ANA KWA ANA: Amerejea kwa fujo!
Na THOMAS MATIKO
MSANII wa Bongo Flava, Ommy Dimpoz karejea kwenye muziki kwa fujo tangu apone upasuaji mkubwa aliofanyiwa kutoka kooni kuelekea tumboni.
Wiki mbili zilizopita Ommy aliwashirikisha Khaligraph Jones na Redsan kwenye kazi yake mpya Kata. Kulingana naye, amerejea kwenye gemu kwa fujo.
Kuna video ilizua gumzo sana mitandaoni ambapo Akothee akiwa kavalia bikini anaonekana akikunengulia usoni mkiwa kwenye bwawa la kuogelea, hebu tuweke sawa?
Ommy: Tulikuwa tumealikwa kwenye pati fulani kule Watamu ambapo jamaa alikuwa amefungua klabu na alitaka tupige shoo pale. Kabla ya hapo tukawa tunajivinjari na Akothee si nyie mwamjua na mambo yake, halafu kipindi hicho ndio nilikuwa nimeachia ule wimbo wa Kata. Tulikata tu ila hatukukata zaidi ya pale.
Kwa hiyo hamna la ziada lililotokea?
Ommy: (Akicheka) Hamna kabisa sema watu wengi wananitania kwamba lazima Ommy nilikata kwa kile walichokiona. Wananiambia nimeshasoma katiba. Akothee ni mshikaji halafu kwa umri wake na majukumu yake na bado anapata muda wa kujichangamsha, ni mtu mpoa sana na mchangamfu.
Mara ya mwisho umekuwa kwenye mahusiano?
Ommy: Miaka miwili iliyopita, toka kipindi hicho nimekuwa tu nikijirusha na kufurahia maisha.
Katika maisha yako ya mahusiano ya kimapenzi umejifunza nini?
Ommy: Sio yangu tu lakini pia ya watu wengine tunaowaona. Kwangu mimi masuala ya mapenzi ni tofauti kwa kila mtu. Unaweza ukampata mtu kawa kwenye mahusiano kwa miaka 10, 15 bila ya kuingia kwenye ndoa kisha wakaachana na mwezi mmoja akaingia kwenye uhusiano mwingine na ndoa juu. Mahusiano ni suala la utulivu wa kiakili tu. Kuna wengine wanakuwa na watu wanawavumilia wakiwa na mawazo kwamba tutakapoingia kwenye ndoa, atabadilisha baadhi ya tabia ninazozivumilia kwa sasa na ambazo zinanikera. Hili huwa kosa, unategemea kumbadilisha mtu.
Wewe kama Ommy, unafikiri itakuchukuwa muda gani kabla ya kuingia kwenye ndoa?
Ommy: Kiukweli siwezi kusema na nimekuwa nikipata presha kutoka familia kwamba umri unakwenda, tuachie wajukuu na vitu kama hivyo. Lakini bado naangalia angalia chini ya maji, hivyo vitu vitatokea inawezakana hata mwisho wa mwaka.
Kuna pia picha zinazoashiria ni kana kwamba umekuwa na ukaribu sana na Zari siku za hivi karibuni?
Ommy: Sio kwamba tuna ukaribu huo, sema unapokuwa kwenye gemu maisha ya kukutana na huyu na yule inakuwa ni kitu cha kawaida. Kuna mradi ambao alikuwa anaushughulikia Akothee na ndio uliotukutanisha sababu wale ni marafiki wakubwa.
Zipo tetesi kwamba unalenga kumuumiza mshikaji wako wa zamani Diamond Platnumz ambaye ni EX wake?
Ommy: Hapana wala siko huko kabisa. Akothee na Zari wana mradi wa kuwawezesha wanawake na wamenihitaji kuwasapoti kama mtumbuizaji.
Kwa hivyo hata ile video ya Zari akiwa anaimbaimba wimbo wa kwako mkiwa naye kwenye dizaini za mapozi hivi sio ishu?
Ommy: Pale tulikuwa tunajifurahisha tu lakini si pia wajua mtu anapoingia kwenye mitandao huja na mawazo yake. Anaweza akaona ameunganisha doti zote wakati sivyo.
Lakini kuna watu watahoji kuwa hii ni tabia yako sababu kuna wakati pia ulionyesha kuwa na ukaribu na Wema Sepetu baada yake kuachana na Diamond?
Ommy: Mimi nimeanza kumjua Wema Sepetu kabla ya Diamond kwa hivyo sisi tumekuwa washikaji wa muda mrefu. Na nitakuambia kabla wao hawajaingia kwenye mahusiano, wote walikuwa washikaji zangu.
Ikiwa hivyo, mbona inaonekana ni kama kuna ishu kati yako na Diamond, zamani mlikuwa vizuri tu ila sio tena?
Ommy: Sipendi kuzungumzia hii ishu sababu ya kuishi kutafsiriwa vibaya lakini kitu ambacho ninaweza kusema ni hichi, sina tatizo na mtu yeyote kabisa na wala D. Hata ikitokea fursa tufanye kazi tena, wala sitakuwa na tatizo.
Kuna tetesi kwamba Gavana Joho kakununulia gari?
Ommy: Alianzisha Ney Wa Mitego kwenye wimbo wake, ila ile ndio staili yake ya kusaka riziki. Anapenda kuwachanachana watu ila sio kweli, nilishamzoea ndio staili yake ya muziki. Halafu sio kwamba kaniimba mimi pekee, kawataja na watu wengine kibao. Ni hulka yake.
Uhusiano wako na Gavana Joho pia umezua gumzo. Juzi kuna msanii katoa wimbo akimshtumu Joho kuwa Gavana wa Kibongo kutokana na ukaribu wake na wasanii wa Bongo, hili unalichukuliaje?
Ommy: Mwanzo tusiishi kwa chuki, hatuwezi kuishi hivyo. Kingine huwezi kumpangia mtu marafiki. Inawezekana mimi tukikutana inakuwa ninakujali zaidi kiasi cha yule anayehisi ndiye anayestahili kuwa karibu na wewe.