ANA KWA ANA: ‘Nitapambana na hali yangu hadi kieleweke’
Na THOMAS MATIKO
SIJUI kama utakuwa unamkumbuka msanii Abel Loshilaa Motika aliyefahamika zaidi kwa jina lake la stejini Mr Ebbo.
Alikuwa mmoja wa wasanii waanzilishi wa muziki wa Bongo Flava.
Mr Ebbo alipata umaarufu mkubwa kutokana na staili yake ya muziki aliokuwa akifanya.
Alikuwa ni mwana Hip hop na ili kujitofautisha na wenzake, aliamua kuja na staili yake ya jamii aliyotokea ya Kimaasai.
Kimsingi alikuwa ni rapa wa Kimaasai na hakika alishia kuachia ‘hits’ kadhaa kama vile Mimi Mmasai, Bado, Kamongo kati ya nyinginezo.
Kazi hizi zilifanya vizuri sana katika miaka hiyo ya 2000. Hata hivyo kwa bahati mbaya alifariki dunia 2011.
Toka wakati huo, wametokea wasanii kibao waliojaribu kuiga mtindo wake huo huku wa sasa anayejitahidi kung’arisha nyota hiyo akiwa ni Gregory Onyango aka Baba Yao.
Tayari ameshaachia kazi kadhaa akiwashirikisha wasanii nyota kama Susumila na Dogo Richie. Safu hii ilipata fursa ya kubarizi naye na mazungumzo yalikwenda kama hivi:
Kwa mtu anayekusikiza kwa mara ya kwanza anaweza kufikiri unawakilisha Pwani?
Baba Yao: Na wala siwezi kumhukumu kwa sababu atakuwa amezenguliwa na staili yangu. Isitoshe, kuwahusisha wasanii wa kule kama Susumila, Chikuzee, Dogo Richie katika baadhi ya kazi zangu itakuwa inachora taswira kuwa natokea kule ila ukweli wa mambo ni kwamba mimi ni msanii ninayewakilisha Bonde la Ufa nikitokea Eldoret.
Staili yako ya kuchana kwa ‘lafudhi’ ya Kimaasai, inanikumbushia marehemu Mr Ebbo. Ni kama vile uliamua kuirithi.
Baba Yao: Kuna kipindi nimeishi Namanga kwa muda nikiwa kwenye harakati zangu za muziki. Niliishia kuvutiwa sana na utamaduni wa Kimaasai halafu kutokana na uwepo wa marehemu Mr Ebbo aliyekuwa anachana kwa kwa lafudhi yao, nikaona bora na mimi nijaribu mtindo huo na mpaka sasa nipo.
Wapo wanaoweza kukukosoa kwa kujaribu staili isiyokusitiri ikilinganishwa na Mr Ebbo ambaye ule ulikuwa ni uhalisia wake kutokana na jamii yake, unasemaje?
Baba Yao: Mimi ni msanii na katika usanii, ubunifu ni suala la kimsingi. Isitoshe, jamii ya Kimaasai inafurahia sana inapoona yupo msanii anayejitahidi kudumisha mila zao. Wametokea wengi baada yake Mr Ebbo waliojaribu kuifanya lakini taratibu wamepotea. Kwa mfano alikuwepo Ero Mtu ila sasa kaacha na kujikita kwenye uigizaji, Ole Karai wa Mombasani kawa Mcee kaacha muziki, Kris Eeh Baba na yeye kazama sasa nafikiri nimebakia mimi tu.
Kwa maelezo yako utakuwa ulianza muziki zamani sana?
Baba Yao: Ni zaidi ya miaka 10 mzee toka enzi za Chaguo la Teeniz nimekuwepo kwenye gemu.
Kwa nini umeshindwa kutoka?
Baba Yao: Kipindi naanza muziki kulikuwa na changamoto kibao. Kwangu mimi maprodusa walinizengua sana kila nilipohitaji kurekodi nao na hilo likawa linanifisha morali sema ari ya muziki haijawahi kufa. Enzi hizo walikuwa ni wachache sana.
Kingine ni kuwa, zama hizo sikuwa na mtaji wa kufanya muziki kwa sababu kama ujuavyo uwekezaji kwenye muziki una gharama kubwa. Hivyo ilinibidi nijishughulishe na mambo mengine niweze kupata mkwanja kwanza.
Sasa hivi unaonyesha ari kubwa ya kujisukuma, mbona?
Baba Yao: Ni kwa sababu nimejifunza mengi kwenye safari hii. Nimejua cha kufanya na ni kipi cha kuepukana nacho. Pia Maprodusa wameongezeka tena wazuri ndio maana nimekuwa na ari hii.
Unaonyesha jitihada kipindi ushindani ukiwa mkubwa, utaweza kweli?
Baba Yao: Sifanyi muziki kushindana na yeyote, naamini tasnia ni kubwa na kila mja ana fursa ya kufanya yake, mimi nami napambania fursa yangu.
Bado nashindwa kuelewa kwa nini baada ya miaka yote hii na gharama kubwa ulioingia katika usanii wako, bado unakazania.
Baba Yao: Hili huwezi kulielewa, unapogundua una kipaji, inakuwa vigumu kuacha licha ya changamoto unazopitia.
Ila kwa nini ubakie kuwa king’ang’anizi wakati muziki haujaanza kukulipa?
Baba Yao: Cha kushangaza ni kuwa licha ya kwamba muziki haunilipi kwa sasa, umeweza kunifungulia njia zingine mbadala za kuingiza riziki. Biashara nyingi zangu zinazonipa riziki, zilitokana na njia nilizofunguliwa na muziki. Kwenye gemu hii nimekutana na wadau mbalimbali na kuweza kuangukia dili zingine hivyo nashukuru siwezi kusema muziki umeniacha hoi.
Hii ishu ya MCSK unaizungumziaje?
Baba Yao: Tumekosea kwa kuwaweka pale viongozi wasio wanamuziki. Hawaelewi chochote kile kuhusu sanaa. Kile ni chama cha matapeli. Pesa wanakusanya sana ila wanaofaidi ni wale wasioimba. Wanaendesha ma-Range Rover kisha sisi wanatulipa Sh2,530. Ni dharau sana!
Ila unagundua kuwa mnalalamika sana na wakati kunapokuwa na uchaguzi wa vyeo hivyo wasanii huwa hampo kugombea!
Baba Yao: Pamoja na hayo sifikiri ni haki kwa yeyote yule anayechaguliwa pale kuwatapeli wasanii sababu bila sisi, MCSK haiwezi kuwepo.
Ndio tunaweza kuwa tumekosa mshikamano pengine kutokana na wengi wetu kufa morali, ila wapo wachache wetu ambao hawajafa moyo. Nafikiri baada ya hili, hatuna jinsi ila kufanya mageuzi.