Makala

ANA KWA ANA: Amebobea kufuma sweta, kofia akitumia sindano kubwa

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANGU KANURI

KUFUMA sweta, skafu ama kashida kwa kutumia sindano ya kushonea sweta ni ujuzi ambao unaweza nasabishwa na nyanya zetu.

Ni nadra kumpata msichana wa kizazi hiki ambaye anauelewa ufundi huu wa kushona sweta kwa kutumia kifaa hicho.

Sweta zilizofumwa kwa uzi na kwa mkono zimezidisha umaarufu wake haswa nyakati hizi huku wengi wakilinganisha na sweta zilizofumwa kwa mashine.

Safu hii inamwangazia mwanamke mmoja ambaye ufundi huu umekuwa kigezo cha biashara yake huku akihakikisha kuwa anapata fedha zinazomuimarisha maishani.

Tueleze kwa kifupi, wewe ni nani?

GEORGINA: Jina langu ni Georgina Mutsotso. Nina umri wa miaka 32. Mimi ni mama, dada na rafiki na ninapenda sanaa tangu utotoni. Sanaa yangu nainadi katika ukurasa wangu wa Facebook ambao ni Georginah Crafts Afrika.

Mwanadada akiwa amevaa sweta na aina fulani ya kofia. Picha/ Hisani

Nguo zilizoshonwa kwa uzi ni nguo ambazo zilivaliwa kitambo. Je, kilichokushawishi ili urejeshe nguo hizo katika soko la leo ni nini?

GEORGINA: Upekee wa nguo hizo hasa sweta, skafu na kashida ndicho kishawishi changu. Isitoshe, umaridadi wa kushona nguo hiyo kwa mtindo ambao huipa nguo hiyo mvuto zaidi, ndiyo ilinitia moyo wa kurejesha nguo hizi katika soko ya leo.

Sindano ya kufumia, ni wachache walio na ujuzi wa jinsi ya kuitumia. Je, wewe ulijulia wapi kushona kwa kutumia kifaa hiki?

GEORGINA: Nilijua kushona kupitia mtandao wa YouTube. Nilijifunza kutoka video zilizoko pale. Hata ingawa nilijifunza mwenyewe, nilikuwa na ari ya kujua na ari hiyo ikanielekeza katika kufahamu vyema jinsi ya kusokota nyuzi na kuwa na sweta, skafu ama kashida.

Ushoni haswa wa nguo za uzi huhitaji mitindo tofauti ili mauzo yake yawe bora. Je, wewe huhakikisha mitindo yako inawiana na mitindo ya kisasa kivipi?

GEORGINA: Ushoni kama sanaa yoyote ile, huhitaji ubunifu wa hali ya juu. Kwa kuelewa vyema hivyo, mimi hubuni mitindo yangu na kuchora kile ninanuia kabla ya kukichukua kisindano changu na kuanza kushona.

Je, kuna tofauti yoyote kati ya uzi wa hapa nchini na ule unaotoka nje?

GEORGINA: Uzi wa kutoka nje ya nchi ni wa ubora wa hali ya juu ukilinganisha na ule unaotengenezwa nchini. Hata hivyo uzi unaoundiwa Kenya ni wa bei nafuu na hupatikana kwa urahisi kwa hivyo mimi huutumia ili hata mauzo yangu yawe afadhali kwa wateja wangu.

Umaarufu wa nguo za uzi haujavuma. Je ni nini kinachoweza kusisimua umaarufu wake?

GEORGINA: Kwa kutaangaza umaarufu wake kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook ama hata Instagram na pia kueleza umuhimu wa ujuzi wa kushona nguo kupitia kisindano cha sweta kwa umma. Kukubali fasheni ya nguo zilizoshonwa kupitia kisindano hicho na kuzionyesha katika maonyesho ya sanaa kunaweza pia sisismua ari ya watu ya kutaka kununua nguo hizo.

Wengi wanapenda kununua bidhaa za kutoka nje. Je, kwa maoni yako ni kina nani wamechelea katika kufanikisha mauzo ya nguo zilizoshonwa nchini?

GEORGINA: Wananchi sawa sawa na serikali. Wananchi wanapaswa kuamini kazi za washonaji na serikali inafaa kuhakikisha kuwa biashara za washoni zimelindwa kwa kupunguza idadi ya nguo zinazotoka nje ya nchi. Kwa muda sasa rais Uhuru Kenyatta amevalia shati zilizoshonwa nchini ishara ya kubadilisha mtazamo ulio baina ya wananchi.

Ni nguo zipi wewe hushona?

GEORGINA: Mimi hupenda kushona nguo za wanawake sana sana poncho, sweta na kashida.

Kwa siku unaweza kushona nguo ngapi na kwa takriban muda upi?

GEORGINA: Miradi midogo kama kofia, glavu na skafu mimi hushona 6 kwa siku na miradi mikubwa kama sweta moja ya mtu mzima mimi huchukua siku tatu.