,” anasema.

Kuna aina mbalimbali za maua katika bustani ya Bw Kombe miongoni mwazo ikiwa ni Palm trees, Ashok (Indian tree), Shrubs na Croton (iliyo na matawi ya aina mbalimbali ya rangi ya kupendeza) miongoni mwa zengine kibao.

Pia kuna maua asilia kutoka Pwani anayohakikisha amedumisha hasa kwa kuhifadhi mbegu na pia kuzipanda kwa wingi ili zisipotelee mbali kwa vizazi vijavyo.

Hata hivyo, maua yaliyo kwa wingi katika bustani ya Kombe ni aina tofati ya Palm tree ikiwemo Bottle palm, Fishtail palm, Golden palm na Royal palm.

Na je, ni kwa nini Kombe anatilia mkazo sana upanzi wa maua aina ya palm tree katika bustani yake?

“Miti ya palm hufanya vyema sana katika mazingira ya joto hasa kipindi zinapochipuka na wengi wanayapenda kuyatumia kama mapambo katika boma, ofisi au nyakati za sherehe,” anasimulia Kombe.

Kulingana na Kombe, mbegu za palm tree huchukua kipindi cha kati ya mwezi mmoja hadi tatu kuchipuza.

Mara baada ya kuchipuka anayatia katika pakiti maalum ya plastiki ili kuendelea kumea zaidi na baada ya muda fulani anayabailisha katika pakiti ili kumudu mizizi inayokua kwa kasi.

“Wakati mwingine nalazimika kubadilisha pakiti na mchanga mpya baada ya mchanga kukosa nguvu na madini yanayohitajika kwa ukuaji wa maua hayo,” anasema.

Na ili kupata maua yanayopendeza na kumeremeta, mazingira yanahitajika kuwa safi na yenye hewa ya kutosha na kunyunyizia maua maji kila mara.

Bw Wilson Kombe akifurahia maua yenye rangi tofauti yanayopendwa na wateja wake wengi. Picha/ Charles Ongadi

Kwa sasa bustani ya Kombe ina zaidi ya miche 2,000 ya aina mbali mbali ya maua mbali na mengine 2,500 ambayo yako tayari kuuzwa.

Anauza mti mmoja wa Royal palm kwa kati ya Sh150 hadi 200 wakati mti uliokomaa ukienda kwa Sh1,000 kulingana na hali ilivyo ijapo anakiri kwamba mara nyingi bei huwa ni maelewano baina yake na wateja.

Anafichua kwamba wakati wa mvua nyingi biashara hunoga sana kutokana na kwamba maua huwa yamechomoza kiumaridadi na kupendeza kuliko nyakati za kiangazi wakati maua mengi huwa yamesinyaa kutokana na jua kali.

Aidha, kati ya changamoto anazokabiliana nazo ni mavamizi ya ghafla ya magonjwa na wadudu waharibifu kama white flies.

Pia kuna mifugo kama ng’ombe, mbuzi na hata kuku wanaopenya katika bustani yake na kula ama kuchakura maua yake na kuyaharibu.

Hata hivyo, Kombe aliyekosa kujiunga na shule ya upili ya kitaifa ya Alliance mwaka wa 1998 kutokana na ukosefu wa karo anasema biashara ya upanzi wa maua inahitaji uvumilivu na kujitolea.

Ndoto yake kuu ni kwamba siku moja ataweza kununua kipande cha ardhi kutumia kupanda miti hasa ya kiasilia anayohofia huenda ikatoweka katika miaka ya karibuni.