• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
ANA KWA ANA: Kendi, msanii aliyetesa na kupotea, sasa arejea

ANA KWA ANA: Kendi, msanii aliyetesa na kupotea, sasa arejea

Na THOMAS MATIKO

KUNA kipindi Calif Records; lebo inayomilikiwa na rapa lejendari Jua Cali pamoja na produsa mkongwe Clemmo, ilikuwa nd’o kusema ndani ya +254 yaani Kenya.

Kila msanii chipukizi alitamani kusainiwa pale, kwa kuwa wale waliokuwemo kule walionekana kufanya vyema. Kipindi hicho wasanii wa kike walikuwa wachache sana na wale waliokuwepo waking’aa walikuwa chini ya Calif Records.

Alikuwepo marehemu Lady S, Rat-at-tat, Choku, Kendi miongoni mwa wengine.

Baadaye nyota ya wasanii hawa wote wa kike ilififia kwa sababu moja au nyingine.

Baada ya ukimya wa miaka mingi, mmoja wao Kendi kaamua kuifufua tena taaluma yake na hivi ndivyo alivyotiririka kwenye safu hii:

Ukimya wako umekuwa wa muda gani toka upotee kwenye gemu?

Kendi: Nafikiri itakuwa ni miaka sita hivi kwa sababu ndio mara ya mwisho niliachia wimbo.

Chanzo na kiini cha kupotea kilikuwa nini haswa?

Kendi: Mahangaiko ya huu muziki tu wakati tunaanza. Nilifanya kazi na lebo nyingi Ogopa, Calif hadi Grand Pa ila sikuwa naona faida. Mwenyewe sikutaka kurudi kabisa kwenye fani unajua ni kwa nini, tulikuwa sisi ni watu maarufu sana ila kwa wakati huo tumesota kinoma. Usimamizi tuliokuwa nao haukuwa mzuri, hatukuwa na maamuzi katika taaluma zetu na vitu hivi vilichangia sana kutuangusha. Tulikuwa ni watumwa wa hizi lebo na nd’o maana nilichoka.

Baada ya kuingia mitini ulikwenda kupiga mishe mishe zipi?

Kendi: Sikupotea kwenye sanaa kivile sema safari hii sikuwa naonekana kwenye mashoo ila nilisalia katika muziki. Nilichofanya ni kwamba niliuza moja ya magari yangu na kuanza kununua vifaa vya kisasa vya bendi na kuanzisha laivu bendi yangu na hapo nikaanza kuwa nikipata shoo kubwa kubwa kutoka kwa Mashirika na makapuni mbalimbali pamoja na watu binafsi. Kwa mfano AP Insuarance walikuwa wateja wangu wakubwa miongoni mwa wengine na ndivyo niliendelea kuunda hela zangu.

Baada ya ukimya wa miaka mingi ulirejea kwa kuachia kazi ‘Into You’ uliyomshirikisha staa mwingine aliyepotea Vinnie Banton, mbona ukaamua kurudi baada kipindi kirefu mno cha miaka kadhaa?

Kendi: Ni kwa sababu nimepata menejimenti mpya kabisa Mainswitch ambayo imenisaini. Nia yangu haikuwa kurudi kama mwanamuziki solo ila baada yao kunifuata na hata kunihamishia karibu na makao makuu ya lebo yenyewe nikaonelea sawa tu acha nijaribu tena. Kuhusu kazi hiyo, ni wimbo niliourekodi zamani kidogo katika studio za Everblazing ila sikuwa na hela ya kuachia, baadaye Mainswitch waliponichukua, ulifanyiwa ukarabati na ikawa hiti sikutegemea kupata mapokezi aina hiyo kwa kweli.

Wimbo huo ni wazi kwamba umefufua vipaji viwili vikali vya zamani, Vinnie mtazamo wake katika hili upoje?

Kendi: Kwa kweli nia yake haikuwa kurudi kwenye gemu kabisa ila baada ya mapokezi ya wimbo huu mwenyewe amefurahia na kupenda. Hakuamini kuwa baada ya ukimya huo angetokea kupendwa bado, tumehudhuria matamasha kadhaa naye na amehisi kuwa bado watu wanamtambua hivyo ni kitu anachokifanyia kazi.

Kurejea kwako kutakuwa na tofauti gani au ni sawa na moto wa gazeti?

Kendi: Nimerejea vitofauti kabisa. Mwanzo nipo chini ya lebo tofauti inayonipa uhuru wa kufanya mambo nitakayo mimi kuhusiana na mchango wangu wa muziki. Zamani nikiwa Calif au Ogopa walikuwa wanalipa mtu haswa Sanapei Tande kuniandikia nyimbo; hawakuwa wakiniruhusu nijiandikie kazi zangu ila sasa nina uhuru huo na ndio maana umeona Into You imefanya vizuri. Hata studioni naona watu wanapendelea zaidi nyimbo nilizoandika mwenyewe ukilinganisha na zile nilizoandikiwa.

Huu upepo wa Gengetone umeupokeaje?

Kendi: Nafikiri ni mzuri umesaidia kuangamiza muziki wa nje na kupromoti zaidi wa kwetu. Gengetone imenikumbushia enzi zetu kipindi tukianza, muziki wa nyumbani ndio uliokuwa ukichezwa sana. Nafurahia tumerudi huko sababu hii itatufungulia wengi wetu.

Kando na usanii, bado wewe ni mke wa mtu?

 Kendi: Hahaha! Wewe nawe kunaye anayetaka kunioa? Ndoa hiyo ilishavunjika zamani, kwa sasa nipo tu.

  • Tags

You can share this post!

Balozi wa Amerika akwama kwenye lifti

Wezi wa kuku waua familia nzima ya watu wanne

adminleo