AKILIMALI: Waungama, maembe yana pato la uhakika
Na RICHARD MAOSI
UPANZI wa miembe kwa ajili ya uzalishaji maembe ni utajiri mkubwa kwa wakulima mashinani, hususan wajasiriamali waliojitosa katika kilimobiashara, wakiwa na lengo la kujipatia riziki kwa kujiongezea kipato.
Utayarishaji wa shamba la kukuza maembe unastahili kuanza mapema, na miche ifanyiwe utafiti wa kutosha kabla ya kuhamishwa shambani kwa ajili ya upanzi wa matunda haya yenye soko pana ulimwenguni.
Takriban mikoa yote nchini Kenya inakuza maembe, lakini kaunti ya Makueni inaongoza katika ukuzaji wa maembe almaarufu kama Apple mangoes.
‘Akilimali’ ilizuru eneo la Tawa, Kaunti ya Makueni na kupatana na Teresia Wambua kutoka eneo la Kiteta ambaye alianza mradi wa kukuza maembe mnamo 2004.
Kilomita moja hivi kutoka Tawa Market nilimkuta Teresia akiendelea kuvuna baadhi ya maembe yake ambayo yalikuwa yamekomaa yakisubiri kuhifadhiwa, ambayo anasema pia wakati mwingine yamekuwa yakimsaidia kulisha mifugo ili kuongeza uzito wa maziwa.
Kwa ushirikiano na mumewe Francis Wambua walipanda miche ya maembe katika kipande cha ardhi cha ekari moja, wakiamini kuwa hii ni kama ajira nyingineyo ile muradi mkulima ajivunie jasho lake.
Teresia anasema hii ni miche ambayo ililetwa kutoka Malindi na ikaishia kufanya vyema katika kaunti ya Makueni kushinda eneo la Pwani, ambapo inaaminika kuwa ndio asili ya maembe dodo.
Teresia anasema miche ya kukuza maembe huchukua miaka mitatu tu kukomaa, kabla ya mkulima aanze kupata mavuno yake ya kwanza.
Kwa kuwa maembe mengi kutoka kaunti ya Makueni ni makubwa kiasi cha haja, wakulima wengi kutoa eneo la Makueni huvuna mazao yao mara moja kwa mwaka.
“Wakazi wengi hapa wanategemea zao la maembe kulipia watoto wao karo, kwani ni mmea unaofanya vyema ikilinganishwa na aina nyingine ya mazao kama vile dengu, viazi na mahindi,” akaongezea.
Akiwa mkulima mtajika anasema kuwa msimu wa kuvuna maembe mara nyingi katika mkoa wa Mashariki ni baina ya Januari na Februari.
Ambapo Machi ni mwezi wa kukagua miti ya kukuza maembe hatimaye kati ya October na November ndio wakati ambao maua huanza kuchomoza kutoka kweneye mashina ya miti ya maembe.
Alifichulia ‘Akilimali’ kuwa katika kipande chake cha ardhi cha ekari moja anamiliki zaidi ya mashina 300 ya maembe ambapo kila moja linaweza kuzaa maembe kati ya matunda 200-300.
Wanunuzi wake wengi wakiwa ni wafanyabiashara wenye mitaji midogo, na wenye uwezo mkubwa na viwanda kutoka soko la Tawa, Nairobi , Kawangware, mpaka Busia.
Mara nyingi matunda yake hutumika kutengeneza juisi ya maembe miongoni mwa bidhaa nyinginezo kutokana na zao hili, kama vile mchanganyiko wa matunda.
Ingawa wadudu na maradhi ni kero wakati mwingine, inampasa kuchukua tahadhari kwa kutoa ratiba maalum wakati wa kupanda, kupalilia na kuvuna.
Teresia na Francis kwa pamoja wanasema wanapenda kutumia mbolea inayotokana na samadi ili kutoa nafasi ya miche kunawiri na kupatia majani afya.
Pili, wanasema hulazimika kurushia mimea yake dawa kukinga miche yao dhidi ya baridi ambayo mara nyingi hutokea baina ya mwezi wa Novemba na Desemba.
Anasema kuwa zao la Apple mango kinyume na aina nyingine ya matunda kama vile machungwa hayahitaji maji mengi, hivyo basi yanaweza kufanya vyema katika maeneo yenye mazingira magumu yasiyokuwa na mvua ya kutosha.
Aliongezea kuwa miale ya jua inahitajika, wakati wa kupatia mazao ya maembe ladha tamu ya kupendeza ambayo hubainisha tofauti ya maembe yanayokuzwa kutoka kaunti ya Makueni ukilinganishwa na maembe kutoka kwingineko.
Teresia alitupatia utaratibu wa kukuza miche ambapo alisema kuwa wakati wa kupanda mkulima atahitaji kuchanganya mchanga na mbolea katika hatua ya kwanza.
“Mimea inapokua na kufikia futi mbili mimi hupandikiza (graft) na tufaha (apple) au tunda la aina yoyote ambalo mkulima atapenda,” akasema.
Hali ya kupandikiza anasema kuwa ni sharti iwiane na hali ya anga ya eneo maalum ikizingatiwa kuwa Mashariki mwa Kenya ni mojawapo ya maeneo nchini ambayo hupokea kiwango kidogo cha mvua hivyo basi kiwango cha maji huwa ni haba.
Tatu aliongezea kuwa yeye hupalilia shamba lake angalau mara moja kila mwezi ili kuondoa magugu ambayo yanaweza kufanya mimea kunyauka wakati wa kushindania virutubishi muhimu, kama vile maji na madini kutoka mchangani.
Kwa upande mwingine Francis anaona kuwa itakuwa jambo la kimsingi endapo serikali ya ugatuzi itawekeza pakubwa katika viwanda vya kutengeneza juisi inayotokana na maembe, ili kuwafaidi wakulima wadogo wasiokuwa na soko la kupeleka bidhaa zao.
Ili wakulima wengi wanaokuza maembe wapate soko la uhakika wakati wa kusafirisha maembe yao kwa wanunuzi wanaopatikana mbali na kaunti ya Makueni.
“Wawasaidie wakulima kupata dawa za kukinga matunda yao dhidi ya wadudu wanaoweza kuharibu maembe yao kabla ya kufikishwa sokoni,” akasema.