Makala

ANA KWA ANA: Ni vizuri mpiga gitaa ajue kuambatanisha ufundi wake na mazingira aliyomo

September 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANGU KANURI

MSANII yeyote yule anapaswa kuelewa vyema ala yake ya muziki.

Aghalabu upigaji wa gitaa unamlazimu msanii kufahamu mazingira yake ili apige gitaa kulingana na anavyohisi.

Uzoefu huu unaweza kuimarishwa iwapo wachezaji wa ala za muziki watapanua mtazamo ili wapate maarifa zaidi.

Tueleze kwa kifupi, Leon Ngunjiri ni nani?

LEON NGUNJIRI: Mimi kwa sasa ni mwanafunzi anayesomea taaluma ya uchumi na anayependa sana kazi za Sanaa ikiwemo muziki.

Ulianza lini kucheza gitaa?

LEON NGUNJIRI: Nilianza kucheza gitaa mwaka wa 2011.

Ala za muziki ni nyingi. Kuna tarumbeta, kinanda, baragumu, ngoma na kadhalika. Mbona ukajikita katika kucheza gitaa?

LEON NGUNJIRI: Licha ya kujua kucheza ngoma, gitaa na kinanda, sikuwa na ala yoyote ya muziki niliyojikita kwake lakini kila mara nikicheza ngoma ama kinanda, nilijipata nikikoleza nyuzi za gitaa. Kwa kila mkolezo wa kuambatanisha na wimbo wowote ule, mapenzi yangu kwa gitaa yakawa dhahiri.

Kila uzi hutoa sauti tofauti na ili sauti ya gitaa iwiane na mahadhi ya wimbo fulani, unahitaji bidii na ukakamavu wa kuelewa jinsi ya kukoleza nyuzi hizo. Je, wewe umelenga hili vipi?

Mpiga gitaa Leon Ngunjiri. Picha/ Hisani

LEON NGUNJIRI: Kuelewa mazingira yako wakati ambapo unacheza gitaa kutakufaa kujua ni uzi gani utakoleza na ni upi hutakoleza. Isitoshe, kujikakamua katika kuimarisha ujuzi wako katika kupiga gitaa kutakufaa wakati wa kucheza.

Ni nini cha kipekee katika upigaji wako wa gitaa?

LEON NGUNJIRI: Ninahakikisha ninaleta mahadhi tofauti kisha uwiano wake ili ulete burudani aali.

Ni vipi instrumentals zinaweza kujisimamia?

LEON NGUNJIRI: Kuwa na ari ya kusikiza wachezaji wa ala za muziki waliotutangulia kutamwezesha yeyote kuimarika wakati ambapo anacheza ala yoyote ile ya muziki kwani atajaribu kucheza ala hiyo kama alivyosikia, huku akiweka zingatio kupata sauti inayofaa.

Mpiga gitaa Leon Ngunjiri. Picha/ Hisani

Kila msanii anayecheza ala yoyote ya muziki huwa na kitengo cha nyimbo mahususi ambacho kwacho yeye amebobea. Je, ni mahadhi ya nyimbo zipi ambazo umeimarika katika kucheza?

LEON NGUNJIRI: Nyimbo za Jazz, Blues, Mugithi, Salsa na Rhumba hunivutia sana.

Gitaa sawa sawa na ngoma ni baadhi ya ala za muziki ambazo zimekuwepo kwa muda lakini umaarufu wake haujawahi kusahauliwa. Je, unafikiri sababu kuu ya hili ni ipi?

LEON NGUNJIRI: Muziki na maisha huwiana kwani palipo na maisha pana muziki. Hii ina maana kuwa sababu kuu ya gitaa sawa sawa ngoma kudumu ni kuwepo kwa watu ambao walizibuni njia mbadala za kucheza ala hizi katika kila kizazi.