• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
AKILIMALI: Warsha ya kilimo ilivyofana Eldoret

AKILIMALI: Warsha ya kilimo ilivyofana Eldoret

Na FAUSTINE NGILA

MNAMO Jumamosi Februari 29, wakulima, wanafunzi, wataalamu na maafisa wa kampuni za kuuza vifaa vya shambani, mbegu, fatalaiza na dawa za kuua wadudu walikongamana mjini Eldoret kwa makala ya kwanza mwaka huu ya ‘Seeds of Gold’, ambapo mbinu bora za kilimo zilijadiliwa.

Kauli mbiu ya warsha hiyo ilikuwa ‘Kilimo bora katika enzi za mabadiliko ya tabianchi’, na wakulima walinufaika pakubwa kutokana na ushauri wa wataalamu kutoka kampuni mbalimbali na vyuo vikuu.

Kampuni ya fatalaiza ya Mavuno, Yara, Cosmos, Agroz, Chuo Kikuu cha Egerton, Chuo Kikuu cha Eldoret, Wizara ya Kilimo, Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu, Taasisi ya Mafunzo ya Eldoret na Isuzu Kenya ni baadhi ya mashirika yaliyojitokeza kujibu maswali ya wakulima.

Mengine yalikuwa CMC Motors, Devki, Elgon Kenya, Cooper Brands, Mamlaka ya Maendeleo ya Kerio Valley, New KCC na Bodi ya Maziwa nchini.

Huku nzige wakivamia zaidi ya kaunti 23 nchini, warsha hiyo ilianza kwa onyo kuwa kuendelea kuwarashia nzige dawa kama inavyofanyika sasa, kunatishia maisha ya nyuki ambao ni tegemeo kuu katika uzalishaji wa chakula nchini.

“Kurashia nzige dawa hewani kunachafua mazingira ya nyuki na hatimaye kuwaua. Hivi, taifa hili litapoteza viumbe hawa wanaotambulika kwa ushavushaji wa maua, mchakato ambao ni tegemeo la chakula cha binadamu na wanyama,” akasema Bw Joel Masobo, mtaalamu wa nyuki katika Chuo Kikuu cha Egerton.

Lakini mkulima Rose Chemutai kutoka Ainabkoi aliomba kuelezwa jinsi anavyoweza kulinda shamba lake dhidi ya wadudu hao.

Mtaalamu wa afya ya mimea kutoka Chuo Kikuu cha Egerton Bw John Ng’ang’a alimshauri kutumia dawa za kibayolojia zisizo na kemikali kuua mayai na kupunguza kuenea kwao.

“Nzige husababisha uharibifu wakikusanyika pamoja. Unaweza kutumia dawa za Pheromone (PAN) au green guard, ambazo huua nzige wakiwa wangali wadogo bila kuchafua mazingira. Pheromone hugawanya nzige wengi hali inayochangia kupunguza kiwango cha uharibifu shambani,” akaeleza.

Mbinu hii imetumiwa pakubwa katika mataifa ya Brazil, Afrika Kusini na Australia kwa mafanikio makuu.

Mbinu inayotumiwa na China ya kutuma bata kuwala nzige pia ilitajwa kama mojawapo ya mbinu bora zaidi katika kudhibiti kuenea kwa wadudu hao.

Mkulima George Maina kutoka eneo la Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu alitaka kujua ni kwa nini kila anapopanda mikarara, majani yake hupata rangi ya manjano kisha kunyauka.

“Ni mambo mengi yanaweza kusababisha hali hiyo. Mojawapo ni kutumia fatalaiza ya upanzi na ile ya kupalilia kwa pamoja. Haifai kabisa. Kunyauka husababishwa na ukosefu wa maji.

“La tatu ni kwamba huenda mchanga wa eneo la Kesses umekosa baadhi ya madini muhimu yanayohitajika na mkarakara. Nakuomba uchukue sampuli ya mchanga huo upimwe,” akajibu Bi Carol Mutua, mtaalamu katika Chuo Kikuu cha Egerton.

Palizuka kicheko wakati Collins Kibet alipouliza iwapo kuwapa ng’ombe mahindi yaliyooza kutokana na uhaba wa lishe kunaweza kuchangia mwa maradhi ya mnyama huyo.

Dkt James Ondieki wa Chuo Kikuu cha Egerton alimuonya dhidi ya kuwapa mifugo chakula ambacho yeye mwenyewe hawezi kukila.

“Aina hiyo ya chakula husababisha sumu ya aflatoxin, ambayo huleta gonjwa la kansa na haiwezi kutolewa kwa kuchemsha wala kuchoma. Hivyo, unafaa kuzika mahindi yaliyooza mchangani.

“Tumia mahindi safi wakati unatengeneza lishe yako. Epuka kununua lishe madukani kwani baadhi ya wafanyabiashara wanaweza kukuuzia lishe yenye aflatoxin.

“Lishe kutokana na mahindi itakupunguzia gharama kwa hadi mara tatu ikilinganishwa na kununua nyasi iliyokauka. Pia, ng’ombe wako watatoa maziwa mengi zaidi,” akashauri.

Mbali na ushauri kuhusu kilimo cha mimea na ufugaji, wakulima walipata fursa ya kujionea baadhi ya teknolojia za kisasa.

Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Egerton kimeibuka na ubunifu wa kufuga nyuki, ambapo ‘malkia’ hutunzwa kutaga mayai na ifikapo siku ya nane, mayai hayo huangua nyuki.

Kwa kutumia bomba la mbao nyepesi, chuo hicho kimeunda aina mpya ya mzinga ambao unasitiri nyuki wapatao elfu tatu. Hatua hii husaidia kuongeza kiwango cha asali inayorinwa na mfugaji.

Mamlaka ya Maendeleo ya Kerio Valley (KVDA) nayo ilionyesha aina mpya ya nyasi ambayo inaweza kustahimili ukame na inayochangia kwa ng’ombe kutoa maziwa mengi.

“Nyasi hii inaweza kukomaa mapema katika maeneo kame. Ni nzuri ya kutengeneza lishe ya mifugo na inaweza kukuzwa kwa ajili ya kuuza, akasema Bw David Biwott, ambaye ni meneja wa idara ya kilimobiashara katika shirika hilo.

  • Tags

You can share this post!

Nambari ya Serikali ya kuripoti coronavirus yageuka...

UFUGAJI: Ufugaji vipepeo ulivyowawezesha wanawake kutunza...

adminleo