ANA KWA ANA: ‘Kama mimi mchepuzi, mbona hatuachani?'
Na THOMAS MATIKO
SAMUEL Muraya afahamikaye na mashabiki wengi kama DJ Mo ni mmoja wa watumbuizaji maarufu wa injili hapa nchini.
Jina lake ni kubwa na hata ushabiki wake vile vile hasa ikizingatiwa kuwa ana zaidi ya wafuasi milioni moja kwenye Instagram.
Hicho ni kitu kikubwa katika dunia ya sasa.
Lakini pia, DJ Mo ni mume wake mwanamuziki Size 8 aliyeamua kujitosa kwenye nyimbo za injili na kuachana na za densi baada yao kuoana.
Katika kipindi cha hivi karibuni, DJ Mo ambaye pia huwa mtangazaji wa kipindi cha injili Crossover 101 kwenye runinga ya NTV amehusishwa kwenye skendo kibao ikiwemo michepuko.
Safu hii iligongana naye kwenye hoteli moja ya kisasa katika pitapita za mjini Nairobi na kuchonga naye kama hivi;
Wewe ni mmoja kati ya maceleb wanaopapatikiwa na kampuni mbalimbali kutangaza bidhaa zao. Inahitaji nini kufikia levo hizo?
DJ Mo: Kile unachokifanya na kikawa na athari nzuri kwa jamii ndio kitu cha muhimu. Kwa mfano mimi ni DJ na ninachokifanya kimeondokea kupendwa na wengi na katika hilo nimeweza kuwa na ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii. Brandi hizi zinapohitaji mtu wa kutangaza bidhaa zao, huangalia ufuasi ulionao kando na wasifu wa kazi machoni mwa jamii.
Kwa sasa upo kwenye mkataba na Oppo kutangaza simu yao mpya F11Pro na F11, dili hii uliipataje na inakupa kiasi gani cha mtonyo?
DJ Mo: (Hahaha) Unanichimba sasa. Ningeweza kukuambia ni kiasi gani cha fedha ila mkataba niliosaini unanifunga kutozungumzia hivyo siwezi kujiweka kwenye hatari hiyo ya kupoteza riziki.
Kuhusu nilivyoangukia hii dili, ni kwamba toka hapo nyuma nimekuwa na Oppo, nafikiri kwa miaka mitano sasa.
Naamini nimekuwa nikiwafanyia kazi nzuri na kuwaboreshea mauzo na ndio sababu ya wao kuendelea kudumisha uhusiano wetu kila wanapoingiza mzigo mpya sokoni.
Hivi majuzi umefanya kituko kwa kuitangaza simu hiyo ya Oppo kwa kutumia simu ya kampuni nyingine kutwiti. Itakuwa uliwakera mabosi wako?
DJ Mo: Mwanzo sio mimi niliyeposti hiyo Twiti. Nina timu inayoendesha akaunti zangu za mitandaoni na ndio waliokosea na ni kwa sababu sikuwa nimewapa maaagizo yanayotakiwa. Niliwaelewesha mabosi na nashukuru waliichukulia poa.
Tasnia ya muziki wa injili kama vile imeoza, kila kukicha ni skendo tu.
DJ Mo: Watu waache kuhukumu wadau wa tasnia hii. Hakuna aliyemlazimisha mtu kujiunga na tasnia ya injili, huwa ni mwito na mtu anapoamua kujitosa humo huwa anao uelewa wa anachotakiwa kufanya.
Hujajibu swali?
DJ Mo: Matatizo yapo kwenye tasnia zote sema za injili zinaamulikwa sana. Sisi pia ni wanadamu kama wengine na kukosea ni sehemu ya maisha yetu pia.
Mapema mwaka 2019 wewe na mkeo Size 8 mlishtumiwa vikali kwa kuwasapoti wasanii wa injili ambao ni washikaji zenu Hopekid na DK Kwenye Beat baada yao kushtumiwa kumwambukiza binti mmoja maradhi ya zinaa. Iliwahusu nini?
DJ Mo: Wale ni kama wadogo zetu wajua. Halafu kingine mimi sikufanya lolote. Ni mke wangu ambaye alirekodi mahojiano yake na DK, lengo likiwa ni kumtaka ayakubali makosa yake ila utafsiri wa wengi ukawa ni kwamba anamsapoti. Mimi mwenyewe nilitwiti na kusema haki itendeke na DK Kwenye Beat lazima akiri makosa yake.
Umewahi pia kushtumiwa kwa kuwaomba wasanii chipukizi mkwanja mnene ili ucheze nyimbo zao katika kipindi chako?
DJ Mo: Huo ni uongo mtupu, sijawahi kumwiitisha msanii yeyote hela kucheza muziki wake. Kama muziki ni mzuri nitaucheza na kama hauridhishi nitaachaana nao. Isitoshe, si wafahamu tena, mti wenye matunda ndio hupigwa mawe.
Ndoa yako pia imemulikwa sana ukidaiwa kuwa mchepukaji hatari?
DJ Mo: Tatizo la Wakenya ni kwamba wao huamini chochote wanachotupiwa, wanachosahau ni kwamba sisi ndio huwapakulia tunachotaka wao wafahamu. Kama mimi ni msaliti wa ndoa, mbona basi na mke wangu bado tupo pamoja?
Ndoa yenu imedumu kwa miaka mingapi sasa?
DJ Mo: Tunaingia mwaka wa sita sasa.
Kwa kifupi unaweza kuelezea ndoa yako ipoje?
DJ Mo: Ndoa ni kitu kizuri sana katika maisha ya yeyote yule hasa unapomwoa rafiki yako. Zipo changamoto zake ila kikubwa ni maelewano na kuvumiliana.
Ulimwoa rafiki yako wa karibu ila Wakenya hawakushuhudia ndoa hiyo?
DJ Mo: Kama nilivyotangulia kusema Wakenya ni wambea sana. Wanachofahamu kutuhusu sicho. Ndoa tulifanya tena ya kufana kanisani na picha zipo, tunazo. Ukifika muda mwafaka tutazichapisha.
Nashangaa mbona iwe ya siri na ndio sababu tetesi kwamba mliifungia kwenye afisi za Mwanasheria Mkuu zimepata nguvu.
DJ Mo: Shauri zenu, sawiri mtakavyo ila kama nilivyokuelezea hapo awali ndoa tulifanya tena ya ibada. Ipo siku tutawasuta kwa kuwapiga sapraizi tukapoachia picha hizo. Nitahakikisha unakuwa mtu wa kwanza kuzicheki.