ANA KWA ANA: Ucheshi wamgeuza bonge la staa
Na THOMAS MATIKO
STEVEN Oduor Dede, wengi wakimfahamu kama DJ Shitti ni miongoni mwa wavunja mbavu wanaopiga mkwanja mnene nchini kutokana na ucheshi wao.
Kuna baadhi wanaofurahia ucheshi wa DJ Shitti na pia wapo wale wanaokwazika. Lakini la wazi ni kuwa ucheshi wake umemgeuza kuwa bonge la staa.
Kama ilivyo ada ya safu hii, juzi tuliamua kumvizia DJ Shitti baada ya kutula chenga kwa mwaka mzima na kufanikisha stori hii.
Mwaka mzima kaka ukinizungusha mjini, wanikaushia mahojiano au ni ustaa umekuingia kichwani?
DJ Shitti: Ninajua nimekuzungusha sana ila naomba msamaha kwa hilo. Sema sikufanya makusudi, nilikuwa nimebanwa sana na kazi za kushuti Real House Helps of Kawangware na matangazo mengine. Pole sana.
Leo imekuwaje ukapatikana?
DJ Shitti: Kwa sasa kazi zimepungua, hatushuti tupo kwenye likizo fupi kidogo ndiyo maana nimeweza kupata muda. Samahani lakini naona bado una hasira (Akicheka).
Hivi mpo likizo kikweli au ni ‘Real Househelps of Kawangware’ haipo tena?
DJ Shitti: Hahaha! Acha wewe, mzigo mbona upo ila sema kwa sasa tumechukua likizo kwa sababu mabosi wapo kwenye harakati za mwisho kukihamishia kituo kingine cha televisheni. Hatutakuwa tena KTN na nafikiri ndiyo sababu hujakiona kwa muda.
‘Real Househelps of Kawangware’ kilikusaidia sana kutengeneza jina?
DJ Shitti: Kilinipa fursa ya kuonyesha uwezo wangu sababu toka mwanzoni nilitamani kuwa msanii. Lakini wengi hukiona kipindi tu, ila mimi huwaangalia wadau zaidi nyuma ya pazia walionisukuma.
Hao ndio kina nani?
DJ Shitti: Wapo wengi sana siwezi kumaliza kuwataja. Ila kwa wachache yupo mvunja mbavu Butita aliyenitambulisha kwa mwigizaji na produsa Abel Mutua. Butita alikuwa ameuona uwezo wangu kwa muda sababu safari yangu nilianzia Churchill Raw. Tukiwa kwenye mazishi ya mzee Ojwang ndipo Butita alimwomba Mutua anipe fursa kimzahamzaha tu na ikawa ndiyo hivyo.
Hao tu?
DJ Shitti: Kwa wasanii ndio ila wapo wengine walionisaidia kwa njia moja au nyingine kifedha na vitu kama hivyo. Lakini zaidi watu ambao naamini walinipa msukumo zaidi ni hawara wa Koinange Street.
Hawara wa Koinange, umenipoteza?
DJ Shitti: Nilipohamia jijini Nairobi 2013 marafiki wote na jamaa niliokuwa nikiwafahamu walinikimbia. Sikuwa na pa kuishi nikawa nalala mtaani. Pale Koinange nilipafanya makao na ndiyo nilikutana na hawara mmoja kwa jina Akshe aliyenitambulisha kwa wenzake. Baada ya kuwapa stori yangu waliamua kunipa makao kwenye nyumba waliyokuwa wakiitumia kama chumba cha kuwapeleka wateja wao. Pale ningelala kipindi hawana wateja na hata kubadilisha nguo, kutwa ningeraukia ‘auditions’ za Churchill Raw au zile za Kenya National Theatre. Ndiyo yalikuwa maisha yangu hayo.
Enhee?
DJ Shitti: Kikubwa zaidi ukiachana na makao waliyonipa, ni maneno waliyokuwa wakinichoma nayo. Siku zote walinisisitizia nisithubutu kurudi nyumbani kwa shida, nipambane na hali hapa mjini hadi siku nitakayotoboa. Kweli siku hiyo ilitimia na hawara hao nawaona kama familia yangu.
Hii ina maana huwa unawasiliana nao?
DJ Shitti: Wakati natoka nilipoteza mawasiliano nao kwa sababu kipindi kile sikuwa na uwezo wa kununua simu ila nashukuru baadhi yao wamenisaka kwenye DM zangu na nimeweza kuwasiliana nao.
Mawasiliano tu kwa watu unaowaita familia?
DJ Shitti: Nimewasaidia kwa kweli sema siwezi kuitangaza lakini hata zaidi nataka kuirudishia shukrani jamii kwa kuwasaidia hawara wa mji huu. Ile daima itasalia kuwa familia yangu. Nipo kwenye harakati ya kuanzisha kampeni ya ‘Okoa Dada Mtaani’ ambayo nalenga kuhamasisha jamii kuhusu dhana potovu kwamba wale ni viruka njia. Lakini pia kampeni hiyo itakuwa ya kusaka ufadhili wa kuwawezesha hata ikiwa ni kuwapa kozi au kuwapa mtaji wa kuanzisha biashara ambazo zinaweza kuwaondoa mtaani. Najua sio kazi rahisi ila nitajaribu.
Kwa dili kama ya Sh15 milioni ulilopiga kuwa balozi wa Star Times, mbona kibarua chepesi hicho?
DJ Shitti: Hehehe! Umeanza mzaha sasa. Nashukuru kwa dili kama hizo kwamba zimeweza kunibadilishia maisha. Nasaidia ninakoweza, na pia usisahahu kwamba nina familia yangu kubwa ya mama na baba pamoja na ndugu zangu ambao wananitegemea pia.
Mwenyewe una familia ya kwako?
DJ Shitti: Si hiyo nishakuelezea.
Ninachouliza ni kwamba, umeoa au unaye mchumba?
DJ Shitti: Kwa ustaa huu mzee, imekuwa vigumu kuwa na demu. Wanakuja wakinikimbia kwa sababu hawaielewi kabisa kazi ninayoifanya. Ila najaribu tu!