AKILIMALI: Vijana waliohamia Mombasa wakijihami na ujuzi wa kuunda vishikizi vya funguo
HALI mbaya ya kiuchumi inayoshuhudiwa nchini Kenya huwafanya vijana kubuni mbinu za kujipatia riziki.
Hili limebainika kwa Geofrey Kiano, 21, na Nathan Gitonga.
Vijana hawa waliingia mjini Mombasa mapema mwezi Januari mwaka huu kutoka Tharaka Nithi huko Meru, na kuweka makazi katika eneo la Kisimani mtaani Bombolulu ambako walianza kutengeneza vishikizi vya funguo (key holders) na kuchuuza kwa wanaovihitaji.
Geofrey Kiano asema shughuli ya utengenezaji wa bidhaa hizo ni mgumu ila unahitaji uvumilivu na umakinifu mkubwa.
“Tuna kazi kubwa ya kubuni au kutafuta majina ya watu sawa na maana ya majina hayo kabla ya kuanza kazi ya utengenezaji,” anasema Kiano.
Kabla ya kutengeneza vishikizi hivyo, vijana hawa wanatafuta rangi tofauti za kupaka vibao hivyo, nyeusi ikitumiwa kwa kuandikia majina.
“Tunatafuta rangi tofauti na kuzipaka kwenye vibao tunavyochonga, halafu tunaandika majina upande mmoja tukitumia rangi nyeusi, na upande wa pili tunaandika maana ya majina hayo kuwavutia wateja wetu wenye majina sawia,” anasema Geofrey Kiano kwenye mahojiano na Akilimali.
Kadhalika, anasema kila mteja anayehitaji bidhaa hiyo, anachagua yenye jina lake na maandiko yenye maana ya jina hilo.
Kazi ngumu
Kuhusu ukusanyaji wa majina yanayofanyiwa kazi kwenye vibao hivyo, Geofrey anasema ni kazi ngumu kwa wanaotaka kuanza shughuli hiyo, lakini kwao ni kazi inayochukua siku chache.
“Katika kipindi cha siku mbili pekee tunaweza kupata majina yasiyopungua 2,000,” anadokeza kijana huyu huku akiongeza biashara si mbaya kwenye soko.
“Mauzo si mabaya pindi tunapoingia sokoni japokuwa pia si mazuri vile, nasema hivyo kwa kuwa kishikizi kimoja tunauza kwa Sh50 na kwa siku tunauza kati ya vishikizi 20 hadi 35. Kwa mwezi mzima tunaweza kuuza vishikizi 600 hadi 1,050,” anaeleza.
“Ukifanya hesabu ya jumla kwa Sh50 kwa kila kishikizi, utaona tunanufaika kwa pato la kati ya Sh30,000 na Sh52,500 kwa mwezi mzima,” anapasha.
Hata hivyo, Akilimali imebaini kuwa Geofrey na mwenzake Nathan hujiingizia pato kubwa la kati ya Sh360,000 na Sh630,000 kwa mwaka mzima kutegemea idadi ya wateja na msimu wa mauzo ya vishikizi hivyo. Aidha wamedokezea Akilimali huwa hawafanyi biashara mahali pamoja.
Akihojiwa zaidi, Geofrey Kiano anasema walipoingia Mombasa walinuia kujiimarisha na kujiinua kimaisha kwa kutafuta riziki halali kwa jasho lao.
“Tuliingia hapa mwezi Januari mwaka huu na kuendeleza biashara hii ya vishikizi vya funguo, hatukuwa na mawazo tofauti na hayo,” anasema Geofrey.
“Kabla ya kuja hapa tulikuwa Kisumu ambako tuliifanya shughuli hii kujitafutia riziki. Ushirikiano wangu na Nathan umekuwa wa manufaa, hatukosi chochote tunachohitaji, tunajikimu na hatutegemei kazi za kuajiriwa,” anaelezea zaidi huku akiambia Akilimali wametengeneza vishikizi hivyo kwa miaka mitano sasa.