Makala

AKILIMALI: Waliunda chama cha wapanzi wa mihogo kukabili ukosefu wa kazi

March 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na STEPHEN DIK

JE, wajua kuna eneo moja hapa nchini Kenya ambapo huwezi kupata omba omba au mtu mwenda wazimu sokoni?

Wakazi wa eneo la mji wa Tangakona kaunti ya Busia waligundua mapema kwamba ‘Umoja ni Nguvu’ utengano ni udhaifu kisha wakaungana.

Mwaka wa 1999 walianza ukulima wa mihogo na bado wanaendelea kupanda mihogo kwa wingi japo mahindi wanazalisha japo kilimo chao hicho ni cha kiasi kidogo tu.

Hii ni kwa sababu mihogo inafanya vyema kwa mchanga shambani mwao ikilinganishwa na mahindi, yaani wanasema mihogo inatoa mazao mazuri zaidi kuliko mahindi.

Ken Okodoi akitandaza mihogo ndani ya Solar drier ili ikauke vyema katika kiwanda cha Tangakona Cassava Village Processing Project Zone. Picha/ Stephen Dik

Wakazi wanasema walikuwa wamezoea kupanda mihogo kila mmoja kivyake lakini mwaka huo wa 1999 ndio mambo yalibadilika baada ya mashamba kuvamiwa.

Mazao ya mihogo yalikuwa duni sana kwani mimea iliharibiwa na wadudu, ugonjwa wa mimea pia uliingia na kuharibu kabisa, wakazi waliumwa kwa njaa kwa miezi kadha kabla ya kuerevuka.

Baadhi ya magonjwa ya mihogo ambayo yaliharibu mimea ni Cassava mosaic na Cassava Brown strike disease.

Wakazi hawa walikuwa wamezoea kupanda mihogo ya kiasili ambayo huchukua zaidi ya mwaka mmoja kukomaa, mimea hii ya kiasili ni kama vile Pungi, Serere na Magana, walitegemea mvua kukuza mazao shambani.

Wakulima hawakuvuna mwaka huo na kusababisha njaa ya mwaka mzima, hivyo basi waliamua kuungana na kuunda chama cha akiba na mikopo, kitambulikanacho kama Agro-Farmers Self Help Group.

Chama hiki kilinawiri upesi na kuwawezesha kutambulika hadi maeneo ya mbali, wakaanza kutembelewa na mashirika mbalimbali ya kilimo kama vile KARI, ambao baada ya kugundua tatizo lao, wakawafunza mbinu mpya za ukulima wa mihogo na kuwapa mbegu za kisasa.

Aina ya mbegu za kisasa za mihogo walizopewa wakati huo ni MM96/5280 na MH95/0183 mongoni mwa zingine lakini wanasema hizi mbili ndio zamea vizuri eneo hili.

Kuvuna

Wanasema mbegu hizi za kisasa ni nzuri, huchukua miezi kumi kukomaa na kuanza kuvunwa shambani.

Wamekuwa wakibadilisha mbegu hizi baada ya muda, ikizingatiwa kwamba mbegu za kisasa zinachipuka kila uchao.

Wanasema kuwa wanazingatia sana upanzi wa mbegu aina tofauti tofauti baada ya muda kwasababu wakiendelea kupanda mbegu ya aina moja kwa muda mrefu magonjwa yanavamia pamoja na wadudu.

Mwaka wa 2011 wanachama wa Agro-Farmers Self Help Group, ambao ni zaidi ya 500 sasa, walianzisha shirika la kijamii (C.B.O) ambapo walizindua mradi wa kiwanda cha kutengeneza unga wa mihogo na pia kutafuta masoko ya nje kwa zao hili la mihogo.

Timothy Ikwenyi Aringo ambaye ni Mwenyekiti katika usimamizi wa mradi huu, anasema wamepiga hatua kubwa sana, kwa sasa wako na wanachama wengi wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bw Kenneth Ekissa Lokokwang’ayel na mwekahazina Bi Inviolat Tolondo.

Kiwanda hiki cha kipekee walichojenga kando ya barabara kuu ya kuelekea mji wa Nambale kinajulikana kama Tangakona – Cassava Village Processing Project Zone.

Katika kiwanda hiki wakulima wa mihogo huleta mazao yao na kuyabambua maganda.

Wakishabambua maganda kisha wanakata kata vipande vidogo vidogo kwa kutumia mashine maalum inayojulikana kama Chipper machine ambayo ina uwezo wa kukatakata tani 10 za mihogo kwa siku moja.

Baada ya kukatwakatwa halafu hukaushwa juani kwanza kabla ya katandazwa kwa chumba chenye joto jingi kijulikanacho kama Solar Drier.

Hiki chumba cha Solar Drier ndio wanatumia kwa kuweka mihogo ili ikauke vizuri kwa urahisi bila kuchafuka kwa vumbi. Baada ya siku mbili ndani ya chumba hiki cha kukausha mihogo, mingine hukusanywa na kusagwa unga na mingine kupakiwa kwa magunia na kuuzwa.

Unga huuzwa kwa wenyeji wa hapa ambao wanapenda sana ugali wa unga wa mihogo.

Mihogo mingine ambayo imekatwakatwa vipande vidogo vidogo na kukaushwa hupakiwa kwa magunia na kuuzwa kwa kampuni ya Trutrade Africa, ambao ndio wateja wao wakuu.

Kampuni hii hutumia mihogo hii kutengeneza bidhaa zake tofauti tofauti na kisha kuuzia wateja wake. Baadhi ya bidhaa hizo ni kama chakula cha mifugo na unga wa keki na mikate ya mihogo ya kuliwa na wanadamu.

Kiwanda hiki cha Tangakona – Cassava Village Processing Project ndio kiwanda cha pekee cha mihogo katika Kaunti ya Busia na pia kuna wataalamu wanaotoa mafunzo mbali mbali kwa wakulima kama vile wakati wa upanzi na mbinu mpya za ukulima.

Kando pia na kutoa mafunzo kwa wakulima na wanachama wake, wageni hutoka vyuo na taasisi mbali mbali za elimu kutembelea kiwanda hiki ili kuelimishwa kuhusu ukuzaji wa mihogo na pia kufanya utafiti.

Wageni wanapotembelea kiwanda hiki huwa wanatoa ada kulingana na tasisi au vyuo ambavyo wametoka.

Kwa mfano, mashirika ambayo ni ya kimataifa hulipishwa Sh5,000, Shirika lolote kutoka hapa Kenya hulipishwa Sh3,000, Vyuo vyote hulipishwa Sh 2,000, C.B.O hulipishwa Sh1, 500, S.H.G (Self Help Group) hulipishwa Sh1,000, Wakulima ambao hawana kikundi hulipishwa Sh500 kila mmoja kufundishwa.