Alivyogeuza eneo kame kuwa Canaan ya Kenya
ELIJAH Oenga aliporithi shamba la babake eneo kame, hakujua tija ambazo zingejiri siku za usoni.
Hii leo, mwasisi huyu wa Ubuntu Kreative Village, jukwaa la mapumziko eneo kame, anajivunia kutokana na ubunifu na uvumilivu wake.
Awali, alikuwa na tashwishi kuhusu uwekezaji wa shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 18 lililonunuliwa 1998 akiwa angali shuleni.
“Sikudhania kuna lolote la thamani lingetokana na ardhi iliyo eneo kame (ASAL),” anasema.
Kuuza urithi, haikuwa jawabu lake na badala yake akaanza kugeuza tashwishi yake kuwa maono.
Shamba hilo sasa ni Canaan ya Kenya.
Akiwa aliiasisi 2017 eneo la Oloosirkon, Tuala, Kaunti ya Kajiado, baada ya kuacha kazi ya kuajiriwa, Ubuntu Kreative Village ni makao ya mseto wa biashara.
Inasitiri shughuli za kilimo, eneo la mapumziko wakati wa likizo, nyumba za kukodi za muda hasa kwa wanafamilia na wapendanao, vituo vya kunyoosha viungo vya mwili, na bustani ya hafla.
Shamba hilo, vilevile lina eneo maalum la wanamuziki kutungia nyumba, sanaa (uchoraji) na kidimbwi cha kuogelea.
“Hayo yote yanatokana na mapenzi yangu kwa mazingira,” Oenga asema.
Alisomea katika Chuo Kikuu cha Baraton, na anasema mazingira yake ya kuridhisha na kutuliza moyo ni kichocheo cha anachoendeleza Kajiado.
Anadokeza, “Chuo hicho kina mazingira maridadi, hivyo basi yakanipa motisha kugeuza shamba nililorithi liwiane nayo”.
Kabla kuafikia malengo yake, Oenga alikuwa Meneja wa Kitengo cha Ununuzi (Procurement) na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kabarak kuanzia 2013, baada ya kurejea nchini kutoka Uingereza (UK).
“Nilisafiri UK kusomea Shahada ya Uzamili, na kwa bahati nzuri nikapata fursa ya kufanya kazi humo,” anafichua mfanyabiashara huyo ambaye 2022 aliwania kiti cha ubunge Dagoretti Kaskazini.
“Mazingira ya Chuo cha Baraton yanafanana na baadhi ya maeneo kadha Uingereza hususan Scotland ambayo inavutia ajabu, na utangamano huo ukachochea zaidi mapenzi yake ya kijani”.
Kwa jumla ya ekari 18 alizorithi, ametumia ekari tano pekee kwa minajili ya biashara anazofanya.
Shamba hilo liko eneo la Rangau, Ongata Rongai, ‘Rangau’ likiwa ni jina la jamii ya Kimaasai lenye maana ya miti midogo yenye miiba.
“Rangau ndio mmea mbadala wa ‘water hyacinth’ huku. Kipande hiki kilisheheni vumbi nilipokitwaa na nyasi za Savannah,” akasema wakati wa mahojiano na Akilimali shambani mwake, akikumbuka taswira iliyokuwepo.
Mwaka 2017, alianza kufufua hadhi ya eneo hilo kwa kupanda miti misimu ya mvua.
Oenga, ambaye anaamini Falsafa ya mambo makubwa hutokana na yale madogo, akiifananisha na jinsi mchwa huunda kilima chake, aligeuza shamba hilo polepole.
Mnamo 2018, aliwekeza kima cha Sh300, 000 kwenye kilimo cha mvungulio (greenhouse) kukuza basil.
Jitihada hizo zimezaa matunda sasa akimiliki jumla ya vivungulio 14 kukuza zao hilo analouza nje ya nchi.
Isitoshe, hulima vitunguu, na ana kiunga cha kila aina ya miti ya matunda, na pia anafuga kuku, bata, sungura na mbuzi aina ya gala.
Akiwa mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira ya Muungano wa wakazi wa Oloosirkon, Oenga ni balozi wa utunzaji mazingira akihimiza wenyeji na shule kupanda miti.
Anaamini Bara la Afrika linaweza kujilisha na kukabiliana na athari hasi za tabianchi, kupitia utunzaji mazingira kwa kukuza miti kwa wingi.
Ubuntu Eco Farm, iko karibu kilomita nane kutoka mji wa Ongata Rongai, na unapozuru mradi huo, langoni utakaribishwa na maua maridadi kwenye njia za kuingia.
Kituo cha Ubuntu Music and Art Gallery, kilichoko karibu na lango, huonyesha michoro yenye asili ya Kiafrika, nayo makao ya kulala yakiwa karibu na dimbwi la kuogelea, na pia yamezungukwa na kiunga cha matunda.
Ukiwa na muundo wa mada ya Kiafrika, uga wa hafla unatumika kwa minajili ya harusi, muziki, uigizaji na pia mashindano ya mapishi.
Vituo vya kunyoosha viungo, kutuliza mwili na mawazo ni pamoja na Aroha Mai SPA yenye sauna, Jacuzzi, na maeneo ya kuoga.
“Aghalabu, watu wakiwa kazini na shughuli zao za kila siku huzongwa na mengi na Ubuntu Kreative Village ndio tulizo,” Oenga anasifia, akiongeza kwamba huduma zake zimevutia hata wageni kutoka nje ya Kenya.
Kukodi nyumba za kulala, kwa siku inagharimu kati ya Sh8, 000 hadi Sh25, 000 kulingana na idadi ya vyumba.
Basil, likiwa ni zao linaloteka soko ng’ambo kilo moja huuza Sh400, navyo vitunguu akiuza humu nchini bei yake ikiwa kati ya Sh70 hadi Sh100 kwa kilo.
Akipepesa macho yake nyuma miaka saba iliyopita, uwekezaji aliofanya anautaja kama mojawapo ya biashara inayomtuza.
“Kufufua eneo kame na kuipa jamii matumaini, ni ufanisi mkubwa. Nilipokuja hapa, ilikuwa nadra kuona ndege ila sasa tunakadiria eneo hili hutembelewa na zaidi ya spishi 20 za nyuni,” anaelezea.
Kuboresha mradi huo, hata hivyo, haijakuwa rahisi akikumbuka jinsi amepoteza hela kwenye kilimo cha stroberi, nyanya, pilipili mboga (maarufu kama hoho) na kuku.
Kufa moyo, hajawahi kuwazia hilo akihimiza wafanyabiashara kuwekeza kiwango cha pesa ambazo watamudu kupoteza.
Ana wafanyakazi 12 wa kudumu, na kazi inapokuwa nyingi huandika vibarua 20, japo anasema kupata wahudumu wenye maarifa na ujuzi ni vigumu.