ANA KWA ANA: Baada ya kutoka jela, sasa arejea kivingine
Na THOMAS MATIKO
BAADA ya kutoka jela kule Bongo, Joe Kariuki, Afisa Mkuu Mtendaji wa Candy n Candy, karudi tena kwenye gemu.
Utakumbuka miaka sita iliyopita, Kariuki alianzisha lebo ya Candy n Candy Records na kuwasajili mastaa wakubwa kama vile Mr Nice, Baby Madaha, Fat S miongoni mwa wengine. Hata hivyo alifunga lebo hiyo miaka miwili baada ya kupata hasara.
Kilichofuatia ni yeye kukamatwa Julai 2017 na kutupwa jela kwa kifungo cha miaka saba kule Arusha,Tanzania kwa madai ya kumtapeli mfanyabiashara mmoja Sh13.3 milioni.
Aliachiliwa mwezi uliopita baada ya kushinda kwenye rufaa na sasa amerejea kwenye gemu kwa kuzindua tamasha ya Amsha Mama Festival. Safu hii ilikutana naye maeneo ya Naivasha na kupiga stori.
Baada ya kufunga lebo ya Candy n Candy kwa nini uliamua kuhamia Tanzania?
Kariuki: Wala sikuhamia Tanzania. Nilichofuata kule ni mishe mishe za kibiashara. Wajua baada ya muziki kuzengua nilionelea bora nijihusishe na biashara zingenezo.
Hiyo ina maana kuwa mawazo yako kwenye biashara ya burudani hayapo tena?
Kariuki: Hapana. Bado nipo kwenye ulingo wa burudani ila safari hii nimekuja vitofauti kabisa. Candy n Candy ya sasa sio lebo tena ambapo tuliwasaini na kuwasimamia wasanii, sasa hivi tunajihusisha zaidi na uandaaji wa shoo kama hiyo ya Amsha Mama Festival itakayofanyika Novemba kule Tanzania na Nairobi, kuwasherehekea kina mama.
Lebo ya Candy n Candy ilipoanza ilionyesha dalili ya kufanya vizuri sana na hata kuwa gumzo, mlikosea wapi?
Kariuki: Tulipoanza, tulikuwa na matumaini kuwa tungetengeneza pesa kutokana na soko la burudani Kenya na Ukanda huu wa jumla. Hilo ndilo lilikuwa kosa la kwanza, kwa sababu hatukugundua kwamba soko la muziki lilikuwa bado linakua.
Kosa la pili ni kwamba tuliishia kuwasajili masupastaa kama Mr Nice, Baby Madaha ambao wote walishindwa kuonyesha kiwango na hata uwezo wa kufanya kazi ili kuvutia shoo. Mwisho wa siku tukagundua ni hasara tu na kuamua kuhamishia Candy n Candy katika biashara zingine.
Ni hasara ya kiasi gani unayozungumzia hapa?
Kariuki: Siwezi kutaja taslimu, ila kwa makadirio hesabu hiyo ilikuwa zaidi ya Sh10 milioni nilizowekeza katika lebo na zote zikazama.
Sasa Candy n Candy ikiwa imerudi safari hii ikijikita kwenye uandaaji wa shoo na tamasha, kuna tofauti gani na usimamizi wa lebo?
Kariuki: Tofauti ni kubwa sana. Kwenye lebo, gharama ya matumizi ni kubwa mno sababu ya matukio ya kila siku. Cha pili, ukikosa kumsaini msanii sahihi mwenye uwezo wa kuvutia soko, basi hesabu tu hasara.
Julai 2017, miezi tu baada ya kufunga lebo, na kuihamishia kwenye biashara zinginezo, ulikamatwa Tanzania na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba kwa kumlaghai mfanyabiashara mmoja Sh13.3 milioni. Unasemaje?
Kariuki: Mwanzo sio kweli na ndio sababu leo hii nipo huru. Yalikuwa ni masuala ya kibiashara tu. Nilitofautiana na mwenzangu kisha akaamua kuniseti ili aweze kuipata dili hiyo. Alichokifanya ni kushirikiana na matapeli wenzake kule Tanzania kuhakikisha nafungiwa kule ndiposa aweze kuiwahi dili hiyo tuliyokuwa tukiipambania hapa nyumbani.
Ina maana skendo hiyo haikutokea Tanzania?
Kariuki: Ilitokea hapa nyumbani Kenya, ila kwa kuwa jamaa alikuwa tayari anafahamu ninazo biashara zingine Tanzania, akafanya mpango kwa ushirikiano na wenzake Watanzania, kuhakikisha napatwa na tuhuma hizo za ulaghai nikiwa kule kwenye mishe mishe zangu. Aliingia gharama kubwa na najua alijipongeza nilipofungwa.
Mahakama ya Arusha ilikupata na hatia na kukuhumu kifungo cha miaka saba?
Kariuki: Na nilipokata rufaa, kifungo hicho kikatupiliwa mbali kwa ukosefu wa ushahidi. Hata kwenye maamuzi ya rufaa, jaji wa mahakama kuu ya Arusha alimshangaa hakimu aliyenihukumu miaka saba kwa vipengele alivyotumia wakati hapakuwepo na ushahidi.
Rufaa ilichukua muda gani?
Kariuki: Nashukuru iliharakishwa ingawaje nilikaa mule sana nafikiri mwaka na miezi saba.
Maisha yalikuwaje nyuma ya nondo?
Kariuki: Magumu kinoma mzee. Niliodhania ni marafiki hapa nyumbani wakanitosa. Kwa kipindi chote walionijulia hali ni familia yangu tu na mfanyabiashara Don Bosco niliyemkuta kule na akanisaidia sana kabla yake kuachiliwa.
Pia nikiwa jela, niliugua na kufanyiwa upasuaji mara mbili. Ninawashukuru Watanzania kwani licha ya kuwa mahabusu, walinionyesha utu.
Ukiwa jela biashara ziliendeshwa na nani?
Kariuki: Nyingi zilisambaratika. Mwanzo Tanzania nilikuwa nimepokonywa mali kadhaa likiwemo jumba ninalomiliki kule Dar, magari kadhaa. Zote hizo zimerejeshwa baaada ya kushinda rufaa. Kenya nilipoteza kila kitu ikiwemo afisi yangu na mazagazaga yote mule ndani. Ilifungwa kutokana na deni kubwa ya kodi ambayo haikuwa na wa kuilipia nikiwa jela. Nikikadiria niliingia hasara ya zaidi ya Sh7 milioni.
Kinachofuata kutoka kwa Candy n Candy?
Kariuki: Kwenye burudani, tuwe tayari kwa shoo kibao tutakazoziandaa kuanzia na Amsha Mama Festival. Tamasha hii imechochewa na Amsha Mama Initiative ambao ni mpango niliouanzisha wa kutoa mkopo wenye riba ndogo kwa kina mama wa kipato cha chini. Kwenye mchakato huu nimeshirikiana na taasisi ndogo ya utoaji mikopo iliyosajiliwa na serikali, Palsunite Capital Ltd.