• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Al-Shabaab warudisha kilimo cha zingifuri kuwa ‘sufuri’

Al-Shabaab warudisha kilimo cha zingifuri kuwa ‘sufuri’

NA KALUME KAZUNGU

KILIMO cha zingifuri, yaani bixa kinakabiliwa na pandashuka tele, mojawapo ikiwa ni changamoto ya mashambulio ya mara kwa mara yanayotekelezwa na Al-Shabaab katika Kaunti ya Lamu.

Maeneo mengi yapatikanayo tarafa za Mpeketoni, Hindi, na Witu katika kaunti hiyo yamekuwa yakisifika kwa kuendeleza kilimo cha zingifuri tangu mmea huo ulipozinduliwa kwa mara ya kwanza Pwani ya Kenya miaka ya sabini (1970s).

Zingifuri ni tunda linaloshabihiana na nyanya ndogo lenye rangi ya manjano mbivu ambalo pia huliwa.

Mmea au zao la zingifuri huletea wakulima pesa kwani huuzwa na kutumiwa kama kiungo kwenye rangi ya mapambo, dawa na bidhaa za vyakula.

Mmea huo hustahimili hali ngumu ya anga, ikiwemo ukame, athari za wadudu na magonjwa.

Vijiji vinavyokabiliwa na changamoto ya ugaidi, hasa Al-Shabaab, ambavyo pia vinasifika kwa kukuza zingifuri ni Juhudi, Salama, Widho, Marafa, Mashogoni na viunga vyake.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa wengi wa wakulima wa Lamu ambao wamekuwa wakijitahidi kukuza zingifuri kwa sasa wamekata tamaa kutokana na changamoto zilizokithiri na ambazo zinahatarisha au kusambaratisha kabisa sekta hiyo.

Wakulima waliohojiwa na Taifa Leo walitaja ukosefu wa soko la zao hilo kuwa kizingiti kikuu kinacholemaza juhudi za kupanuliwa kwa kilimo hicho.

Bw Samuel Mwangi, mkazi wa Hongwe, alisema inavunja moyo mkulima anapojikaza kukuza zingifuri na kisha baadaye inasalia shambani bila mnunuzi.

“Soko limekuwa kizingiti kwetu sisi wakulima wa zingifuri. Tunajikaza kuendeleza kilimo hicho lakini hatuoni faida. Tunauza zingifuri rejareja kwa matumizi ya papa hapa nyumbani. Tutafurahi endapo serikali itatukumbuka na kututafutia soko sisi wakulima wa zingifuri. Mmea huo unafanya vyema eneo hili,” akasema Bw Mwangi.

Bi Mary Karanja, mkazi wa kijiji cha Salama, anasema mbali na ukosefu wa soko, utovu wa kila mara wa usalama maeneo yao unaochangiwa na Al-Shabaab pia ni kikwazo katika kuendelezwa kwa kilimo cha zingifuri.

Mashamba mengi ya zingifuri kwenye vijiji vya Salama, Juhudi na viunga vyake yameachwa yakimea magugu pamoja na zao hilo kutokana na wakulima kuogopa kuingia mashambani kupalilia mmea huo kwa kuhofia usalama wao.

“Licha ya serikali kujitahidi kuboresha usalama eneo hili, imani bado haijarejea kikamilifu kiasi cha mkulima kuingia shambani kupalilia au kuvuna zingifuri,” akasema Bi Karanja.

Naye Bw Samson Kamau, alisema wengi wao waliokuwa awali wakikuza zingifuri mashambani mwao wameishia kuikata na kupanda mimea mbadala ya kuwaletea mapato.

Alisema miundopmsingi duni iliyopo kwenye kilimo cha zingifuri ni sababu tosha ya wakulima wengi kubadilisha kilimo hicho.

Bw Kamau alihoji kwa nini kuendelea kukuza mimea isiyokuwa na faida mashambani.

Anasema walivumilia kupanda na kuendeleza kilimo cha zingifuri kwa muda mrefu.

“Mwishowe tulishindwa. Soko hakuna. Serikali yenyewe haitutambui na kutuhamasisha kuhusiana na kilimo cha zingifuri. Ndiyo sababu tukaamua kuacha kilimo cha zingifuri na kuingilia ukulima wa matikitimaji, mahindi, pojo, maharagwe, maembe na mimea mingine, ilmradi tupate mtaji wa kusongesha haya maisha,” akasema Bw Kamau.

Bi Lucy Katama naye alitaja changamoto ya wafanyabiashara walaghai kuwa miongoni mwa mambo yanayosambaratisha kilimo cha zingifuri.

“Kuna wafanyabiashara potovu ambao kwa miaka mingi wamejidai kuwa madalali wa kununua zingifuri kutoka kwetu kwa bei ya okota, ambapo wao ndio wanafaidi ilhali mkulima akiendelea kuumia. Ni vyema serikali ifikirie kuanzisha kiwanda cha bixa hapa Lamu ili kutatua hili zogo la madalali kwani mkulima atakuwa akipata soko tayari la zingifuri papa hapa nyumbani,” akasema Bi Katama.

Tunda la zingifuri linapovunwa huwezesha kupata mbegu zake ambazo pia hutumiwa kutayarisha rangi ya vyakula, kuandaa kachumbari.

Mbegu za zingifuri zinapopondwapondwa pia hutumika kuchanganya na kutayarisha mbolea.

Mbali na faida nyingi za kawaida zinazolinganishwa na zingifuri, mmea huo pia ni kipenzi cha wanamuziki ambao hutumia kama kikolezo au kiungo cha kuungia mashairi yao ya kukoleza utamu wa muziki.

Kwa mfano, msanii maarufu wa Bongo Flava kutoka Tanzania, Diamond Platnumz, alitumia mmea wa zingifuri kwenye mistari ya baadhi ya nyimbo zake.

  • Tags

You can share this post!

Chaguo la mambo matatu la Rais laleta afueni sekta ya miwa...

Waislamu wahimizwa kuhifadhi Qur’an kupalilia tabia njema

T L