Aliponea ajali 2 barabarani, akauawa na ndege Malindi
KATIKA mwaka wa 2017, Bi Naomi Chitsaka, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Mashamba iliyoko Malindi, Kaunti ya Kilifi, alihusika katika ajali ya barabarani iliyomlazimu kukatwa mguu.
Ingawa aliponea kifo katika ajali hiyo, Bi Chitsaka wiki iliyopita alikuwa kati ya watu watatu waliopoteza maisha yao wakati ndege ilipoanguka barabarani katika eneo la Kwachocha, barabara ya Malindi-Mombasa.
Isitoshe, Naibu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi Mwaka Rubea, alifichua kuwa, marehemu alikuwa akielekea kujiandaa kwa mahojiano ya kupandishwa cheo wakati ajali ilipotokea Ijumaa.
“Alikuwa jasiri. Alipoteza mguu wake kwenye ajali ya barabarani mwaka wa 2017. Inasikitisha sana jinsi alivyofariki kifo cha uchungu,” akasema Bi Rubea.
Wakati ndege hiyo ilipopata hitilafu na kuanguka, Bi Chitsaka alikuwa kwenye pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Felix Hamisi, ambaye pia alifariki.
Ilibainika propela ya ndege ilimkata kichwa mwalimu huyo mkuu kutoka shingoni.
Mhudumu mwingine wa bodaboda, Vincent Kasena Ruwa, pia alifariki.
Bw Stephen Mwagona, 26, mwanawe Chitsaka, alifichua kuwa, wiki iliyopita, walihusika katika ajali nyingine tena na mamake.
Alieleza kuwa, mnamo Januari 7, alikuwa akimwendesha mamake kwenye pikipiki kuelekea kazini asubuhi wakati ilipoteleza barabarani wakaanguka na kupata majeraha madogo.
“Ajali ya mamangu itatuuma milele. Tunataka haki,” akasema.
Hitilafu za kimitambo
Ndege hiyo ndogo aina ya Cessna 172 ilikuwa imeondoka katika Uwanja wa Ndege wa Malindi mwendo wa saa nane na dakika 50 mchana.
Ilikuwa imeratibiwa kuelekea Nairobi ikiwa na rubani, mkufunzi wa uendeshaji ndege, na mwanafunzi wa uendeshaji ndege.
Wote watatu walipata majeraha na kutibiwa baada ya ajali hiyo inayoaminika ilitokana na hitilafu ya injini.
Bi Chitsaka alikuwa ni mteja wa mara kwa mara wa marehemu Felix, mwendeshaji bodaboda.
Felix ameacha mke na watoto wawili wenye umri wa miaka saba na mwaka mmoja.
“Nilimwona mara ya mwisho Ijumaa hiyo mwendo wa saa nane mchana kabla aondoke kuenda kumchukua mteja wake, marehemu Bi Naomi,” mkewe, Bi Loice Reuben, akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Rubani wa ndege alisema hawakuwa na namna nyingine walipogundua ndege ilikuwa na hitilafu ila kutafuta mahali wazi karibu pa kutua.
Bw Kahindi Kenga, mjomba wa marehemu Vincent, alieleza kwamba waliona ndege ikiwa angani bila sauti ya injini na ghafla ikaanza kuanguka.
“Ilijaribu kutua barabarani lakini ilipoepuka kugongana na lori lililokuwa likitokea upande wa pili, ilipoteza mwelekeo na kuanguka katika eneo la Kwachocha. Waliokuwa ndani ya ndege walifanikiwa kutoka kabla ilipuke na walijaribu kumwokoa Ruwa lakini hawakufaulu,” akasema Bw Kenga.