Alipwa Sh64.9 milioni baada ya polisi kuua mbwa wake
MMILIKI wa mbwa katika mji mmoja jimbo la Missouri atalipwa Sh64 milioni baada ya afisa wa polisi kupiga risasi na kumuua mbwa huyo aliyekuwa kipofu na kiziwi na mwenye uzito wa kilo 5.89.
Ni tukio lililosababisha kujiuzulu kwa meya wa mji huo na wito wa kulivunja shirika la polisi la eneo hilo.
Maafisa wa Sturgeon, Missouri, na mmoja wa maafisa wa polisi wa mji hio walikubali malipo hayo kwa Nicholas Hunter, ambaye alikuwa mmiliki wa Teddy. Hunter alimiliki mbwa huyo wa miaka mitano wa aina ya Shih Tzu tangu akiwa na wiki 12.
Hunter alishtaki mji huo hapo Mei 2024 baada ya Afisa wa Polisi Myron Woodson kufyatulia Teddy risasi mara mbili kutoka mita chache wakati alipoitikia wito wa jirani aliyeripoti kuwepo kwa mbwa aliyepotea.
Mawakili wa Hunter kutoka kampuni ya Crinnian walisema katika taarifa ya kutangaza makubaliano ya suluhu kwamba wanatumai idara nyingine za polisi “zitajifunza kutokana na hili na kutoa mafunzo bora kwa maafisa wao siku zijazo ili matukio kama haya yasijirudie.”
“Bwana Hunter amepata nafuu kwamba suala hili limekamilika, lakini hakuna chochote kitakachoweza kumrudisha Teddy wake,” mawakili waliongeza katika taarifa iliyosambazwa na Shirika la Kulinda Wanyama lililounga mkono kesi ya Hunter. “Teddy alikuwa mbwa mwema na hakustahili haya.”
Ofisi ya meya wa Sturgeon haikujibu ombi la maoni. Woodson, ambaye tayari ameondoka kwenye idara hiyo, hakuweza kupatikana kwa maoni.
Kuuawa kwa Teddy kuliwashtua na kuwakasirisha wakazi wa Sturgeon, mji wenye watu takribani 1,150 ulio maili 20 kaskazini mwa Columbia, ambapo majukumu ya kudhibiti wanyama yalikuwa yakisimamiwa na polisi wa eneo hilo. Wito ulitolewa kuvunja idara ya polisi yenye maafisa wawili pekee baada ya tukio hilo.
Teddy alitoroka kwenye kibanda chake chenye uzio wakati Hunter alipokuwa ametoka kwenda kula chakula cha jioni na akaingia uani mwa jirani. Jirani huyo aliwafahamisha polisi akitumaini kumrejesha Teddy kwa mmiliki wake.
Woodson alifika na akajaribu bila mafanikio kumkamata Teddy kwa kutumia “kitanzi cha kumteka mnyama” kwa takriban dakika tano kabla ya kutoa bastola yake na kumfyatulia risasi mara mbili mbwa huyo mdogo aliyekuwa amegeukia upande mwingine, kulingana na kesi ya Hunter na video ya kamera ya mwilini.
Mji huo uliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba afisa huyo alimfyatulia mbwa huyo risasi kwa kuhofia kwamba alikuwa na kichaa cha mbwa. Ujumbe mwingine baadaye uliongeza kuwa maafisa walitazama video ya kamera ya mwilini na wakaona kitendo cha afisa huyo kilikuwa sahihi.
Meya wa Sturgeon wakati huo, Kevin Abrahamson, alitetea awali kitendo hicho kabla ya kujiuzulu ghafla. Meya mpya alimsimamisha Woodson ambaye ripoti zinasema hatimaye aliacha kazi.
“Mji haukushughulikia suala hili vizuri,” Seth Truesdell aliyejaza nafasi ya Abrahamson kama meya, aliiambia runinga ya KMIZ. Truesdell alisema mji “ulimiminikiwa na zaidi ya simu 700 kwa siku kutoka kote duniani” baada ya tukio hilo.
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Kulinda Wanyama, Chris Green, alisema mbwa wa kufugwa wanauliwa na polisi mara nyingi zaidi kuliko watu wanavyofahamu. Aliongeza kuwa ilikuwa wazi kutokana na video ya kamera ya mwilini kuwa Teddy “hakuwa tishio.”
“Yeyote anayetazama video ya Teddy anaona kuwa ni mbwa mdogo sana, wala hakusogea kuelekea kwa afisa,” Green akasema.
Kundi hilo linatumai kwamba makubaliano hayo ya malipo yatasukuma Missouri kupitisha sheria itakayowataka maafisa wa polisi kupewa mafunzo ya kushughulikia wanyama wa watu wanapokutana nao. Kukosa mafunzo hayo kunaweka watu na wanyama hatarini, Green akasema.
“Na pia kinawagharimu fedha nyingi ambazo si lazima,” aliongeza.
Imetafsiriwa na Geoffrey Anene