Makala

ANA KWA ANA: Mshonaji aliyezamia katika kuwang’arisha wanaume

September 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WANGU KANURI

USHONI wa mavazi kimtindo ni biashara ambayo kwa sasa imenoga japo washonaji wengi hulalamikia kutoaminiwa na Wakenya hali inayofanya iwe vigumu wao kuimarisha biashara zao.

Aghalabu washonaji wengi wamezoea kushona nguo za kiume, kike na hata za watoto hii ikiwa na maana kuwa ni nadra umpate fundi aliyejitolea na kuangazia kazi yake katika nguo mahususi ya jinsia moja.

Mapema wiki hii mwanadada Valerie Nyamwaya alieleza Taifa Leo kwamba upekee wa shati ndicho kishawishi kikubwa katika kazi yake.

Tueleze kwa kifupi, wewe ni nani?

VALARIE: Valerie Nyamwaya ni mama anayependa kutangamana sana na wanafamilia na marafiki zake. Isitoshe, ninapenda kusoma na kupiga gumzo nipatapo muda. Kikazi mimi ni mbunifu wa mitindo ya mavazi na pia mwanzilishi wa Afrivazi.

Ni nini kilichochochea Afrivazi?

VALARIE: Afrivazi ilianzishwa kama pahala pa wabunifu wengi wa mitindo ya mavazi. Ndoto yangu ilikuwa kuwa na pahala ambapo wabunifu wa mitindo ya mavazi wangejumuika na kupata fursa ya kuuza nguo zao kijumla na kuonyesha kazi za mikono yao kwa wateja. Mtazamo huu ulibadilika huku Afrivazi ikizamia katika kubuni mitindo ya mavazi hasa mashati ya wanaume. Nilimakinika katika mashati ya wanaume kwa kuangalia mchango chanya ambao wanaume huchangia katika jamii. Isitoshe, mimi kama mwanamke wanaoniongoza na kunisaidia sana huwa wanaume.

Washonaji wengi hushona nguo mbali mbali; za kike, za kiume na hata watoto. Mbona ukachagua mashati ya wanaume pekee?

VALARIE: Hii ni kwa sababu nimevutiwa na umaridadi wa mashati hata kabla nianze kufanya kazi hii. Upekee wa shati lililoshonwa vizuri hunivutia sana ndiposa nikajitosa katika ulingo wa ubunifu wa mitindo ya mavazi ili hata mimi nichangie. Isitoshe, ninafahamu kuwa mashati wanayovaa watu wakienda kazini yanaweza kuwa na mvuto wa kipekee na hata yakavaliwa wikendi wakati ambapo watu wanajipumzisha na marafiki na wanafamilia wenzao.

Je wewe hutoa wapi mitindo yako?

VALARIE: Mimi hutoa mitindo yangu kupitia nguo za wanawake ambazo hunisaidia kupata mitindo ambayo mimi hubadilisha na kushona mashati ya wanaume. Vile vile, mimi hutoa mitindo yangu kutoka nguo zilizoshonwa katika nchi za Afrika Magharibi kwani wateja wangu wengi hupendezwa na mitindo hiyo. Ninapenda pia mitindo ya Kurta ya Wahindi. Kwa kuwa mashati niliyoshona yana hadithi nyuma yake, mimi huangaza macho yangu kwingi ili kupata mtindo bora na ulio wa kipekee.

Changamoto unazopitia katika ushoni wako ni?

VALARIE: Kuaminiwa na wateja wangu asilimia 100 na wao kuniruhusu niwaeleze ni nini kitakachowafaa na nini hakitawafaa ili nisiwe tu nashona shati sawa sawa na lile waliloliona bali waniruhusu nishone mashati yao kwa mitindo mipya na ile itakayowafaa.

Upekee wa nguo ndiyo kigezo kikuu cha ufanisi. Je, wewe huangaza nini cha pekee unaposhona mashati ya wanaume?

VALARIE: Kulingana na uzoefu wangu katika kubuni mitindo ya mashati ninaweza kumweleza mteja wangu kile kitakachomfaa na kile kitakachomfanya ang’ae. Pili kwa wateja ambao hukubali mitindo mpya na niliyoishona kwa upekee wa ubunifu wangu, mimi huwachagulia rangi na vitambaa vya shati zao ambazo najua zitawiana na wao binafsi.

Wewe hutumia mbinu na majukwaa gani kuwafikia wateja?

VALARIE: Nimeweza kuonyesha kazi yangu kupitia mtandao wa kijamii na katika ukurasa wa Facebook na hata Instagram ni Afrivazi. Mapema mwaka huu ndivyo niliamua kulipia ads za kazi yangu na nikachapisha katika vikundi mbali mbali katika mitandao ya kijamii.

Umejivunia nini kutokana na ushoni wako?

VALARIE: Kuwa na watu ambao wataangalia kazi yangu na wao kupenda mitindo na ubora wa kazi yangu hiyo hunifanya nijivunie sana. Isitoshe, nimewapata watu ambao wameangalia kazi ambayo mimi nimefanya na wakashawishika kuwa nguo zinazoshonwa nchini ni za hali ya juu pia.

Mwanamume akiwa amevaa shati. Picha/ Wangu Kanuri

Mkurupuko wa janga la corona umeathiri biashara nyingi nchini. Wewe Covid-19 imekuathiri vipi?

VALARIE: Kazi ilikuwa imeanza kupungua lakini kile ambacho kilinisaidia ni ushoni wa maski ili nisije nikaangamia kibiashara. Kwa hivyo, nilijiunga na washoni wenzangu katika soko ya Makina iliyoko Kibra na tukapata oda za kushona maski nyingi. Janga hili la corona limenisaidia kutumbukiza neti zangu za ushoni kwingine na nikaweza kushona shati za mikono mifupi na mifuko ya kubebea suti.

Serikali inafaa kuwafanyia nyinyi?

VALARIE: Katika eneo la Makina, Kibra, washonaji wengi huwa na kazi zinazovutia lakini wengi wao hawajafikia hatua ya kufurahia jasho lao. Wakati huu wa janga la corona, serikali ingewapa washonaji hawa wadogo kandarasi za kushona maski kwa wingi lakini hiyo haikuwa hali. Hata ingawa kuna washoni walionufaika kutokana na zabuni hiyo, malipo waliyopata ni peni chache tu huku ikiwalazimu wengi kufunga maduka yao na kuenda mashambani.

Wosia wako kwa wanawake wanaohofu kujitosa katika kazi za kujiajiri ni upi?

VALARIE: Biashara yoyote ile ina changamoto zake lakini pia inamfaa mtu sio tu kwa malipo bali hata kumwezesha kujijua vyema. Kwa wanawake wanaotaka kujitosa katika kazi za kujiajiri, ni sharti wafahamu wanapaswa kuwa karibu na watu ambao watawasaidia pale ambapo watahitaji msaada wowote.