• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
ANA KWA ANA: Mwaka 2019 alikuwa anauguza koo, yukoje?

ANA KWA ANA: Mwaka 2019 alikuwa anauguza koo, yukoje?

Na THOMAS MATIKO

UTAKUMBUKA kuwa mwaka 2019 msanii wa injili James Mutheremu al-maarufu Jimmy Gaits alikumbwa na tatizo la koo na kumfanya ashindwe kuimba.

Madaktari wa humu nchini waliomfanyia uchunguzi wakamshauri atahitaji kufanyiwa upasuaji. Hapo akaamua kwenda India kukutana na madaktari bingwa walioishia kugundua tatizo la ugonjwa huo lilisababishwa na maradhi yaliyotokana na tumbo lake na wala hakuhitaji kufanyiwa upasuaji. Hapo Gaits akaanza harakati ya kushinikiza serikali kuwakazia madaktari wa humu nchini alioshtumu kwa kuwa matapeli waliotaka kumtoanisha kimfuko bila sababu. Gaits sasa kafunguka mengi.

Mwaka 2019 ulipiga kelele sana mitandaoni kuhusu ugonjwa huu uliokuwa ukikutatiza, tupashe?

Gaits: Miaka mitatu iliyopita nilianza kupata matatizo ya koo langu. Nikajaribu kununua dawa kutuliza ila halikupoa. Ndipo nikaamua kuanza kwenda kwa madaktari ila hakuna aliyeweza kubaini kilichokuwa kikinitatiza. Kwa miaka mitatu nikawa nameza dawa tofauti nilizoandikiwa na madaktari tofauti bila ya kupata afueni. Mwishowe nikatumwa kwa daktari mtaalamu wa magonjwa ya koo akanisikiza, akanipa matibabu na bado hayakunisaidia. Nikaenda kwa daktari mwingine ambaye baada tu ya kunisikiza hata bila ya kunifanyia vipimo, akaniambia eti nahitaji upasuaji. Huyo ndiye aliyenishtua ukizingatia kuwa sauti yangu ndiyo inanilisha. Taarifa hiyo kwa kweli ilinisumbua.

Endelea…

Gaits: Nilipomuuliza ikiwa ana uhakika baada ya upasuaji nitaweza kuimba, alinihakikishia kwamba ndio. Ila tayari nilikuwa nishamtilia shaka kwa namna alivyokuwa akinikimbiza.

Kukukimbiza kivipi?

Gaits: Nilikutana naye kwenye kliniki yake na maongezi yake yakawa kwenye masuala ya pesa zaidi ya ugonjwa wangu. Aliniambia kwamba yeye ni mmoja wa madaktari bingwa nchini hivyo hata nikienda kwenye hospitali kubwa, kuna uwezekano mkubwa upasuaji utamwangukia yeye. Hivyo akanishauri anifanyie upasuaji kwenye kliniki yake na ada atakayonilipisha itakuwa kidogo. Hapo nikaingiwa kiwewe, sababu nilichokusudia mwanzo ni kupata ufahamu wa ugonjwa uliokuwa ukinitatiza na kila nilipomuuliza maswali haya, akawa anakwazika. Hapo ndipo nikaamua kusaka suluhu. Hadi nafikia kwenda India, nilikuwa nakohoa damu na koo langu lilikuwa lina maumivu makali sana.

Wazo la India lilikujia vipi?

Gaits: Ni rafiki yangu mmoja aliyenishauri nisake ufafanuzi zaidi India kwa sababu ni moja ya mataifa bora kwenye utoaji huduma za afya. Nilipewa majina ya baadhi ya hospitali za kule ambazo ningeweza kwenda kuchekiwa.

Ulipofika India?

Gaits: Daktari niliyekutana naye aliniambia kwamba sihitaji upasuaji hasa zaidi kwa sababu mimi ni mwanamuziki. Alinihakikisha kuwa ikiwa nitafanyiwa upasuaji wa kooni, basi niwe na uhakika kuwa sauti yangu itabadilika kabisa. Lakini muhimu zaidi, aliniambia hawezi kunifanyia upasuaji bila ya kunifanyia vipimo kujua chanzo. Kwa wiki nzima, ikawa ni shughuli ya kufanyiwa vipimo. Moja ya vipimo hivyo ilihusu kinywa changu, njia ya chakula kuelekea tumboni. Hiki ndicho kipimo kiligundua kuwa chanzo cha matatizo ya koo langu ni tumbo.

Baadaye kulizuka tetesi kwamba utakuwa unaugua kansa?

Gaits: Sio kweli ila daktari aliyegundua lile tatizo aliniambia endapo hali ile ingeendelea kwa miezi sita zaidi, basi ningepatwa na kansa ya utumbo. Kwa maana hiyo kama ningefanyiwa upasuaji, ningepoteza sauti na kisha baadaye kansa inikute.

Upoje kwa sasa?

Gaits: Nimekuwa nikiendelea na matibabu na mambo yamebadilika, sihisi tena maumivu na ndio sababu hata kuimba ninaweza.

Yule daktari aliyependekeza upasuaji umemchukulia hatua gani?

Gaits: Niliwazia sana kumshtaki lakini baada ya kukutana na Wakenya zaidi ya mia kule India na kuona uchungu na magumu waliyokuwa wakipitia kutokana na ishu kama yangu ya kupendekezewa tiba isiyostahili, niliamua nitakuwa mhamasishaji wa jambo hili. Lazima madaktari wawajibike. Na ndio sababu nimekuwa nikiendesha kampeni ya kuitaka serikali iwasukume kwenye hili.

Kuhusu muziki wako je, umeacha kuimba kabisa sababu zipo tetesi kama hizo?

Gaits: Mwanzo kama nilivyotangulia kusema kwa miaka mitatu nilikuwa naugua koo. Pili, tetesi hizo zilianza baada yangu kusema naachia ngoma ya mwisho itakayofunga hatua moja katika maisha yangu, nikihamia nyingine. Tatizo watu waliamua kutafsiri kivingine.

Majuzi Rais aliamrisha kwamba malipo kwa wasanii yawe yakikusanywa na KECOBO (Kenya Copyrights Boards) badala ya hivyo vyombo vingine SKIZA, VIUSASA, MCSK, PRISK na zinginezo ambazo wasanii mumekuwa mkilalamikia zawapunja. Mawazo yako?

Gaits: Mbinu ya Rais naona ni nzuri ila nafikiri itakuwa bora tukipewa uhuru wa kuuza muziki wetu tunapopataka. Kwa mfano mimi nimepata faida sana kuuza muziki wangu ‘Skiza’ nikilinganisha na kwingineko.

You can share this post!

DOMO KAYA: Size 8, DJ Moh kutoza wageni elfu 10 Valentino

KIKOLEZO: Secular ila wanafanya Gospel fire!

adminleo