Makala

AKILIMALI: Wanaume waliunda vitanda vyao, kina dada hawa wakaonyesha ubunifu zaidi

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LUCY MKANYIKA

HUKU serikali ikiendelea kujizatiti kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa wa corona nchini, wanawake wawili mjini Voi wameunda kitanda cha kusaidia kukabiliana na janga hilo.

Wanawake hao; Rosalia Sanguli na Jecinta Chao ambao wamekuwa wakifanya kazi ya kuchomelea vyuma katika karakana yao iliyo eneo la Birikani, viungani mwa Voi, walisema kitanda hicho kitasaidia kushinda vita dhidi ya Covid-19.

Wakiongea na wanahabari, wawili hao walisema walisukumwa kutengeneza kitanda hicho na mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19 uliosababisha uhitaji wa vitanda vya wagonjwa katika hospitali za humu nchini.

Bi Sanguli, alisema rafiki yao mmoja aliwapa changamoto ya kutengeneza kitanda hicho ili kuchukua fursa ya soko iliyoko nchini.

“Tulisaidiwa na marafiki kwa ushauri na vilevile kununua vifaa vinavyohitajika,” akasema.

Kitanda hicho kimeundwa na sensa na kengele ambayo hulia punde tu mtu anapokaribia mgonjwa. Bi Sanguli alisema kengele itasaidia wagonjwa na waliokaribu nao kuweka umbali wa mita moja, unaohitajika kuzingatiwa ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo.

“Sensa ina uwezo wa kuhisi mtu anapokaribia na inaweza kuzimwa wakati hakuna mgonjwa kitandani,” akasema.

Kitanda hicho vilevile kinaweza kutumiwa na wagonjwa mahututi kwani kinaweza kupandishwa juu na chini ili kufikia urefu unaohitajika. Aidha, kimetengenezwa na vyuma kando yake ili kuzuia mgonjwa kuanguka.

Vilevile, kimeundwa na magurudumu ya kuwezesha mgonjwa kusukumwa anapohitaji kuhamishwa ama kupelekwa sehemu nyingine ya matibabu.

Anasema kuwa walitumia vifaa vinavyopatikana humu nchini ili kuunda kitanda hicho ambacho kimevutia watu wengi nchini.

Tangu kuvumbuliwa kwa kitanda hicho siku chache zilizopita, wanawake hao wamepokea simu nyingi kutoka kwa watu na hospitali ambazo zimeonyesha nia ya kuvinunua.

Walisema kuwa ingawa bado hawajapata mnunuzi, wana matumaini ya kuwa watapata biashara ambayo itawawezesha kupanua karakana yao na vilevile kubadilisha maisha yao.

Wawili hao walifungua karakana hiyo mwaka jana baada ya kufuzu na stashahada ya kuchomelea katika chuo kimoja cha ufundi katika Kaunti ya Taita Taveta.

“Tulionelea tufungue karakana yetu ili tusitegemee kuajiriwa. Lakini tangu kuanza kwa janga la corona hatujawa na biashara,” akasema Bi Chao.

Wanawake hao walisifiwa na wenyeji na viongozi wa eneo hilo ambao waliahidi kuhakikisha kuwa watapata soko la vitanda hivyo.

Waziri wa Afya wa kaunti hiyo, Bw John Mwakima alisema serikali hiyo itanunua vitanda hivyo endapo kutahitajika vitanda zaidi.

Alisema kwa sasa kaunti hiyo imefikia idadi ya vitanda 300 vinavyohitajika ila akaahidi kuwa kikosi cha maafisa wa afya kitazuru karakana hiyo ili kukagua aina hiyo ya vitanda.

“Ninasikitika kuwa hatutaweza kununua kwa sasa kwa kuwa tushafanya ununuzi tayari. Lakini tutafanya biashara nao punde tu tutakapohitaji vitanda zaidi,” akasema.

Kwa sasa kaunti hiyo inajenga jumba la matibabu ya Covid-19 katika hospitali ya Mwatate ili kujitayarisha kukabiliana na maambukizi. Jumba hilo linalogharimu Sh15 milioni, linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Agosti.

Julai 2020 serikali ya kitaifa iliahidi kununua vitanda 500 maalum kutoka kwa maseremala wawili kutoka Githunguri na Thika, Kiambu kama njia ya kuwatia moyo kwa ubunifu wao wa kipekee na uchocheaji wa sekta ya viwanda nchini badala ya kutegemea nchi za kigeni.