Makala

AKILIMALI: Yeye ni miongoni mwa wakulima bingwa wa Mishiri eneo la Mlima Kenya

August 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DUNCAN MWERE

MIAKA nenda miaka rudi, eneobunge la Kieni limekuwa likipokea msaada wa vyakula na kuhesabiwa kama mojwapo ya maeneo kame nchini.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni, eneo hili lililo katika Kaunti ya Nyeri limechukua mkondo mpya ambao umeliwezesha kujitosheleza kwa chakula.

Hii ni baada ya wenyeji wa eneo hili kung’amua kuwa kuna rotuba ya kutosha na kumaliza itikadi ya kuwa sehemu yenyewe ni kame.

Aidha, wakulima wa hapa wameanza kukumbatia mbinu za kisasa za ukulima na kuchochea wakazi wa maeneo mengine kununua mashamba hapa.

Katika kitongoji cha Honi, mji wa Chaka, utapatana na mkulima stadi wa zao la mishiri au French beans.

Amekuwa akitia fulusi lukuki mfukoni mwaka baada ya mwingine kutokana na kuutunza mmea huu katika kipande chake cha ardhi.

Tulipozuru shamba lake, tulikutana na wakulima wakivuna zao la mishiri na hapa ndipo Maina Muriuki alimfichulia mwandishi wa makala haya hatua zote za kuukuza na hatimaye kufanikiwa.

Mishiri ni mmea unaochukua muda mfupi kukua japo unahitaji kutunzwa kila wakati,” aeleza Maina.

Mkulima huyu anaweza kuvuna mazao yake kati ya siku 45-60 kutegemea na mbegu alizotumia, hali ya anga na namna alivyoutunza tangu upandwe na kuvunwa.

Baadaye mkulima atakuwa akivuna angaa mara mbili kwa wiki.

Maina anatoa tahadhari kwa wakulima wanaopania kujitosa katika zaraa hii kuwa makini hasa wakati wa kuvuna.

“Wakati wa kuvuna mkulima anastahili kuwa makinifu kwani kampuni zinazonunua hususia zao hili na hatimaye kutupwa kutokana na kucheleweshwa wakati wa kuvuna na kutopanga inavyohitajika,” afichua.

Pili mazao yake yanafaa kuuzwa kwa wakati kutokana na kuwa yanaweza kuoza kwa haraka. Awali kabla ya kupata tajriba kuhusu mmea huu alipoteza mazao yake kwa wingi lakini sasa mambo ni shwari baada ya kupata kampuni ya kuwauzia.

Kampuni ya Instaveg kutoka Kaunti ya Kirinyaga imekuwa ikinunua bidhaa hii kwa muda sasa. Kwa mujibu wa wataalamu wa kilimo nyanjani, mmea huu ni muhimu kwa siha ya binadamu.

Aghalabu wanahoji kuwa matabibu wamekuwa wakiwarai hata wagonjwa kutumia mishiri kutokana na kuwa na madini ya fosiforasi sawa na vitamini A, B na D.

Maina ambaye pia ni mkulima ngangari wa mboga na nyanya, hakosi kutia kibindoni Sh750,000 kwa msimu baada ya kudondoa matumizi yake katika kilimo cha mishiri pekee.

Ni kutokana na hili ambapo wengi wanasadiki yeye ni mmoja wa wakulima wanaongoza katika upanzi wa mishiri eneo la Mlima Kenya.

Maji yahitajika

Mojawapo wa hitaji kuu ni maji. Kwa mujibu wa mkulima huyu, mmea huu hufanya vyema hasa msimu wa mvua kwani huhitaji unyevunyevu kila wakati.

Anahimiza wakulima kujihami na vifaa vya kuhifadhi maji endapo mvua itapungua. Majira ya kiangazi mkulima hana budi ila kunyunyizia maji kila wakati. Yeye hupata maji kutoka Mto Honi ulio karibu na shamba lake.

Hii haimaanishi kuwa zao la mishiri halihitaji joto.

Mishiri hufanya vizuri katika maeneo yaliyo na joto la wastani nchini. Maeneo haya ni pamoja na Murang’a, Kirinyaga, Nyandarua, Embu na Kiambu.

Maeneo kadhaa ya Bonde la Ufa mathalani Naivasha yamekuwa yakikuza mishiri kwa wingi kwa matumizi ya hapa nchini na ng’ambo.

Pili kiungo kingine ni dawa, lazima mkulima ajue ni wakati upi na dawa aina gani inayofaa kurashiwa.

Baada ya wiki mbili mkulima anafaa kupulizia dawa ya kuangamiza mdudu aina ya Beanfly ambaye Maina anakiri ni kikwazo kikuu kwa mavuno. Fatalaiza kwa upande mwingine hutumika kwa wingi katika viwango tofauti.